Kutoka 15

Kutoka 15

Wimbo wa Musa na Miriamu

1Ndipo Musa na Waisraeli wakamwimbia Bwana wimbo huu:

“Nitamwimbia Bwana ,

kwa kuwa ametukuzwa sana.

Farasi na mpanda farasi

amewatosa baharini.

2“Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu;

amekuwa wokovu wangu.

Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu,

Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza.

3Bwana ni shujaa wa vita;

Bwana ndilo jina lake.

4Magari ya vita ya Farao na jeshi lake

amewatosa baharini.

Maafisa wa Farao walio bora sana

wamezamishwa katika Bahari ya Shamu.

5Maji yenye kina yamewafunika,

wamezama vilindini kama jiwe.

6Mkono wako wa kuume, Ee Bwana

ulitukuka kwa uweza.

Mkono wako wa kuume, Ee Bwana ,

ukamponda adui.

7“Katika ukuu wa utukufu wako,

ukawaangusha chini wale waliokupinga.

Uliachia hasira yako kali,

ikawateketeza kama kapi.

8Kwa pumzi ya pua yako

maji yalijilundika.

Mawimbi ya maji yakasimama imara kama ukuta,

vilindi vikagandamana ndani ya moyo wa bahari.

9Adui alijivuna,

‘Nitawafuatia, nitawapata.

Nitagawanya nyara;

nitajishibisha kwao.

Nitafuta upanga wangu

na mkono wangu utawaangamiza.’

10Lakini ulipuliza kwa pumzi yako,

bahari ikawafunika.

Wakazama kama risasi

kwenye maji makuu.

11Ni nani miongoni mwa miungu aliye kama wewe, Ee Bwana ?

Ni nani kama Wewe:

uliyetukuka katika utakatifu,

utishaye katika utukufu,

ukitenda maajabu?

12“Uliunyoosha mkono wako wa kuume

na nchi ikawameza.

13Katika upendo wako usiokoma utawaongoza

watu uliowakomboa.

Katika nguvu zako utawaongoza

hadi makao yako matakatifu.

14Mataifa watasikia na kutetemeka,

uchungu utawakamata Wafilisti.

15Wakuu wa Edomu wataogopa,

viongozi wa Moabu watatetemeka kwa hofu,

Wakanaani watayeyuka,

16vitisho na hofu vitawaangukia.

Kwa nguvu ya mkono wako

watatulia kama jiwe,

hadi watu wako wapite, Ee Bwana ,

hadi watu uliowanunua wapite.

17Utawaingiza na kuwapandikiza

juu ya mlima wa urithi wako:

hapo mahali, Ee Bwana ,

ulipopafanya kuwa makao yako,

mahali patakatifu, Ee Bwana ,

ulipopajenga kwa mikono yako.

18“Bwana atatawala

milele na milele.”

19Farasi wa Farao, magari yake ya vita na wapanda farasi wake walipoingia baharini, Bwana aliyarudisha maji ya bahari yakawafunika, lakini Waisraeli walipita baharini mahali pakavu.

20Kisha Miriamu yule nabii mke, ndugu yake Haruni, akachukua matari mkononi mwake na wanawake wote wakamfuata na matari yao wakicheza.

21Miriamu akawaimbia:

“Mwimbieni Bwana ,

kwa maana ametukuka sana.

Farasi na mpanda farasi

amewatosa baharini.”

Maji ya Mara na Elimu

22Kisha Musa akawaongoza Israeli kutoka Bahari ya Shamu na kuingia katika Jangwa la Shuri. Kwa siku tatu walisafiri jangwani bila kupata maji.

23Walipofika Mara, hawakuweza kunywa maji yake kwa sababu yalikuwa machungu. (Ndiyo sababu mahali hapo panaitwa Mara.)[#15:23 maana yake Chungu]

24Kwa hiyo watu wakamnungʼunikia Musa, wakisema, “Tunywe nini?”

25Ndipo Musa akamlilia Bwana , naye Bwana akamwonesha kipande cha mti. Akakitupa ndani ya maji, nayo maji yakawa matamu.

Huko Bwana akawapa amri na sheria na huko akawajaribu.

26Mungu akasema, “Mkisikiliza kwa makini sauti ya Bwana Mungu wenu na kuyafanya yaliyo mema machoni pake, na mkiyatii maagizo yake na kuzishika amri zake zote, sitaleta juu yenu ugonjwa wowote niliowaletea Wamisri, kwa kuwa Mimi ndimi Bwana , niwaponyaye.”

27Kisha wakafika Elimu, mahali palipokuwa na chemchemi kumi na mbili, na miti sabini ya mitende, wakapiga kambi huko karibu na maji.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.