The chat will start when you send the first message.
1Wakati wa utawala wa Yehoyakimu, Nebukadneza mfalme wa Babeli aliishambulia nchi, naye Yehoyakimu akawa mtumwa wake kwa miaka mitatu. Lakini hatimaye akabadili mawazo yake na kuasi dhidi ya Nebukadneza.
2Bwana akatuma wavamiaji wa Wakaldayo, Waaramu, Wamoabu na Waamoni ili kumshambulia. Aliwatuma kuiangamiza Yuda sawasawa na neno la Bwana lililosemwa na watumishi wake manabii.
3Hakika mambo haya yalitokea Yuda kulingana na agizo la Bwana , ili kuwaondoa kutoka machoni pake kwa sababu ya dhambi za Manase na yote aliyoyafanya,
4ikiwa ni pamoja na kumwaga damu isiyo na hatia. Kwa kuwa aliijaza Yerusalemu kwa damu isiyo na hatia, naye Bwana hakuwa radhi kusamehe.
5Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yehoyakimu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
6Yehoyakimu akalala na baba zake. Naye Yehoyakini mwanawe akawa mfalme baada yake.
7Mfalme wa Misri hakutoka tena katika nchi yake, kwa sababu mfalme wa Babeli alikuwa ameitwaa himaya yake yote, kuanzia Kijito cha Misri hadi Mto Frati.
8Yehoyakini alikuwa na umri wa miaka kumi na nane alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miezi mitatu. Mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani kutoka Yerusalemu.
9Akafanya maovu machoni pa Bwana , kama vile baba yake alivyokuwa amefanya.
10Wakati huo, maafisa wa Nebukadneza mfalme wa Babeli walikuja kushambulia Yerusalemu, nao wakauzingira kwa jeshi.
11Nebukadneza mwenyewe akaupandia mji wakati maafisa wake walipokuwa wameuzingira.
12Yehoyakini mfalme wa Yuda, mama yake, wahudumu wake, wakuu na maafisa wake wote wakajisalimisha kwa Nebukadneza.
Katika mwaka wa nane wa utawala wa mfalme wa Babeli, akamchukua Yehoyakini kuwa mfungwa.
13Kama vile Bwana alivyokuwa amesema, Nebukadneza akaondoa hazina yote kutoka Hekalu la Bwana na kutoka jumba la mfalme, akavichukua vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Sulemani mfalme wa Israeli alikuwa amevitengeneza kwa ajili ya Hekalu la Bwana .
14Akawachukua watu wa Yerusalemu wote kwenda uhamishoni: yaani maafisa wote na wapiganaji, watu wenye ustadi wa ufundi na wahunzi, jumla yao watu elfu kumi. Watu maskini sana tu ndio walibaki katika nchi.
15Nebukadneza akamchukua mateka Yehoyakini hadi Babeli. Pia akawachukua utumwani kutoka Yerusalemu hadi Babeli mama yake mfalme, wake zake, maafisa wake, na viongozi wote wa nchi.
16Mfalme wa Babeli pia akawahamishia Babeli wapiganaji elfu saba wenye nguvu na tayari kwa vita, na mafundi na wahunzi elfu moja.
17Akamfanya Matania, ndugu wa baba yake Yehoyakini, kuwa mfalme mahali pake, na akalibadilisha jina lake kuwa Sedekia.
18Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na moja alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na moja. Mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia, kutoka Libna.
19Alifanya maovu machoni pa Bwana , kama alivyofanya Yehoyakimu.
20Haya yote yalitendeka Yerusalemu na Yuda kwa sababu ya hasira ya Bwana , naye mwishoni akawaondoa mbele zake.
Basi, Sedekia akaasi dhidi ya mfalme wa Babeli.