The chat will start when you send the first message.
1Kwa hiyo, kwa kuwa tuna huduma hii kwa rehema za Mungu, hatukati tamaa.
2Lakini tumekataa mambo ya siri na ya aibu; hatufuati njia za udanganyifu, wala kulichanganya neno la Mungu na uongo. Kinyume cha hayo, tunadhihirisha kweli waziwazi na kujitambulisha wenyewe kwenye dhamiri ya kila mtu mbele za Mungu.
3Hata nayo Injili yetu kama imetiwa utaji, ni kwa wale tu wanaopotea.
4Kwa habari yao, mungu wa dunia hii amepofusha akili za wasioamini, ili wasione nuru ya Injili ya utukufu wa Kristo, aliye sura ya Mungu.
5Kwa maana hatujihubiri sisi wenyewe, ila tunamhubiri Yesu Kristo kuwa ni Bwana, na sisi ni watumishi wenu kwa ajili ya Yesu.
6Kwa kuwa Mungu, yeye aliyesema, “Nuru na ingʼae gizani,” ameifanya nuru yake ingʼae mioyoni mwetu ili kutupatia nuru ya maarifa ya utukufu wa Mungu katika uso wa Kristo.[#4:6 Mwa 1:3]
7Lakini tunayo hazina hii katika vyombo vya udongo, ili ijulikane wazi kwamba uwezo huu wa ajabu unatoka kwa Mungu, wala si kwetu.
8Twataabika kila upande lakini hatuangamizwi; twaona wasiwasi lakini hatukati tamaa;
9twateswa lakini hatuachwi; twatupwa chini lakini hatupondwi.
10Siku zote twachukua katika mwili kufa kwake Yesu ili uzima wa Yesu uweze kudhihirishwa katika miili yetu.
11Kwa maana sisi tulio hai siku zote tumetolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili uzima wake upate kudhihirishwa katika mwili wetu upatikanao na mauti.
12Hivyo basi, mauti inatenda kazi ndani yetu, bali uzima unatenda kazi ndani yenu.
13Imeandikwa, “Niliamini, kwa hiyo nimesema.” Kwa roho yule yule wa imani pia tuliamini na hivyo tunasema,[#4:13 Za 116:10]
14kwa sababu tunajua kwamba yeye aliyemfufua Bwana Yesu kutoka kwa wafu atatufufua sisi pia pamoja na Yesu na kutuleta sisi pamoja nanyi mbele zake.
15Haya yote ni kwa faida yenu, ili neema ile inavyowafikia watu wengi zaidi na zaidi ipate kusababisha shukrani nyingi kwa utukufu wa Mungu.
16Kwa hiyo, hatukati tamaa. Ingawa utu wetu wa nje unachakaa, utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku.
17Kwa maana dhiki yetu nyepesi iliyo ya kitambo inatutayarisha kwa ajili ya utukufu wa milele unaozidi kuwa mwingi kupita kiasi.
18Kwa hivyo hatuangalii yale yanayoonekana, bali yale yasiyoonekana. Kwa maana yale yanayoonekana ni ya kitambo tu, bali yale yasiyoonekana ni ya milele.