2 Wafalme 11

2 Wafalme 11

Athalia na Yoashi

(2Nya 22:10–23:21)

1Athalia mamaye Ahazia alipoona kuwa mwanawe amekufa, akainuka na kuangamiza jamaa yote ya mfalme.

2Lakini Yehosheba, binti ya Mfalme Yehoramu, aliyekuwa pia dada yake Ahazia, akamtwaa Yoashi mwana wa Ahazia kwa siri kutoka miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa karibu kuuawa. Akamweka Yoashi pamoja na yaya wake ndani ya chumba cha kulala na kumficha humo ili Athalia asimwone; kwa hiyo hakuuawa.

3Alibaki amefichwa pamoja na yaya wake katika Hekalu la Bwana kwa muda wa miaka sita wakati Athalia alikuwa akitawala nchi.

4Katika mwaka wa saba, Yehoyada akatumania wakuu wa vikundi vya mamia, na Wakari na walinzi, nao wakaletwa kwake katika Hekalu la Bwana . Alifanya agano nao na kuwaapisha katika Hekalu la Bwana . Ndipo akawaonesha mwana wa mfalme.[#11:4 yaani Wakerethi (taz. 1Sam 30:14; Eze 25:16; Sef 2:5, 6).]

5Akawaamuru akisema, “Hivi ndivyo iwapasavyo kufanya: Ninyi ambao mko makundi matatu mnaoingia zamu siku ya Sabato, theluthi moja italinda jumba la kifalme,

6theluthi nyingine Lango la Suri, na theluthi nyingine lango lililo nyuma ya walinzi, ambao hupeana zamu kulinda Hekalu.

7Nanyi ambao mko katika makundi mengine mawili ambao kwa kawaida hupumzika siku ya Sabato, wote mtalinda Hekalu kwa ajili ya mfalme.

8Jipangeni kumzunguka mfalme, kila mtu akiwa na silaha yake mkononi. Yeyote anayesogelea safu zenu lazima auawe. Kaeni karibu na mfalme popote aendapo.”

9Wakuu wa vikosi vya mamia wakafanya vile kuhani Yehoyada aliagiza. Kila mmoja akawachukua watu wake, wale waliokuwa wakiingia zamu siku ya Sabato na wale waliokuwa wakienda mapumziko, nao wakaja kwa kuhani Yehoyada.

10Ndipo akawapa wale wakuu mikuki na ngao zilizokuwa za Mfalme Daudi, zilizokuwa ndani ya Hekalu la Bwana .

11Wale walinzi, kila mmoja akiwa na silaha yake mkononi mwake, wakajipanga kumzunguka mfalme, karibu na madhabahu na Hekalu, kuanzia upande wa kusini hadi upande wa kaskazini mwa Hekalu.

12Yehoyada akamtoa mwana wa mfalme na kumvika taji, akampa nakala ya agano, na kumtangaza kuwa mfalme. Wakampaka mafuta, nao watu wakapiga makofi na kupaza sauti, wakisema, “Mfalme aishi maisha marefu!”

13Athalia aliposikia kelele za walinzi pamoja na watu, akawaendea watu katika Hekalu la Bwana .

14Akaangalia, na tazama, mfalme alikuwa amesimama karibu na nguzo, kama ilivyokuwa desturi. Maafisa na wapiga tarumbeta walikuwa kando ya mfalme, nao watu wote wa nchi walikuwa wanashangilia na kupiga tarumbeta. Ndipo Athalia akararua mavazi yake na kulia, “Uhaini! Uhaini!”

15Kuhani Yehoyada akawaamuru majemadari wa vikosi vya mamia, waliokuwa viongozi wa jeshi, “Mtoeni nje kati ya safu, na mkamuue kwa upanga yeyote anayemfuata.” Kwa kuwa kuhani alikuwa amesema, “Hatauawa ndani ya Hekalu la Bwana .”

16Basi wakamkamata Athalia alipofika mahali farasi huingilia katika viwanja vya jumba la mfalme, wakamuua hapo.

17Kisha Yehoyada akafanya agano kati ya Bwana na mfalme na watu kwamba watakuwa watu wa Bwana . Akafanya pia agano kati ya mfalme na watu.

18Watu wote wa nchi wakaenda kwenye hekalu la Baali na kulibomoa. Wakavunjavunja madhabahu na sanamu, na kumuua Matani kuhani wa Baali mbele ya hayo madhabahu.

Kisha Yehoyada kuhani akawaweka walinzi kwenye Hekalu la Bwana .

19Pamoja naye akawachukua majemadari wa mamia, Wakari, walinzi na watu wote wa nchi, nao kwa pamoja wakamteremsha mfalme kutoka Hekalu la Bwana na kwenda kwenye jumba la mfalme, wakiingilia njia ya lango la walinzi. Ndipo mfalme akachukua nafasi yake kwenye kiti cha ufalme;

20nao watu wote wa nchi wakafurahi. Mji ukatulia, kwa sababu Athalia alikuwa ameuawa kwa upanga nyumbani mwa mfalme.

21Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.