The chat will start when you send the first message.
1Mitume na waumini waliokuwa huko Yudea wakasikia kuwa watu wa Mataifa nao wamepokea neno la Mungu.
2Hivyo Petro alipopanda Yerusalemu, waumini waliotahiriwa wakamshutumu,
3wakisema, “Ulienda kwa watu wasiotahiriwa na kula pamoja nao.”
4Ndipo Petro akaanza kuwaeleza kuhusu mambo yote yalivyotokea hatua kwa hatua akisema,
5“Nilikuwa katika mji wa Yafa nikiomba, nami nikapitiwa na usingizi wa ghafula, nikaona maono. Kulikuwa na kitu kama kitambaa kikubwa kikishuka kutoka mbinguni, kikashushwa kwa ncha zake nne, nacho kikanikaribia.
6Nilipoangalia ndani yake kwa karibu niliona wanyama wenye miguu minne wa nchini, wanyama mwitu, wanyama watambaao, na ndege wa angani.
7Ndipo nikasikia sauti ikiniambia, ‘Petro, ondoka uchinje na ule.’
8“Nikajibu, ‘La hasha, Bwana! Kitu chochote kilicho najisi hakijaingia kinywani mwangu.’
9“Sauti ikasema kutoka mbinguni mara ya pili, ‘Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.’
10Jambo hili lilitokea mara tatu, ndipo kile kitu kikavutwa tena mbinguni.
11“Wakati ule ule watu watatu, waliokuwa wametumwa kutoka Kaisaria waliwasili katika nyumba niliyokuwa nikikaa.
12Roho Mtakatifu akaniambia niende nao bila kuwa na ubaguzi kati yao na sisi. Hawa ndugu sita pia walifuatana nami, nasi tukaingia nyumbani mwa huyo Kornelio.
13Akatuambia jinsi alivyoona malaika aliyekuwa amesimama katika nyumba yake na kusema, ‘Tuma watu waende Yafa wakamlete Simoni aitwaye Petro.
14Yeye atakupa ujumbe ambao kwa huo wewe na wa nyumbani mwako wote mtaokoka.’
15“Nami nilipoanza kusema, Roho Mtakatifu akashuka juu yao kama vile alivyotushukia sisi hapo mwanzo.
16Nami nikakumbuka yale Bwana aliyosema, ‘Yohana alibatiza kwa maji, lakini ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu.’
17Basi ikiwa Mungu aliwapa hawa watu kipawa kile kile alichotupatia sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani hata nifikirie kuwa ningeweza kumpinga Mungu?”
18Waliposikia haya hawakuwa na lingine la kupinga. Nao wakamsifu Mungu, wakisema, “Basi, Mungu amewapa hata watu wa Mataifa toba iletayo uzima wa milele.”
19Basi wale waliotawanyika kwa ajili ya mateso yaliyotokea Stefano alipouawa walisafiri hadi Foinike na Kipro na Antiokia. Nao hawakuhubiri lile Neno kwa mtu yeyote isipokuwa Wayahudi.
20Lakini baadhi yao walikuwa watu wa Kipro na Kirene, ambao walipokuja Antiokia walinena na Wayunani pia wakiwahubiria Habari Njema kuhusu Bwana Yesu.
21Mkono wa Bwana ulikuwa pamoja nao, nayo idadi kubwa ya watu wakaamini na kumgeukia Bwana.
22Habari hizi zilipofika masikioni mwa kanisa huko Yerusalemu, wakamtuma Barnaba aende Antiokia.
23Alipofika na kuona madhihirisho ya neema ya Mungu, akafurahi na kuwatia moyo waendelee kuwa waaminifu kwa Bwana kwa mioyo yao yote.
24Barnaba alikuwa mtu mwema, aliyejaa Roho Mtakatifu, mwenye imani, nayo idadi kubwa ya watu wakaongezeka kwa Bwana.
25Kisha Barnaba akaenda Tarso kumtafuta Sauli,
26naye alipompata akamleta Antiokia. Hivyo kwa mwaka mzima Barnaba na Sauli wakakutana na kanisa na kufundisha idadi kubwa ya watu. Wanafunzi waliitwa Wakristo mara ya kwanza huko Antiokia.
27Wakati huo manabii walishuka toka Yerusalemu hadi Antiokia.
28Mmoja wao aliyeitwa Agabo akasimama, akatabiri kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwamba njaa kubwa ingeenea ulimwengu mzima. (Njaa hiyo ilitokea wakati wa utawala wa Klaudio.)
29Mitume wakaamua kwamba kila mtu, kulingana na uwezo alio nao, atoe msaada kwa ajili ya ndugu wanaoishi Yudea.
30Wakafanya hivyo, misaada yao ikapelekwa kwa wazee kwa mikono ya Barnaba na Sauli.