Kumbukumbu 7

Kumbukumbu 7

Kuyafukuza mataifa

(Kut 34:11‑16)

1Bwana Mungu wako akuletapo katika nchi unayoingia kuimiliki, na awafukuzapo mbele yako mataifa mengi, yaani Wahiti, Wagirgashi, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, mataifa saba makubwa tena yenye nguvu kuliko wewe,

2pia Bwana Mungu wako atakapowatia mkononi mwako na ukawashinda, basi ni lazima uwaangamize wote kabisa. Usifanye agano nao, wala usiwahurumie.

3Usioane nao. Usimtoe binti yako kuolewa na mwanawe, au kumchukua binti yake aolewe na mwanao.

4Kwa maana watamgeuza mwanao aache kunifuata, ili aitumikia miungu mingine, nayo hasira ya Bwana itawaka dhidi yako, naye atakuangamiza ghafula.

5Hili ndilo utakalowafanyia: Vunja madhabahu yao, vunja mawe yao ya kuabudia, katakata nguzo zao za Ashera, na kuchoma sanamu zao kwa moto;

6kwa kuwa wewe ni taifa takatifu kwa Bwana Mungu wako. Bwana Mungu wako amekuchagua kutoka mataifa yote duniani uwe taifa lake, hazina yake ya pekee.

7Bwana hakuweka upendo wake juu yenu na kuwachagua kwa sababu mlikuwa wengi mno kuliko watu wengine, kwa maana ninyi ndio mliokuwa wachache sana kuliko mataifa yote.

8Lakini ni kwa sababu Bwana aliwapenda ninyi na kutunza kiapo alichowaapia babu zenu kwamba atawatoa ninyi kwa mkono wenye nguvu na kuwakomboa kutoka nchi ya utumwa, kutoka nguvu za Farao mfalme wa Misri.

9Basi ujue kwamba Bwana Mungu wako ndiye Mungu; ni Mungu mwaminifu, anayetunza agano la upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanaompenda na kuzishika amri zake.

10Lakini

kwa wale wanaomchukia

atawalipiza kwenye nyuso zao

kwa maangamizi;

hatachelewa kuwalipiza kwenye nyuso zao

wale wamchukiao.

11Kwa hiyo, kuweni waangalifu kufuata maagizo, amri na sheria ninazowapa leo.

Baraka za utiifu

(Kum 28:1‑14)

12Mkizingatia sheria hizi na kuzifuata kwa uangalifu, basi Bwana Mungu wenu atatunza agano lake la upendo nanyi, kama alivyowaapia baba zenu.

13Atawapenda ninyi na kuwabariki na kuongeza idadi yenu. Atabariki uzao wa tumbo lenu, mazao ya nchi yenu, nafaka, divai mpya na mafuta, ndama za ngʼombe wa makundi yenu, na kondoo wa makundi yenu katika nchi ile aliyoapa kuwapa baba zenu.

14Mtabarikiwa kuliko mataifa mengine yote, hakuna wanaume wala wanawake kwenu watakaokosa watoto, wala mifugo yenu haitakuwa tasa.

15Bwana atawakinga na kila ugonjwa. Mungu hatatia juu yenu ugonjwa wowote mbaya mlioufahamu huko Misri, lakini atatia ugonjwa juu ya wale wote wanaokuchukia.

16Ni lazima mwangamize watu wote ambao Bwana Mungu wenu atawatia mikononi mwenu. Msiwatazame kwa kuwahurumia na msiitumikie miungu yao, kwa kuwa itakuwa mtego kwenu.

17Mnaweza kujiuliza wenyewe: “Mataifa haya ni yenye nguvu kuliko sisi. Tutawezaje kuwafukuza?”

18Lakini msiwaogope. Kumbukeni vyema jinsi Bwana Mungu wenu alivyofanya kwa Farao na kwa wote huko Misri.

19Mliona kwa macho yenu wenyewe majaribu makubwa, ishara za miujiza na maajabu, mkono wenye nguvu na ulionyooshwa, ambao kwa huo Bwana Mungu wenu aliwatoa mtoke Misri. Bwana Mungu wenu atawafanyia hivyo watu wote ambao mnawaogopa sasa.

20Zaidi ya hayo, Bwana Mungu wenu atatuma nyigu miongoni mwao hadi yale mabaki watakaojificha waangamie.

21Msiingiwe na hofu kwa sababu yao, kwa kuwa Bwana Mungu wenu, ambaye yupo miongoni mwenu ni mkuu naye ni Mungu wa kutisha.

22Bwana Mungu wenu atawafukuza mataifa hayo mbele yenu kidogo kidogo. Hamtaruhusiwa kuwaondoa wote kwa mara moja, la sivyo wanyama pori wataongezeka na kuwa karibu nanyi.

23Lakini Bwana Mungu wenu atawatia watu hao mikononi mwenu, akiwatia katika machafuko makubwa hadi waangamizwe.

24Atawatia wafalme wao mikononi mwenu, nanyi mtayafuta majina yao chini ya mbingu. Hakuna hata mmoja atakayeweza kusimama dhidi yenu bali mtawaangamiza.

25Sanamu za miungu yao mtazichoma moto. Msitamani fedha wala dhahabu iliyo juu ya vinyago hivyo, wala msiichukue iwe yenu, la sivyo mtakuwa mmetekwa nayo. Kwa kuwa ni chukizo kwa Bwana Mungu wenu.

26Msilete vitu vya machukizo katika nyumba zenu kwani ninyi, mtatengwa kama vitu hivyo kwa maangamizi. Ukichukie kabisa kitu hicho kwa kuwa kimetengwa kwa maangamizi.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.