Mhubiri 10

Mhubiri 10

1Kama vile inzi waliokufa huacha harufu mbaya kwenye manukato,

ndivyo upumbavu kidogo huzidi nguvu hekima na heshima.

2Moyo wa mwenye hekima huelekea kuume,

lakini moyo wa mpumbavu huelekea kushoto.

3Hata anapotembea barabarani,

mpumbavu hukosa ufahamu

na kudhihirisha kwa kila mmoja

jinsi alivyo mpumbavu.

4Kama hasira ya mtawala ikiwaka dhidi yako,

usiache mahali pako,

utulivu huweza kuzuia makosa mengi.

5Kuna ubaya niliouona chini ya jua,

aina ya kosa litokalo kwa mtawala:

6Wapumbavu kuwekwa kwenye nafasi nyingi za utawala,

hali matajiri wanashika nafasi za chini.

7Mimi nimeona watumwa wamepanda farasi,

wakati wakuu wakitembea

kwa miguu kama watumwa.

8Yeye achimbaye shimo

aweza kutumbukia ndani yake,

yeyote abomoaye ukuta

anaweza kuumwa na nyoka.

9Yeyote apasuaye mawe

inawezekana yakamuumiza,

yeyote apasuaye magogo

inawezekana yakamuumiza.

10Kama shoka ni butu

na halikunolewa,

nguvu nyingi zinahitajika,

lakini ustadi utaleta mafanikio.

11Nyoka akiuma kabla ya kuchezeshwa,

mchezeshaji hatahitajika tena.

12Maneno yanayotoka kinywani mwa mtu mwenye hekima yana neema,

bali mpumbavu huangamizwa

na midomo yake mwenyewe.

13Mwanzoni maneno yake ni upumbavu,

mwishoni ni wazimu mbaya,

14naye mpumbavu huzidisha maneno.

Hakuna yeyote ajuaye linalokuja,

ni nani awezaye kueleza ni jambo gani

litakalotokea baada yake?

15Kazi ya mpumbavu humchosha mwenyewe,

hajui njia iendayo mjini.

16Ole wako, ee nchi ambayo mfalme wako alikuwa mtumwa

na ambayo wakuu wako hufanya karamu asubuhi.

17Heri wewe, ee nchi ambayo mfalme wako

ni wa uzao wenye kuheshimika,

na ambayo wakuu wako hula chakula

kwa wakati unaofaa:

wao hula ili kupata nguvu

na si kwa ajili ya ulevi.

18Kama mtu ni mvivu, paa la nyumba huinama;

kutokana na mikono milegevu, nyumba huvuja.

19Karamu hufanywa kwa ajili ya kicheko,

nao mvinyo hufurahisha maisha,

lakini fedha ni jawabu la mambo yote.

20Usimshutumu mfalme hata ikiwa ni katika mawazo yako,

au kumlaani tajiri katika chumba chako cha kulala,

kwa sababu ndege wa angani wanaweza kuchukua maneno yako,

naye ndege anayeruka anaweza kutoa taarifa ya yale uliyosema.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.