The chat will start when you send the first message.
1Kwa maana twajua kama hema letu la dunia tunayoishi likiharibiwa, tunalo jengo kutoka kwa Mungu, nyumba iliyo ya milele kule mbinguni, isiyojengwa kwa mikono ya wanadamu.
2Katika hema hili twalia kwa uchungu, tukitamani kuvikwa makao yetu ya mbinguni,
3kwa kuwa tukishavikwa hatutaonekana tena kuwa uchi.
4Kwa kuwa tukiwa bado katika hema hili twalia kwa uchungu na kulemewa, kwa sababu hatutaki kuvuliwa bali kuvikwa makao yetu ya mbinguni ili kile kipatikanacho na mauti kimezwe na uzima.
5Basi Mungu ndiye alitufanya kwa ajili ya jambo lilo hilo, naye ametupatia Roho Mtakatifu kuwa amana, akituhakikishia ahadi ya kile kijacho.
6Kwa hiyo siku zote tuna ujasiri, hata ingawa tunajua kwamba tukiwa katika mwili huu, tuko mbali na Bwana.
7Kwa maana twaenenda kwa imani wala si kwa kuona.
8Naam, tuna ujasiri, na tunaona ingekuwa bora zaidi kuuacha mwili huu na kwenda kukaa na Bwana.
9Kwa hiyo, tukiwa katika mwili huu au tukiwa mbali nao, lengo letu ni kumpendeza Bwana.
10Kwa kuwa sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mmoja apate kulipwa kwa ajili ya yale ambayo yametendwa katika mwili wake, yakiwa mema au mabaya.
11Basi, kwa kuwa tunajua kumcha Bwana, tunajitahidi kuwavuta wengine. Lakini Mungu anatufahamu dhahiri, nami natumaini kwamba tu dhahiri katika dhamiri zenu pia.
12Sio kwamba tunajaribu kujistahilisha kwenu tena, lakini tunataka kuwapa nafasi ili mwone fahari juu yetu, mweze kuwajibu hao wanaoona fahari kuhusu mambo yanayoonekana badala ya mambo yaliyo moyoni.
13Kama tumerukwa na akili, ni kwa ajili ya Mungu; kama tuna akili timamu, ni kwa ajili yenu.
14Kwa kuwa upendo wa Kristo unatutia nguvu, kwa sababu tunasadiki kuwa mmoja alikufa kwa ajili ya wote, kwa hiyo wote walikufa.
15Naye alikufa kwa ajili ya watu wote, ili wote wanaoishi wasiishi tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa na kufufuliwa tena kwa ajili yao.
16Hivyo tangu sasa hatumwangalii mtu yeyote kwa mtazamo wa kibinadamu. Ingawa wakati fulani tulimwangalia Kristo kwa namna ya kibinadamu, hatumwangalii tena hivyo.
17Kwa hiyo mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya: ya kale yamepita; tazama, yamekuwa mapya.
18Haya yote yanatokana na Mungu, ambaye ametupatanisha sisi na nafsi yake kupitia kwa Yesu Kristo, na kutupatia sisi huduma ya upatanisho:
19kwamba Mungu alikuwa ndani ya Kristo akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake mwenyewe, akiwa hawahesabii watu dhambi zao. Naye ametukabidhi sisi ujumbe huu wa upatanisho.
20Kwa hiyo sisi ni mabalozi wa Kristo, kana kwamba Mungu anawasihi kupitia kwa vinywa vyetu. Nasi twawaomba sana ninyi kwa niaba ya Kristo: mpatanishwe na Mungu.
21Kwa maana Mungu alimfanya yeye asiyekuwa na dhambi kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kufanywa haki ya Mungu kupitia kwake Kristo.[#5:21 au kuwa sadaka ya dhambi]