The chat will start when you send the first message.
1Sikia sasa, ee Israeli, amri na sheria nitakazokufundisha wewe. Zifuate ili upate kuishi na uingie kuimiliki nchi ambayo Bwana , Mungu wa baba zako, anawapa.
2Usiongeze wala usipunguze chochote ninachowaamuru ninyi, ila myashike maagizo ya Bwana Mungu wenu ambayo nawapa.
3Mliona kwa macho yenu wenyewe kile Bwana alichokifanya kule Baal-Peori. Bwana Mungu wenu aliwaangamiza kutoka miongoni mwenu kila mmoja aliyemfuata Baali wa Peori,
4lakini ninyi nyote mlioshikamana na Bwana kwa uthabiti, Mungu wenu, mko hai hadi leo.
5Tazama, nimewafundisha amri na sheria kama Bwana Mungu wangu alivyoniamuru mimi, ili mzifuate katika nchi mnayoiingia kuimiliki.
6Zishikeni kwa uangalifu, kwa kuwa hii itaonesha hekima na ufahamu wenu kwa mataifa, ambayo yatasikia kuhusu amri zote hizi, nao watasema, “Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na ufahamu.”
7Ni taifa gani jingine lililo kubwa kiasi cha kuwa na miungu yao iliyo karibu nao kama Bwana Mungu wetu alivyo karibu nasi wakati wowote tunapomwomba?
8Nalo ni taifa gani jingine lililo kubwa hivi lenye kuwa na amri na sheria za haki kama hizi ninazoweka mbele yenu leo?
9Mwe waangalifu na makini ili msije mkasahau mambo ambayo mliyaona kwa macho yenu, wala kuyaacha yaondoke mioyoni mwenu siku zote za uhai wenu. Mwafundishe hayo watoto wenu na watoto wao baada yao.
10Kumbuka siku uliyosimama mbele za Bwana Mungu wako kule Horebu aliponiambia, “Wakutanishe watu mbele yangu wasikie maneno yangu ili waweze kujifunza kuniheshimu kwa muda wote watakaoishi katika nchi, nao waweze kuwafundisha watoto wao maneno hayo.”
11Mlisogea karibu na mkasimama chini ya mlima wakati ulipowaka moto hadi juu mbinguni, pamoja na mawingu meusi na giza nene.
12Ndipo Bwana alipozungumza nanyi kutoka kati ya moto. Mkasikia sauti ya maneno lakini hamkuona umbo, kulikuwa na sauti tu.
13Aliwatangazia agano lake, hizo Amri Kumi ambazo aliwaamuru mzifuate, kisha akaziandika juu ya vibao viwili vya mawe.
14Naye Bwana alinielekeza wakati huo kuwafundisha ninyi sheria na amri ambazo mnapaswa kuzifuata katika nchi ambayo mnavuka Yordani kuimiliki.
15Hamkuona umbo la aina yoyote siku ambayo Bwana alizungumza nanyi kule Horebu kutoka kati ya moto. Kwa hiyo mjihadhari kwa uangalifu sana,
16ili msije mkajichafua na kujitengenezea sanamu au kinyago chenye umbo lolote kama la mwanaume au mwanamke,
17au kama mnyama aliye juu ya nchi au ndege yeyote arukaye angani,
18au kama kiumbe kinachotambaa juu ya ardhi, au samaki yeyote aliye ndani ya maji.
19Na utazamapo juu angani na ukaliona jua, mwezi na nyota na vyote vinavyoipamba mbingu, usije ukashawishiwa kuviinamia na kuviabudu vitu ambavyo Bwana Mungu wenu alivigawia mataifa yote chini ya mbingu.
20Lakini ninyi, Bwana amewatoa kutoka tanuru la kuyeyushia chuma, kutoka Misri, kuwa watu wa urithi wake, kama mlivyo sasa.
21Bwana alinikasirikia kwa sababu yenu na akaapa kwamba sitavuka Yordani kuingia katika nchi nzuri Bwana Mungu wenu anayowapa kuwa urithi wenu.
22Nitakufa katika nchi hii; sitavuka Yordani, lakini ninyi ni karibu mvuke mkaimiliki ile nchi nzuri.
23Jihadharini msilisahau agano la Bwana Mungu wenu lile alilofanya nanyi; msijitengenezee sanamu katika umbo la kitu chochote ambacho Bwana Mungu wenu amewakataza.
24Kwa kuwa Bwana Mungu wenu ni moto ulao, Mungu mwenye wivu.
25Baada ya kuwa na watoto na wajukuu na kuishi katika nchi hiyo siku nyingi, tena mkijichafua na kutengeneza sanamu ya aina yoyote, mkifanya maovu machoni pa Bwana Mungu wenu na kumfanya awe na hasira,
26ninaziita mbingu na nchi kama mashahidi dhidi yenu siku hii kwamba mtaangamia mara moja kutoka katika nchi ile ambayo mnavuka Yordani kuimiliki. Hamtaishi kule kwa muda mrefu bali kwa hakika mtaangamizwa.
27Bwana atawatawanya miongoni mwa mataifa, na ni wachache wenu tu watakaosalia miongoni mwa mataifa hayo ambayo Bwana atawafukuzia.
28Huko mtaabudu miungu ya miti na mawe iliyotengenezwa na watu, ambayo haiwezi kuona au kusikia wala kula au kunusa.
29Lakini kama mtamtafuta Bwana Mungu wenu, mtampata; kama mtamtafuta kwa moyo wote na kwa roho yote.
30Mnapokuwa katika dhiki, nayo mambo haya yote yamewatokea siku hizo, ndipo mtamrudia Bwana Mungu wenu na kumtii.
31Kwa maana Bwana Mungu wenu ni Mungu mwenye huruma, hatawaacha au kuwaangamiza wala kusahau agano alilofanya na baba zenu, alilowathibitishia kwa kiapo.
32Sasa uliza kuhusu siku za zamani, zamani kabla ya wakati wako, tangu siku ile Mungu alipomuumba mtu juu ya nchi, uliza kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwisho mwingine wa mbingu. Je, kumepata kutokea jambo jingine lililo kubwa kama hili, au kuna jambo jingine kama hilo limepata kusikiwa?
33Je, kuna watu wengine wowote waliosikia sauti ya Mungu ikizungumza kwenye moto, kama mlivyosikia, nao wakaishi?
34Je, kuna mungu yeyote amepata kujaribu mwenyewe kuchukua taifa moja kutoka taifa lingine, kwa mapigo, kwa ishara za miujiza na maajabu, kwa vita, kwa mkono wenye nguvu na mkono ulionyooshwa au kwa matendo makuu ya kutisha, kama yale ambayo Bwana Mungu wenu aliyofanya kwa ajili yenu huko Misri mbele ya macho yenu?
35Mlioneshwa mambo haya ili mpate kujua kuwa Bwana ndiye Mungu; hakuna mwingine ila yeye.
36Kutoka mbinguni amewasikizisha sauti yake ili kuwaadilisha. Hapa duniani aliwaonesha moto wake mkubwa, nanyi mlisikia maneno yake kutoka kati ya ule moto.
37Kwa sababu aliwapenda baba zenu na alichagua wazao wao baada yao, aliwatoa katika nchi ya Misri kwa Uwepo wake na kwa uwezo wake mkuu,
38aliwafukuza mbele yenu mataifa makubwa na yenye nguvu kuliko ninyi na kuwaleta ninyi katika nchi yao na akawapa ninyi kuwa urithi wenu, kama ilivyo leo.
39Kubalini na mweke moyoni leo kuwa Bwana ndiye Mungu mbinguni juu na duniani chini. Hakuna mwingine.
40Mshike amri na maagizo yake ninayowapa leo, ili mpate kufanikiwa ninyi na watoto wenu baada yenu, na mpate kuishi maisha marefu katika nchi anayowapa Bwana Mungu wenu siku zote.
41Kisha Musa akatenga miji mitatu mashariki mwa Yordani,
42ambayo mtu yeyote aliyemuua mtu angeweza kukimbilia ikiwa amemuua jirani yake bila kukusudia na bila kuwa na chuki naye siku zilizopita. Angeweza kukimbilia katika mmoja ya miji hii na kuokoa maisha yake.
43Miji hiyo ilikuwa: Bezeri katika tambarare ya jangwa kwa ajili ya Wareubeni; Ramothi katika nchi ya Gileadi kwa ajili ya Wagadi; nao mji wa Golani katika nchi ya Bashani kwa ajili ya Wamanase.
44Hii ndiyo sheria Musa aliyoweka mbele ya Waisraeli.
45Haya ndio masharti, amri na sheria Musa alizowapa Waisraeli walipotoka Misri,
46nao walikuwa katika bonde karibu na Beth-Peori mashariki mwa Yordani, katika nchi ya Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alitawala Heshboni; naye alishindwa na Musa na Waisraeli walipotoka Misri.
47Waliimiliki nchi yake na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani, wafalme wawili Waamori waliotawala mashariki mwa Yordani.
48Nchi hii ilienea kutoka Aroeri ukingoni mwa Bonde la Arnoni hadi Mlima Sioni (yaani Hermoni),
49pamoja na eneo lote la Araba mashariki mwa Yordani, na kuenea hadi Bahari ya Araba kwenye miteremko ya Pisga.