Matendo 2

Matendo 2

Kushuka kwa Roho Mtakatifu

1Siku ya Pentekoste ilipowadia, waumini wote walikuwa mahali pamoja.

2Ghafula, sauti kama mvumo mkubwa wa upepo mkali ikatoka mbinguni, ikaijaza nyumba yote walimokuwa wameketi.

3Zikatokea ndimi kama za moto zilizogawanyika na kutua juu ya kila mmoja wao.

4Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakaanza kunena kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia.

5Basi walikuwako Yerusalemu Wayahudi wanaomcha Mungu kutoka kila taifa chini ya mbingu.

6Waliposikia sauti hii, umati wa watu walikusanyika pamoja wakistaajabu, kwa sababu kila mmoja wao aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.

7Wakiwa wameshangaa na kustaajabu, wakauliza, “Je, hawa wote wanaozungumza si Wagalilaya?

8Imekuwaje basi kila mmoja wetu anawasikia wakinena kwa lugha yake ya kuzaliwa?

9Wapathi, Wamedi, Waelami, wakazi wa Mesopotamia, Yudea, Kapadokia, Ponto na jimbo la Asia,

10Frigia, Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni kutoka Rumi

11(Wayahudi na wale walioongokea dini ya Kiyahudi), Wakrete na Waarabu: sote tunawasikia watu hawa wakisema mambo makuu ya ajabu ya Mungu katika lugha zetu wenyewe.”

12Wakiwa wameshangaa na kufadhaika wakaulizana, “Ni nini maana ya mambo haya?”

13Lakini wengine wakawadhihaki wakasema, “Hawa wamelewa kwa divai!”

Petro ahutubia umati

14Ndipo Petro akasimama pamoja na wale mitume kumi na mmoja, akapaza sauti yake na kuhutubia umati ule wa watu, akasema: “Wayahudi wenzangu na nyote mnaoishi Yerusalemu, nisikilizeni kwa makini, ili jambo hili lijulikane kwenu.

15Hakika watu hawa hawajalewa kama mnavyodhania, kwa kuwa sasa ni saa tatu asubuhi!

16La, hili ni jambo lililotabiriwa na nabii Yoeli, akisema:

17“ ‘Katika siku za mwisho, asema Mungu,

nitamimina Roho wangu

juu ya wote wenye mwili.

Wana wenu wa kiume na wa kike watatabiri,

vijana wenu wataona maono,

na wazee wenu wataota ndoto.

18Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake,

katika siku zile nitamimina Roho wangu,

nao watatabiri.

19Nami nitaonesha maajabu juu mbinguni,

na ishara chini duniani:

damu, moto, na mawimbi ya moshi.

20Jua litakuwa giza

na mwezi utakuwa mwekundu kama damu,

kabla ya kuja siku ile kuu ya Bwana

iliyo tukufu.

21Na kila mtu atakayeliitia

jina la Bwana, ataokolewa.’

22“Enyi Waisraeli, sikilizeni maneno haya nisemayo: Yesu wa Nazareti alikuwa mtu aliyethibitishwa kwenu na Mungu kwa miujiza, maajabu na ishara, ambayo Mungu alitenda miongoni mwenu kupitia kwake, kama ninyi wenyewe mjuavyo.

23Baada ya huyu mtu kutolewa kwenu kwa mpango wa Mungu uliokusudiwa kwa kujua kwake Mungu tangu zamani, ninyi mlimuua kwa kumsulubisha msalabani, kwa mikono ya watu waovu.

24Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu akamwondolea uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana yeye kushikiliwa na nguvu za mauti.

25Kwa maana Daudi asema hivi kumhusu:

“ ‘Nilimwona Bwana mbele yangu daima.

Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume,

sitatikisika.

26Kwa hiyo moyo wangu unafurahia,

na ulimi wangu unashangilia;

mwili wangu nao utapumzika kwa tumaini.

27Kwa maana hutaniacha kaburini,

wala hutamwacha Aliye Mtakatifu wako kuona uharibifu.

28Umenionesha njia za uzima,

utanijaza na furaha mbele zako.’

29“Ndugu zangu Waisraeli, nataka niwaambie kwa uhakika kwamba baba yetu wa zamani Daudi alikufa na kuzikwa, nalo kaburi lake lipo hapa hadi leo.

30Lakini alikuwa nabii na alijua ya kuwa Mungu alikuwa amemwahidi kwa kiapo, kwamba angemweka mmoja wa wazao wake penye kiti chake cha utawala.

31Daudi, akiona mambo yaliyo mbele, akanena kuhusu kufufuka kwa Kristo, kwamba hakuachwa kaburini, wala mwili wake haukuona uharibifu.[#2:31 maana yake Masiya , yaani Aliyetiwa mafuta.]

32Mungu alimfufua huyu Yesu, na sisi sote ni mashahidi wa jambo hilo.

33Basi yeye ametukuzwa hadi mkono wa kuume wa Mungu, na amepokea kutoka kwa Baba ahadi ya Roho Mtakatifu, naye amemimina kile mnachoona sasa na kusikia.

34Kwa kuwa Daudi hakupaa kwenda mbinguni, lakini anasema,

“ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu:

“Keti mkono wangu wa kuume,

35hadi nitakapowaweka adui zako

chini ya miguu yako.”’

36“Kwa hiyo Israeli wote na wajue jambo hili kwa uhakika kwamba: Mungu amemfanya huyu Yesu, ambaye ninyi mlimsulubisha, kuwa Bwana na Kristo.”

Waumini waongezeka

37Watu waliposikia maneno haya yakawachoma mioyo yao, wakawauliza Petro na wale mitume wengine, “Ndugu zetu tufanye nini?”

38Petro akawajibu, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu kwa jina la Yesu Kristo, ili mpate kusamehewa dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu na watoto wenu, na kwa wote walio mbali, na kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita amjie.”

40Petro akawaonya kwa maneno mengine mengi na kuwasihi akisema, “Jiepusheni na kizazi hiki kilichopotoka.”

41Wale wote waliopokea ujumbe wa Petro kwa furaha wakabatizwa, na siku ile waliongezeka watu wapatao elfu tatu.

Ushirika wa waumini

42Nao wakadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali.

43Kila mtu akaingiwa na hofu ya Mungu, nayo miujiza mingi na ishara zikafanywa na mitume.

44Waumini wote walikuwa mahali pamoja, nao wakashirikiana katika mambo yote.

45Waliuza mali yao na vitu walivyokuwa navyo, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.

46Siku zote kwa moyo mmoja walikutana ndani ya ukumbi wa Hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, wakila chakula chao kwa furaha na moyo mweupe,

47wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Kila siku Bwana akaliongeza kanisa wale waliokuwa wakiokolewa.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.