Matendo 6

Matendo 6

Mateso na kuenea kwa Injili

Saba wachaguliwa kuhudumu

1Basi ikawa katika siku hizo, wakati idadi ya wanafunzi ilipokuwa ikiongezeka sana, Wayahudi wa Kiyunani walinungʼunika dhidi ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahaulika katika mgawo wa chakula wa kila siku.[#6:1 Wayahudi waliofuata lugha na desturi za Kiyunani; #6:1 Wayahudi walioshikilia lugha na desturi zao za Kiebrania]

2Wale mitume kumi na wawili wakakusanya wanafunzi wote pamoja wakasema, “Haitakuwa vyema sisi kuacha huduma ya neno la Mungu ili kuhudumu mezani.

3Kwa hiyo ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, watu wenye sifa njema, waliojawa na Roho Mtakatifu na hekima, ambao tunaweza kuwakabidhi kazi hii,

4nasi tutatumia muda wetu kuomba na katika huduma ya neno.”

5Yale waliyosema yakawapendeza watu wote, nao wakamchagua Stefano (mtu aliyejawa na imani na Roho Mtakatifu) pamoja na Filipo, Prokoro, Nikanori, Timoni, Parmena na Nikolao kutoka Antiokia, mtu wa Mataifa aliyeongokea dini ya Kiyahudi.

6Wakawaleta watu hawa mbele ya mitume, nao wakawaombea na kuwawekea mikono.

7Neno la Mungu likazidi kuenea. Idadi ya wanafunzi ikazidi kuongezeka sana katika Yerusalemu, hata makuhani wengi wakaitii ile imani.

Kukamatwa kwa Stefano

8Stefano, akiwa amejaa neema na nguvu za Mungu, alifanya ishara na miujiza mikubwa miongoni mwa watu.

9Hata hivyo, ukainuka upinzani wa watu wa Sinagogi la Watu Huru (kama lilivyokuwa linaitwa) la Wayahudi wa Kirene na wa Iskanderia, na wengine kutoka Kilikia na jimbo la Asia. Watu hawa wakaanza kupingana na Stefano.

10Lakini hawakuweza kushindana na ile hekima aliyopewa na Roho alipokuwa akisema.

11Ndipo kwa siri wakawashawishi watu fulani waseme, “Tumemsikia Stefano akisema maneno ya kufuru dhidi ya Musa na dhidi ya Mungu.”

Stefano afikishwa mbele ya Baraza

12Wakawachochea watu, wazee na walimu wa sheria, nao wakamkamata Stefano wakamfikisha mbele ya Baraza la Wayahudi.[#6:12 ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi; liliundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu.]

13Wakawaleta mashahidi wa uongo ambao walishuhudia, wakasema, “Mtu huyu kamwe haachi kusema dhidi ya mahali hapa patakatifu na dhidi ya Sheria.

14Kwa maana tumemsikia akisema kwamba Yesu wa Nazareti atapaharibu mahali patakatifu na kubadili desturi zote tulizopewa na Musa.”

15Watu wote waliokuwa wameketi katika Baraza la Wayahudi wakamkazia macho Stefano, wakaona uso wake unangʼaa kama uso wa malaika.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.