The chat will start when you send the first message.
1Musa na wazee wa Israeli wakawaagiza watu: “Yashikeni maagizo haya yote ninayowaagiza leo.
2Mtakapokuwa mmevuka Mto Yordani na kuingia katika nchi anayowapa Bwana Mungu wenu, msimamishe mawe makubwa na myapake chokaa.
3Andikeni juu yake maneno yote ya sheria hii wakati mtakapokuwa mmevuka na kuingia katika nchi anayowapa Bwana Mungu wenu, nchi inayotiririka maziwa na asali, kama vile Bwana , Mungu wa baba zenu, alivyowaahidi.
4Mtakapokuwa mmevuka Yordani, simamisheni mawe haya juu ya Mlima Ebali, kama ninavyowaagiza leo, na myapake chokaa.
5Huko mjengeeni Bwana Mungu wenu madhabahu, madhabahu ya mawe. Msitumie kifaa chochote cha chuma juu yake.
6Jengeni madhabahu ya Bwana Mungu wenu kwa mawe ya shambani, na mtoe sadaka za kuteketezwa juu yake kwa Bwana Mungu wenu.
7Toeni sadaka za amani juu yake, mkizila na kufurahia mbele za Bwana Mungu wenu.
8Nanyi mtaandika maneno yote ya sheria hii kwa wazi sana juu ya mawe haya ambayo mmesimamisha.”
9Kisha Musa na makuhani, ambao ni Walawi, wakawaambia Israeli wote, “Nyamaza ee Israeli, sikiliza! Sasa umekuwa taifa la Bwana Mungu wako.
10Mtii Bwana Mungu wako, na kufuata amri zake na maagizo ninayokupa leo.”
11Siku ile ile Musa akawaagiza watu:
12Mtakapovuka Mto Yordani, makabila haya yatasimama juu ya Mlima Gerizimu kubariki watu: Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari, Yusufu na Benyamini.
13Makabila haya yatasimama juu ya Mlima Ebali kwa kutamka laana: Reubeni, Gadi, Asheri, Zabuloni, Dani na Naftali.
14Nao Walawi watawasomea watu wote wa Israeli kwa sauti kubwa:
15“Alaaniwe mtu afanyaye sanamu ya kuchonga au mwenye kusubu sanamu, kitu ambacho ni chukizo kwa Bwana , kazi ya mikono ya fundi stadi, na kuisimamisha kwa siri.”
16“Alaaniwe mtu amdharauye baba yake na mama yake.”
17“Alaaniwe mtu asogezaye jiwe la mpaka wa jirani yake.”
18“Alaaniwe mtu ampotoshaye kipofu njiani.”
19“Alaaniwe mtu apotoshaye haki ya mgeni, yatima au mjane.”
20“Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na mke wa baba yake, kwa maana anadharau malazi ya baba yake.”
21“Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na mnyama yeyote.”
22“Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na dada yake, binti ya baba yake au binti ya mama yake.”
23“Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na mama mkwe wake.”
24“Alaaniwe mtu amuuaye jirani yake kwa siri.”
25“Alaaniwe mtu apokeaye rushwa ili kumuua mtu asiye na hatia.”
26“Alaaniwe mtu yule ambaye hatashikilia maneno ya sheria hii kwa kuyatekeleza.”