The chat will start when you send the first message.
1Apolo alipokuwa huko Korintho, Paulo alisafiri sehemu za bara, akafika Efeso. Huko akawakuta wanafunzi kadhaa,
2akawauliza, “Je, mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini?”
Wakajibu, “Hapana, hata hatukusikia kuwa kuna Roho Mtakatifu.”
3Ndipo Paulo akawauliza, “Je, mlibatizwa kwa ubatizo gani?” Wakajibu, “Kwa ubatizo wa Yohana.”
4Paulo akasema, “Ubatizo wa Yohana ulikuwa wa toba, aliwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja baada yake, yaani Yesu.”
5Waliposikia haya, wakabatizwa katika jina la Bwana Yesu.
6Paulo alipoweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akawashukia, nao wakanena kwa lugha mpya na kutabiri.
7Walikuwa wapatao wanaume kumi na wawili.
8Paulo akaingia katika sinagogi na kunena humo kwa ujasiri kwa muda wa miezi mitatu, akijadiliana na watu na kuwashawishi katika mambo ya ufalme wa Mungu.
9Lakini baadhi yao wakakaidi; walikataa kuamini, na wakakashifu Njia Ile hadharani. Basi Paulo aliachana nao. Akaenda na wanafunzi wale, akahojiana nao kila siku katika darasa la Tirano.[#19:9 maana yake wafuasi wa Yesu (Yn 14:6; Mdo 24:14); walichukuliwa kuwa dhehebu la dini ya Wayahudi.]
10Jambo hili likaendelea kwa muda wa miaka miwili, kiasi kwamba Wayahudi na Wayunani wote walioishi huko jimbo la Asia wakawa wamesikia neno la Bwana.
11Mungu akafanya miujiza mingi isiyo ya kawaida kupitia kwa Paulo,
12hivi kwamba leso au vitambaa vilivyokuwa vimegusa mwili wa Paulo viliwekwa juu ya wagonjwa, nao wakapona magonjwa yao, na pepo wachafu wakawatoka.
13Baadhi ya Wayahudi waliotangatanga wakitoa pepo wachafu wakajaribu kutumia jina la Bwana Yesu kwa wale wenye pepo, wakisema, “Kwa jina la Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo, nakuamuru utoke.”
14Wana saba wa Skewa, Myahudi aliyekuwa kiongozi wa makuhani, walikuwa wanafanya hivyo.
15Siku moja pepo mchafu akawajibu, “Yesu namjua na Paulo pia namjua, lakini ninyi ni nani?”
16Kisha yule mtu aliyekuwa na pepo mchafu akawarukia, akawashambulia vikali, akawashinda nguvu wote, wakatoka ndani ya ile nyumba wakikimbia wakiwa uchi na wenye majeraha.
17Habari hii ikajulikana kwa Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawajaa wote, nalo jina la Bwana Yesu likaheshimiwa sana.
18Wengi wa wale waliokuwa wameamini wakati huu wakaja na kutubu waziwazi kuhusu matendo yao maovu.
19Idadi kubwa ya wale waliofanya mambo ya uganga wakaleta vitabu vyao na kuviteketeza kwa moto hadharani. Walipofanya hesabu ya thamani ya vitabu vilivyoteketezwa ilikuwa drakma elfu hamsini za fedha.[#19:19 Drakma moja ilikuwa na thamani sawa na mshahara wa kibarua wa siku moja.]
20Hivyo neno la Bwana likaenea sana na kuwa na nguvu.
21Baada ya mambo haya kutukia, Paulo akakusudia rohoni kwenda Yerusalemu kupitia Makedonia na Akaya. Akasema, “Baada ya kufika huko, yanipasa pia kwenda Rumi.”
22Hivyo akatuma wasaidizi wake wawili, Timotheo na Erasto, waende Makedonia, wakati yeye mwenyewe alibaki kwa muda kidogo huko jimbo la Asia.
23Wakati huo huo pakatokea dhiki kubwa kwa sababu ya Njia Ile.
24Mtu mmoja jina lake Demetrio mfua fedha aliyekuwa akitengeneza vinyago vya fedha vya Artemi na kuwapatia mafundi wake biashara kubwa,
25aliwaita pamoja watu wengine waliofanya kazi ya ufundi kama yake na kusema, “Enyi watu, mnajua ya kuwa utajiri wetu unatokana na biashara hii!
26Mnaona na kusikia jinsi huyu Paulo amewashawishi na kuwapoteza watu wengi hapa Efeso na karibu jimbo lote la Asia. Anasema kwamba miungu iliyofanywa kwa mikono ya wanadamu si miungu hata kidogo.
27Kwa hiyo kuna hatari si kwa kazi yetu kudharauliwa tu, bali pia hata hekalu la mungu wa kike Artemi aliye mkuu, anayeabudiwa jimbo lote la Asia na ulimwengu wote, litakuwa limepokonywa fahari yake ya kiungu.”
28Waliposikia maneno haya, wakaghadhibika, wakaanza kupiga kelele wakisema, “Artemi wa Waefeso ni mkuu!”
29Mara mji wote ukajaa ghasia. Watu wakawakamata Gayo na Aristarko, wenyeji wa Makedonia waliokuwa wakisafiri na Paulo, wakakimbilia nao katika ukumbi wa maonesho.
30Paulo akataka kuingia katikati ya umati, lakini wanafunzi hawakumruhusu.
31Hata baadhi ya viongozi wa sehemu ile, waliokuwa rafiki zake Paulo, wakatuma watu wakitamani asiingie katika ule ukumbi wa maonesho.
32Umati wa watu walikuwa na taharuki. Walikuwa wakipiga kelele, hawa wakisema hili na wengine lile. Idadi kubwa ya watu hawakujua hata ni kwa nini walikuwa wamekusanyika huko.
33Wayahudi wakamsukumia Iskanda mbele na baadhi ya watu kwenye umati ule wakampa maelekezo. Akawaashiria kwa mkono ili watulie aweze kujitetea mbele ya watu.
34Lakini walipotambua kwamba alikuwa Myahudi, wote wakapiga kelele kwa sauti moja kwa karibu muda wa saa mbili, wakisema, “Artemi wa Efeso ni mkuu!”
35Baadaye karani wa mji akanyamazisha umati ule wa watu na kusema, “Enyi watu wa Efeso, je, ulimwengu wote haujui ya kuwa mji wa Efeso ndio unaotunza hekalu la Artemi aliye mkuu na ile sanamu yake iliyoanguka kutoka mbinguni?
36Kwa hiyo, kwa kuwa mambo haya hayawezi kukanushwa, inawapasa mnyamaze na wala msifanye lolote kwa haraka.
37Kwa kuwa mmewaleta hawa watu hapa, ingawa hawajaiba hekaluni wala kumkufuru huyu mungu wetu wa kike.
38Basi, ikiwa Demetrio na mafundi wenzake wana mashtaka dhidi ya mtu yeyote, mahakama ziko wazi na wasaidizi wa mwakilishi wa mtawala. Wanaweza kufungua mashtaka.
39Lakini kama kuna jambo jingine lolote zaidi mnalotaka kulileta, itabidi lisuluhishwe katika kusanyiko halali.
40Kama ilivyo sasa, tuko hatarini kushtakiwa kwa kufanya ghasia kwa sababu ya tukio la leo. Kwa kuwa hakuna sababu tutakayoweza kutoa kuhalalisha msukosuko huu.”
41Baada ya kusema haya akavunja mkutano.