Kutoka 10

Kutoka 10

Pigo la nane: Nzige

1Ndipo Bwana akamwambia Musa, “Nenda kwa Farao, kwa kuwa nimeufanya moyo wake kuwa mgumu na mioyo ya maafisa wake ili nipate kutenda ishara hizi zangu za ajabu miongoni mwao,

2ili upate kuwaeleza watoto wako na wajukuu wako jinsi nilivyowatendea Wamisri kwa ukali, na jinsi nilivyofanya ishara zangu miongoni mwao, nanyi mpate kujua kuwa Mimi ndimi Bwana .”

3Kwa hiyo Musa na Haruni wakaenda kwa Farao na kumwambia, “Hili ndilo Bwana , Mungu wa Waebrania, asemalo: ‘Utaendelea hata lini kukataa kunyenyekea mbele yangu? Waachie watu wangu waende, ili waniabudu.

4Ukikataa kuwaachia waende, kesho nitaleta nzige katika nchi yako.

5Nao watafunika uso wa ardhi hata usionekane. Watatafuna mabaki machache yaliyobakizwa baada ya ile mvua ya mawe, yaani pamoja na kila mti unaoota katika mashamba yenu.

6Nzige hao watajaza nyumba zako, za maafisa wako wote na za Wamisri wote. Jambo ambalo baba zenu wala babu zenu hawajapata kuona tangu siku ile walipoanza kuishi katika nchi hii hadi leo.’ ” Ndipo Musa akageuka na kumwacha Farao.

7Maafisa wa Farao wakamwambia, “Hadi lini huyu mtu atakuwa tanzi kwetu? Waachie hao watu waende zao, ili wapate kumwabudu Bwana Mungu wao. Je, bado hutambui kuwa Misri imeangamia?”

8Ndipo Musa na Haruni wakaletwa kwa Farao. Farao akawaambia, “Nendeni, mkamwabudu Bwana Mungu wenu. Lakini ni nani hasa watakaoenda?”

9Musa akajibu, “Tutaenda na vijana wetu na wazee, pamoja na wana wetu na binti zetu, pia pamoja na mbuzi, kondoo, na ngʼombe wetu kwa sababu tutaadhimisha sikukuu kwa Bwana .”

10Farao akasema, “Kama kweli nitawaruhusu mwondoke pamoja na wanawake wenu na watoto wenu, Bwana awe pamoja nanyi! Ni wazi kwamba mna makusudi mabaya.

11La hasha! Wanaume peke yao na waende, wakamwabudu Bwana , kwa kuwa hilo ndilo mmekuwa mkiomba.” Kwa hiyo Musa na Haruni wakaondolewa mbele ya Farao.

12Basi Bwana akamwambia Musa, “Nyoosha mkono wako juu ya Misri, ili kundi la nzige liweze kuvamia nchi na kutafuna kila kitu kinachoota katika mashamba na kila kitu kilichosazwa na ile mvua ya mawe.”

13Kwa hiyo Musa akanyoosha fimbo yake juu ya Misri, Bwana akauleta upepo wa mashariki ukavuma katika nchi yote mchana wote na usiku kucha, kufikia asubuhi upepo ukawa umeleta nzige.

14Wakaivamia Misri yote na kukaa katika kila eneo la nchi kwa wingi. Kamwe halijapata kutokea pigo la nzige kama hilo, wala halitakuwa tena.

15Wakafunika ardhi yote hata ardhi ikawa nyeusi. Wakatafuna kila kilichokuwa kimebakizwa na ile mvua ya mawe: kila kitu kilichoota shambani, pamoja na matunda kwenye miti. Hakuna kitu chochote cha kijani kilichosalia katika miti au mmea katika nchi yote ya Misri.

16Farao akawaita Musa na Haruni kwa haraka na kuwaambia, “Nimetenda dhambi dhidi ya Bwana Mungu wenu na dhidi yenu pia.

17Sasa unisamehe dhambi yangu mara moja tena na umwombe Bwana Mungu wako aondoe pigo hili baya kwangu.”

18Kisha Musa akaondoka kwa Farao akamwomba Bwana .

19Naye Bwana akaugeuza upepo kuwa upepo mkali sana kutoka magharibi, ambao uliwaondoa wale nzige na kuwapeleka kwenye Bahari ya Shamu. Hakuna nzige hata mmoja aliyebaki popote katika nchi ya Misri.

20Lakini Bwana akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, wala hakuwaachia Waisraeli waondoke.

Pigo la tisa: Giza

21Kisha Bwana akamwambia Musa, “Nyoosha mkono wako kuelekea angani ili giza litande katika nchi ya Misri, giza ambalo watu wanaweza kulipapasa na kulihisi.”

22Kwa hiyo Musa akaunyoosha mkono wake kuelekea angani, na giza nene likafunika pote katika nchi ya Misri kwa muda wa siku tatu.

23Hakuna mtu yeyote aliyeweza kumwona mwenzake, wala kuondoka mahali alipokuwa kwa muda wa siku tatu. Lakini Waisraeli wote walikuwa na mwanga katika maeneo waliyokuwa wanaishi.

24Ndipo Farao akamwita Musa na kusema, “Nendeni, mkamwabudu Bwana . Hata wanawake na watoto wenu mwaweza kwenda nao pia, lakini kondoo, mbuzi na ngʼombe wenu waacheni.”

25Lakini Musa akasema, “Huna budi kuturuhusu tuwe na dhabihu, na sadaka za kuteketezwa za kutoa mbele za Bwana Mungu wetu.

26Sisi ni lazima tuondoke na mifugo yetu pia, wala hakuna ukwato utakaoachwa nyuma. Inatupasa kutumia baadhi ya hiyo mifugo katika kumwabudu Bwana Mungu wetu, kwa kuwa hadi tutakapofika huko, hatutakuwa tumefahamu ni nini tutakachotumia katika kumwabudu Bwana .”

27Lakini Bwana akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, hakuwa radhi kuwaachia waondoke.

28Farao akamwambia Musa, “Ondoka mbele yangu! Hakikisha kuwa hutakuja mbele yangu tena! Siku ile utakapouona uso wangu utakufa.”

29Musa akamjibu, “Iwe kama ulivyosema! Kamwe sitauona uso wako tena.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.