2 Wafalme 8

2 Wafalme 8

Ardhi ya Mshunami yarudishwa

1Basi Elisha alikuwa amemwambia yule mwanamke ambaye mwanawe alikuwa amefufuliwa, “Ondoka wewe na jamaa yako ukaishi mahali popote unapoweza kwa kitambo kidogo, kwa sababu Bwana ameamuru njaa katika nchi hii ambayo itadumu kwa miaka saba.”

2Yule mwanamke akafanya kama vile yule mtu wa Mungu alivyosema. Yeye na jamaa yake wakaondoka na kwenda kuishi katika nchi ya Wafilisti kwa miaka saba.

3Baada ya miaka saba, yule mwanamke akarudi kutoka nchi ya Wafilisti, akaenda kwa mfalme kumsihi kwa ajili ya nyumba yake na shamba lake.

4Mfalme alikuwa anazungumza na Gehazi, mtumishi wa mtu wa Mungu, naye alikuwa amesema, “Hebu niambie mambo yote makuu yaliyofanywa na Elisha.”

5Gehazi alipokuwa akimweleza mfalme jinsi Elisha alivyomfufua mtu, yule mwanamke ambaye mwanawe alikuwa amefufuliwa na Elisha akaja ili amsihi mfalme kwa ajili ya nyumba yake na shamba lake.

Gehazi akasema, “Huyu ndiye huyo mwanamke, bwana wangu mfalme, na huyu ndiye mwanawe ambaye Elisha alimfufua.”

6Mfalme akamuuliza yule mwanamke kuhusu mambo hayo, naye akamweleza.

Ndipo akaamuru afisa amshughulikie, kwa kumwambia, “Mrudishie huyu mwanamke kila kitu kilichokuwa mali yake, pamoja na mapato yote yaliyotokana na shamba lake tangu siku alipoondoka nchini hadi sasa.”

Hazaeli amuua Ben-Hadadi

7Elisha akaenda Dameski, naye Ben-Hadadi mfalme wa Aramu alikuwa mgonjwa. Mfalme alipoambiwa, “Mtu wa Mungu amekuja hadi hapa,”

8mfalme akamwambia Hazaeli, “Chukua zawadi na uende kumlaki mtu wa Mungu. Muulize Bwana kupitia yeye, kwamba, ‘Je, nitapona ugonjwa huu?’ ”

9Hazaeli akaenda kumlaki Elisha, akiwa amechukua zawadi ya kila kitu kizuri kilichopatikana Dameski, mizigo iliyobebwa na ngamia arobaini. Akaingia ndani na kusimama mbele yake, akasema, “Mwanao Ben-Hadadi mfalme wa Aramu amenituma niulize, ‘Je, nitapona ugonjwa huu?’ ”

10Elisha akajibu, “Nenda ukamwambie, ‘Hakika utapona’; lakini Bwana amenifunulia kwamba kweli atakufa.”

11Elisha akamkazia Hazaeli macho kwa nguvu hata akaona aibu. Kisha mtu wa Mungu akaanza kulia.

12Hazaeli akauliza “Kwa nini bwana wangu analia?”

Elisha akajibu, “Kwa sababu najua mabaya utakayowatendea Waisraeli. Utachoma moto ngome zao, utawaua vijana wao kwa upanga, kuwatupa chini kwa nguvu watoto wachanga, na kuwatumbua wanawake wenye mimba.”

13Hazaeli akasema, “Itawezekanaje mtumishi wako, aliye mbwa tu, kufanya tendo la ajabu hivyo?”

Elisha akamjibu, “Bwana amenionesha kuwa utakuwa mfalme wa Aramu.”

14Kisha Hazaeli akamwacha Elisha na kumrudia bwana wake. Ben-Hadadi akamuuliza, “Elisha alikuambia nini?” Hazaeli akajibu, “Aliniambia kwamba hakika utapona.”

15Lakini kesho yake Hazaeli akachukua nguo nzito, akailoweka ndani ya maji, akaitandaza juu ya uso wa mfalme, hivyo akafa. Kisha Hazaeli akawa mfalme baada yake.

Yehoramu mfalme wa Yuda

(2Nya 21:1‑20)

16Katika mwaka wa tano wa Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli, wakati huo Yehoshafati akiwa mfalme wa Yuda, Yehoramu mwana wa Yehoshafati akaanza kutawala kama mfalme wa Yuda.

17Alikuwa na umri wa miaka thelathini na mbili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka nane.

18Akaenenda katika njia za wafalme wa Israeli, kama nyumba ya Ahabu ilivyokuwa imefanya, kwa kuwa alimwoa binti Ahabu. Akatenda maovu machoni pa Bwana .

19Hata hivyo, kwa ajili ya Daudi mtumishi wake, Bwana hakutaka kuiangamiza Yuda. Alikuwa ameahidi kuidumisha taa kwa ajili ya Daudi na wazao wake milele.

20Wakati wa utawala wa Yehoramu, Edomu waliasi dhidi ya Yuda na kujiwekea mfalme wao wenyewe.

21Basi Yehoramu akaenda Sairi pamoja na magari yake yote ya vita. Waedomu wakamzunguka yeye na majemadari wake wa magari yake ya vita, lakini akaondoka, akapenya usiku na kuwashambulia Waedomu. Hata hivyo, jeshi lake likatorokea nyumbani mwao.

22Hadi leo Edomu wameasi dhidi ya Yuda. Libna pia wakaasi wakati huo huo.

23Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yehoramu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?

24Yehoramu akalala na baba zake, akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi. Naye Ahazia mwanawe akawa mfalme baada yake.

Ahazia mfalme wa Yuda

(2Nya 22:1‑6)

25Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli, Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda alianza kutawala.

26Ahazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mbili alipoanza kutawala, naye akatawala katika Yerusalemu kwa mwaka mmoja. Mama yake aliitwa Athalia, mjukuu wa Omri mfalme wa Israeli.

27Akaenenda katika njia za nyumba ya Ahabu, na kutenda maovu machoni pa Bwana , kama nyumba ya Ahabu ilivyokuwa imefanya, kwa kuwa alikuwa ameoa kutoka nyumba ya Ahabu.

28Ahazia akaenda vitani na Yoramu mwana wa Ahabu kupigana na Hazaeli mfalme wa Aramu huko Ramoth-Gileadi. Waaramu wakamjeruhi Yoramu.

29Hivyo Mfalme Yoramu akarudi Yezreeli ili apate kuuguza majeraha aliyojeruhiwa na Waaramu huko Ramothi alipopigana na Hazaeli mfalme wa Aramu.[#8:29 Rama kwa Kiebrania]

Ndipo Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda akashuka kwenda Yezreeli kumtazama Yoramu mwana wa Ahabu, kwa sababu alikuwa amejeruhiwa.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.