Kutoka 32

Kutoka 32

Ndama wa dhahabu

(Kum 9:6‑29)

1Watu walipoona kuwa Musa amekawia sana kushuka kutoka mlimani, walimsonga Haruni na kumwambia, “Njoo, tutengenezee miungu itakayotutangulia. Kwa maana huyu jamaa yetu Musa aliyetupandisha kutoka Misri, hatujui yaliyompata.”

2Haruni akawajibu, “Vueni vipuli vya dhahabu ambavyo wake zenu, wana wenu, na binti zenu wamevaa, mkaniletee.”

3Kwa hiyo watu wote wakavua vipuli vyao, wakavileta kwa Haruni.

4Akavichukua vile vitu walivyomkabidhi, akasubu sanamu yenye umbo la ndama, akaichonga kwa kutumia chombo. Kisha wakasema, “Hii ndiyo miungu yenu, ee Israeli, iliyowapandisha kutoka Misri.”

5Haruni alipoona hili, akajenga madhabahu mbele ya yule ndama na kutangaza, “Kesho kutakuwa na sikukuu kwa Bwana .”

6Kwa hiyo siku iliyofuata watu wakaamka asubuhi na mapema na kutoa sadaka za kuteketeza na sadaka za amani. Baadaye watu wakaketi kula na kunywa, nao wakasimama, wakajizamisha katika sherehe.

7Kisha Bwana akamwambia Musa, “Shuka, kwa sababu watu wako, uliowatoa Misri, wamepotoka.

8Wamekuwa wepesi kugeuka na kuacha niliyowaamuru, na wamejitengenezea sanamu ya kusubu yenye umbo la ndama. Wameisujudia na kuitolea dhabihu, nao wamesema, ‘Hii ndiyo miungu yenu, ee Israeli iliyokupandisha kutoka Misri.’ ”

9Bwana akamwambia Musa, “Nimeona watu hawa, nao ni watu wenye shingo ngumu.

10Sasa niache ili hasira yangu ipate kuwaka dhidi yao, nami nipate kuwaangamiza. Kisha nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa.”

11Lakini Musa akamsihi Bwana Mungu wake, akasema, “Ee Bwana , kwa nini hasira yako iwake dhidi ya watu wako, wale uliowatoa Misri kwa uweza mkuu na mkono wenye nguvu?

12Kwa nini Wamisri waseme, ‘Ni kwa nia mbaya aliwatoa Misri, ili awaue milimani na kuwafuta usoni mwa dunia’? Achilia mbali hasira yako kali, waonee huruma na usilete maafa juu ya watu wako.

13Wakumbuke watumishi wako Abrahamu, Isaka na Israeli, ambao uliwaapia kwa nafsi yako mwenyewe: ‘Nitawafanya uzao wako kuwa wengi kama nyota za angani, nami nitawapa wazao wako nchi hii yote niliyowaahidia, nayo itakuwa urithi wao milele.’ ”

14Kisha Bwana akawaonea huruma, wala hakuleta juu ya watu wake maafa aliyokuwa amekusudia.

15Musa akageuka, akateremka kutoka mlimani akiwa na vile vibao viwili vya Ushuhuda mikononi mwake. Vilikuwa vimeandikwa pande zote mbili, mbele na nyuma.

16Vibao hivyo vilikuwa kazi ya Mungu; maandishi yalikuwa mwandiko wa Mungu, yaliyochorwa kama muhuri juu ya vibao.

17Yoshua aliposikia sauti za watu wakipiga kelele, akamwambia Musa, “Kuna sauti ya vita kambini.”

18Musa akajibu:

“Si sauti ya ushindi,

wala si sauti ya kushindwa;

ni sauti ya kuimba ninayosikia.”

19Musa alipoikaribia kambi na kuona yule ndama na ile michezo, hasira yake ikawaka, akatupa vile vibao vilivyokuwa mikononi mwake, akavipasua vipande vipande pale chini ya mlima.

20Kisha akamchukua yule ndama waliokuwa wamemtengeneza na kumchoma kwenye moto, kisha akamsaga kuwa unga, akanyunyiza kwenye maji na kuwafanya Waisraeli wanywe.

21Musa akamwambia Haruni, “Watu hawa walikufanyia nini, hata ukawaongoza kufanya dhambi kubwa hivyo?”

22Haruni akamwambia, “Usikasirike bwana wangu. Unajua jinsi watu hawa walivyo tayari kwa maovu.

23Waliniambia, ‘Tufanyie miungu itakayotuongoza. Kwa kuwa huyu jamaa yetu Musa aliyetupandisha kutoka Misri, hatujui yaliyompata.’

24Kwa hiyo nikawaambia, ‘Yeyote aliye na kito chochote cha dhahabu avue.’ Kisha wakanipa hiyo dhahabu, nami nikaitupa motoni, akatokea huyu ndama!”

25Musa akaona kuwa watu wameasi, kwa kuwa Haruni alikuwa amewaacha waasi, na hivyo kuwa kichekesho kwa adui zao.

26Kwa hiyo Musa akasimama kwenye ingilio la kambi, akasema, “Yeyote aliye upande wa Bwana , aje upande wangu.” Walawi wote wakamjia.

27Ndipo alipowaambia, “Hili ndilo Bwana , Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Kila mmoja wenu ajifunge upanga wake kiunoni aende huku na huko kambi yote mwisho hadi mwisho mwingine, kila mmoja amuue ndugu yake, na rafiki yake na jirani yake.’ ”

28Walawi wakafanya kama Musa alivyoamuru, siku ile wakafa watu wapatao elfu tatu.

29Kisha Musa akasema, “Leo mmewekwa wakfu kwa Bwana , kwa kuwa mlikuwa kinyume na wana wenu wenyewe na ndugu zenu, naye Mungu amewabariki leo.”

30Siku iliyofuata Musa akawaambia watu, “Mmefanya dhambi kubwa. Lakini sasa nitapanda juu kwa Bwana , labda nitaweza kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu.”

31Hivyo Musa akarudi kwa Bwana na kumwambia, “Lo! Hawa watu wamefanya dhambi kubwa namna gani! Wamejitengenezea miungu ya dhahabu.

32Lakini sasa nakusihi, wasamehe dhambi yao; lakini kama sivyo, basi nifute kutoka kitabu ulichoandika.”

33Bwana akamjibu Musa, “Yeyote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta kutoka kitabu changu.

34Sasa nenda, uongoze hao watu hadi mahali nilipokuambia, naye malaika wangu atakutangulia. Pamoja na hayo, wakati utakapofika wa mimi kuwaadhibu, nitawaadhibu kwa ajili ya dhambi yao.”

35Ndipo Bwana akawapiga watu kwa ugonjwa wa tauni kwa sababu ya yale waliyoyafanya na ndama yule ambaye alitengenezwa na Haruni.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.