The chat will start when you send the first message.
1Hizi ndizo amri na sheria ambazo ni lazima mwe waangalifu kuzifuata katika nchi ambayo Bwana , Mungu wa baba zenu, amewapa kumiliki, kwa muda wote mtakaoishi katika nchi.
2Haribuni kabisa kila mahali pao pa kuabudia kwenye milima mirefu, vilima na chini ya kila mti mkubwa ambamo mataifa haya mnayoenda kuchukua ardhi yao huabudia miungu yao.
3Bomoeni madhabahu zao, vunjeni yale mawe wanayoabudu, chomeni moto nguzo zao za Ashera; katilieni mbali sanamu za miungu yao na mfute majina yao mahali hapo.
4Kamwe msimwabudu Bwana Mungu wenu kama wanavyoabudu wao.
5Bali mtatafuta mahali Bwana Mungu wenu atakapopachagua katika makabila yenu yote ili aliweke jina lake huko kuwa makao yake. Mahali hapo ndipo iwapasapo kwenda;
6hapo ndipo mtakapoleta sadaka zenu za kuteketezwa na dhabihu, zaka zenu na changizo zenu, kile ulichoweka nadhiri kutoa, sadaka zenu za hiari na wazaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ngʼombe, na ya mbuzi na kondoo.
7Hapo, katika uwepo wa Bwana Mungu wenu, ninyi pamoja na jamaa zenu, mtakula na kufurahia kila kitu ambacho mmegusa kwa mikono yenu, kwa sababu Bwana Mungu wenu amewabariki.
8Msifanye kama tunavyofanya hapa leo, kila mtu anavyopenda mwenyewe,
9kwa kuwa bado hamjafikia mahali pa mapumziko na urithi ambao Bwana Mungu wenu anawapa.
10Lakini mtavuka Yordani na kuishi katika nchi Bwana Mungu wenu anayowapa kama urithi, naye atawapa pumziko kutokana na adui zenu wote wanaowazunguka ili ninyi mpate kuishi kwa salama.
11Kisha kuhusu mahali Bwana Mungu wenu atakapopachagua kuwa makao ya Jina lake, hapo ndipo inapowapasa kuleta kila kitu ninachowaamuru: sadaka zenu za kuteketezwa na dhabihu, zaka zenu na changizo, pamoja na vitu vyote vyenye thamani ambavyo mmeweka nadhiri kumtolea Bwana .
12Hapo furahini mbele za Bwana Mungu wenu, ninyi, wana wenu na binti zenu, watumishi wenu wa kiume na wa kike, pamoja na Walawi kutoka miji yenu ambao hawana mgawo wala urithi wao wenyewe.
13Kuweni waangalifu, msitoe dhabihu zenu za kuteketezwa mahali popote mnapopapenda.
14Mtazitoa tu mahali atakapopachagua Bwana katika mojawapo ya makabila yenu, nanyi hapo zingatieni kila jambo ninalowaamuru.
15Hata hivyo, mnaweza kuwachinja wanyama wenu katika miji yenu yoyote ile na kula nyama nyingi mpendavyo kama vile mmemchinja paa au kulungu, kulingana na baraka mtakazojaliwa na Bwana Mungu wenu. Watu walio najisi na walio safi wanaweza kula.
16Lakini kamwe usile damu; imwage ardhini kama maji.
17Hamruhusiwi kula katika miji yenu zaka yenu ya nafaka, ya divai mpya na ya mafuta, au mzaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ngʼombe na makundi yenu ya mbuzi na kondoo, wala chochote ambacho mmeweka nadhiri kukitoa, au sadaka zako za hiari, wala matoleo maalum.
18Badala yake, mtakula vitu hivyo katika uwepo wa Bwana Mungu wenu mahali Bwana Mungu wenu atakapopachagua: wewe, wana wako na binti zako, watumishi wako wa kiume na wa kike, na Walawi kutoka miji yenu. Mnatakiwa mfurahi mbele za Bwana Mungu wenu kwa kula kitu mtakachoweka mikono yenu.
19Mwe waangalifu msiwapuuze Walawi kwa muda wote mnaoishi katika nchi yenu.
20Bwana Mungu wenu atakapokuwa ameongeza nchi yenu kama alivyowaahidi, nanyi mkitamani nyama na mkisema, “Ningependa nyama,” hapo unaweza kula nyingi upendavyo.
21Kama mahali Bwana Mungu wenu atakapopachagua kuweka Jina lake ni mbali sana kutoka kwenu, unaweza kuchinja wanyama kutoka makundi yenu ya ngʼombe, ya mbuzi na ya kondoo ambayo Bwana amewapa, kama nilivyokuamuru, na mkiwa katika miji yenu wenyewe mnaweza kula nyingi mtakavyo.
22Mle kama vile mngekula paa na kulungu. Wote walio najisi na walio safi mnaweza kula.
23Lakini hakikisheni kwamba hamkula damu, kwa sababu damu ni uhai, kamwe msile uhai pamoja na nyama.
24Hamruhusiwi kamwe kula damu; imwageni ardhini kama maji.
25Msile damu, ili mweze kufanikiwa ninyi pamoja na watoto wenu baada yenu, kwa sababu mtakuwa mkifanya lililo haki machoni pa Bwana .
26Lakini vichukueni vitu vyenu vilivyowekwa wakfu pamoja na vile mlivyoweka nadhiri, mwende mahali pale Bwana atakapopachagua.
27Leteni sadaka zenu za kuteketezwa juu ya madhabahu ya Bwana Mungu wenu, vyote nyama na damu. Damu ya dhabihu zenu lazima imiminwe kando ya madhabahu ya Bwana Mungu wenu, lakini nyama mnaweza kula.
28Mwe waangalifu kutii masharti haya yote ninayowapa, ili siku zote mweze kufanikiwa, ninyi pamoja na watoto wenu baada yenu, kwa sababu mtakuwa mkifanya lililo jema na sahihi mbele za macho ya Bwana Mungu wenu.
29Bwana Mungu wenu atayakatilia mbali mbele yenu mataifa ambayo punde kidogo mtayavamia na kuyaondoa. Lakini mtakapokuwa mmeyafukuza na kuishi katika nchi yao,
30na baada ya kuangamizwa mbele yenu, mwe waangalifu msijiingize katika tanzi kwa kuuliza habari za miungu yao, mkisema, “Je, mataifa haya hutumikiaje miungu yao? Nasi tutafanya vivyo hivyo.”
31Kamwe msimwabudu Bwana Mungu wenu kwa njia wanayoabudu miungu yao, kwa sababu katika kuabudu miungu yao, wanafanya aina zote za machukizo anayoyachukia Bwana . Hata huwateketeza watoto wao wa kiume na wa kike motoni kama kafara kwa miungu yao.
32Hakikisheni kwamba mnafanya yote niliyowaamuru; msiongeze kitu wala msipunguze kitu.