Kutoka 13

Kutoka 13

Kuwekwa wakfu kwa wazaliwa wa kwanza

1Bwana akamwambia Musa,

2“Niwekeeni wakfu kila mzaliwa wa kwanza wa kiume. Kila mtoto wa kwanza aliye kifungua mimba miongoni mwa Waisraeli ni mali yangu, akiwa wa mwanadamu au wa mnyama.”

3Ndipo Musa akawaambia watu, “Ikumbukeni siku hii, siku ambayo mlitoka katika nchi ya Misri, katika nchi ya utumwa, kwa sababu Bwana aliwatoa humo kwa mkono wenye nguvu. Msile chochote kilichotiwa chachu.

4Leo, katika mwezi wa Abibu, mnatoka.[#13:4 mwezi wa kwanza katika kalenda ya Kiyahudi]

5Bwana atakapokuleta katika nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Wahivi na Wayebusi, nchi aliyowaapia baba zako kukupa, nchi inayotiririka maziwa na asali, utaiadhimisha sikukuu hii katika mwezi huu:

6Kwa siku saba utakula mikate isiyotiwa chachu na katika siku ya saba utamfanyia Bwana sikukuu.

7Kwa muda wa siku saba utakula mikate isiyotiwa chachu, pasionekane kitu chochote kilicho na chachu miongoni mwako, wala chachu yoyote isionekane popote ndani ya mipaka yako.

8Siku ile utamwambia mwanao, ‘Nafanya hivi kwa sababu ya jambo ambalo Bwana alinitendea nilipotoka katika nchi ya Misri.’

9Adhimisho hili, litakuwa kama alama kwenye mkono wako na ukumbusho katika paji lako la uso, kwamba sheria ya Bwana inapaswa iwe kinywani mwako. Kwa kuwa Bwana alikutoa katika nchi ya Misri kwa mkono wake wenye nguvu.

10Ni lazima ulishike agizo hili kwa wakati uliopangwa mwaka baada ya mwaka.

11“Baada ya Bwana kukuingiza katika nchi ya Wakanaani na kukupa nchi hiyo, kama alivyokuahidi kwa kiapo na kwa baba zako,

12inakupasa kumtolea Bwana kila mzaliwa wa kwanza. Wazaliwa wote wa kwanza wa kiume wa mifugo yako ni mali ya Bwana .

13Kila mzaliwa wa kwanza wa punda utamkomboa kwa mwana-kondoo, lakini kama hutamkomboa, utamvunja shingo yake. Kila mzaliwa wa kwanza mwanaume miongoni mwa wana wenu utamkomboa.

14“Katika siku zijazo, mwanao akikuuliza, ‘Hii ina maana gani?’ Mwambie, ‘Kwa mkono wenye nguvu Bwana alitutoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa.

15Farao alipokataa kwa ukaidi kuturuhusu kuondoka, Bwana aliua kila mzaliwa wa kwanza wa Wamisri, mwanadamu na wa mnyama. Hii ndiyo sababu ninatoa dhabihu kwa Bwana mzaliwa wa kwanza wa kiume wa kila tumbo, na kumkomboa kila mzaliwa wa kwanza wa wana wangu.’

16Jambo hili litakuwa kama ishara kwenye mkono wako na kama alama kwenye paji la uso wako, kwamba Bwana alikutoa katika nchi ya Misri kwa mkono wake wenye nguvu.”

Nguzo ya wingu na moto

17Farao alipowaachia watu waende, Mungu hakuwaongoza kufuata njia ipitayo katika nchi ya Wafilisti, ingawa njia hiyo ilikuwa fupi zaidi. Kwa maana Mungu alisema, “Wakikabiliana na vita, wanaweza kubadili mawazo yao na kurudi Misri.”

18Kwa hiyo Mungu akawaongoza watu kupitia njia ya kuzunguka kupitia jangwani, kuelekea Bahari ya Shamu. Waisraeli walipanda kutoka nchi ya Misri wakiwa wamejiandaa kwa vita.

19Musa akachukua mifupa ya Yusufu kwa sababu Yusufu alikuwa amewaapisha wana wa Israeli. Alikuwa amewaambia, “Hakika Mungu atakuja kuwasaidia, nanyi ni lazima mwichukue mifupa yangu mwende nayo kutoka mahali hapa.”[#13:19 taz. Mwa 50:25]

20Baada ya Waisraeli kuondoka Sukothi wakapiga kambi huko Ethamu pembeni mwa jangwa.

21Wakati wa mchana Bwana aliwatangulia kwa nguzo ya wingu kuwaongoza katika njia yao, na wakati wa usiku aliwatangulia kwa nguzo ya moto kuwaangazia, ili waweze kusafiri mchana au usiku.

22Ile nguzo ya wingu wakati wa mchana au ile nguzo ya moto wakati wa usiku haikuondoka mahali pake mbele ya watu.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.