Kumbukumbu 14

Kumbukumbu 14

Vyakula vilivyo najisi na vilivyo safi

(Law 11:1‑47)

1Ninyi ni watoto wa Bwana Mungu wenu. Msijichanje ama kujinyoa upara kwenye paji la uso kwa ajili ya aliyekufa,

2kwa kuwa ninyi ni taifa takatifu kwa Bwana Mungu wenu. Bwana amewachagua ninyi kuwa taifa lake la pekee kutoka mataifa yote duniani.

3Msile kitu chochote ambacho ni machukizo.

4Hawa ndio wanyama mtakaokula: ngʼombe, kondoo, mbuzi,

5kulungu, paa, kongoni, paa mweupe, mbuzi-mwitu, pofu na kondoo wa mlimani.

6Mnaweza kumla mnyama yeyote mwenye kwato zilizogawanyika mara mbili, pia yule anayecheua.

7Hata hivyo, miongoni mwa wale wanaocheua au wale walio na kwato zilizogawanyika kamwe msile ngamia, sungura na pelele. Iwapo wanacheua, lakini hawana kwato zilizogawanyika; ni najisi kwenu.

8Nguruwe pia ni najisi; ingawa ana kwato zilizogawanyika, hacheui. Msile nyama yake wala kugusa mzoga wake.

9Katika viumbe hai vyote viishivyo kwenye maji, mnaweza kula yeyote aliye na mapezi na magamba.

10Lakini chochote kisicho na mapezi na magamba msile; kwenu ni najisi.

11Mnaweza kula ndege yeyote aliye safi.

12Lakini wafuatao msiwale: tai, furukombe, kipungu,

13kengewa mwekundu, kengewa mweusi, mwewe wa aina yoyote,

14kunguru wa aina yoyote,

15mbuni, kiruka-njia, dudumizi, kipanga wa aina yoyote,

16bundi, mumbi, bundi mkubwa,

17mwari, nderi, mnandi,

18korongo, koikoi wa aina yoyote, hudihudi na popo.

19Wadudu wote warukao kwa makundi ni najisi kwenu, msiwale.

20Lakini viumbe vyote vyenye mabawa vilivyo safi mwaweza kula.

21Msile kitu chochote mtakachokuta kimekufa. Mnaweza kumpa mgeni yeyote anayeishi katika mojawapo ya miji yenu, naye anaweza kula au mnaweza kumuuzia mtu wa nchi nyingine. Lakini ninyi ni watu watakatifu kwa Bwana Mungu wenu.

Msitokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.

Zaka

22Hakikisheni mmetenga sehemu ya kumi ya mazao yote ya mashamba yenu kila mwaka.

23Mtakula zaka za nafaka yenu, divai mpya, mafuta na wazaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ngʼombe na ya kondoo na mbuzi mbele za Bwana Mungu wenu pale mahali atakapopachagua kama maskani kwa ajili ya Jina lake, ili mpate kujifunza kumheshimu Bwana Mungu wenu daima.

24Lakini ikiwa mahali pale ni mbali sana nanyi mmebarikiwa na Bwana Mungu wenu na hamwezi kubeba zaka yenu (kwa sababu mahali pale Bwana atakapopachagua kuliweka Jina lake ni mbali sana),

25basi badilisheni zaka yenu kuwa fedha, mkaichukue hiyo fedha mwende nayo mahali Bwana Mungu wenu atakapopachagua.

26Tumieni hiyo fedha kununua chochote ukitakacho: ngʼombe, kondoo, divai au kinywaji chochote chenye chachu au chochote mnachotaka. Kisha ninyi na watu wa nyumbani mwenu mtaila mbele za Bwana Mungu wenu na kufurahi.

27Msiache kuwajali Walawi wanaoishi katika miji yenu, kwa kuwa hao hawana shamba wala urithi wao wenyewe.

28Mwishoni mwa kila mwaka wa tatu, leteni zaka zote za mazao ya miaka ile na uyahifadhi kwenye miji yenu,

29ili Walawi (ambao hawana mashamba wala urithi wao wenyewe) na wageni, yatima na wajane wanaoishi kwenye miji yenu wapate kuja kula na kushiba, ili Bwana Mungu wenu apate kuwabariki ninyi katika kazi zote za mikono yenu.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.