Kutoka 36

Kutoka 36

2Ndipo Musa akawaita Bezaleli na Oholiabu na kila mtu mwenye ustadi ambaye Bwana alikuwa amempa uwezo na mwenye kupenda kuja na kufanya kazi.

3Wakapokea kutoka kwa Musa sadaka zote ambazo Waisraeli walikuwa wameleta ili kuifanya kazi ya ujenzi wa Mahali Patakatifu. Nao watu wakaendelea kuleta sadaka za hiari kila asubuhi.

4Ikafika wakati mafundi wote wenye ujuzi waliokuwa wakiifanya kazi yote ya mahali patakatifu wakasimamisha kazi zao,

5wakaja na kumwambia Musa, “Watu wanaleta vitu vingi kuliko tunavyohitaji kwa ajili ya kazi hii ambayo Bwana ameagiza ifanyike.”

6Ndipo Musa akatoa agizo, nao wakapeleka neno hili katika kambi yote: “Mwanaume au mwanamke yeyote asilete tena kitu chochote kwa ajili ya sadaka ya mahali patakatifu.” Hivyo watu wakazuiliwa kuleta zaidi,

7kwa sababu walivyokuwa navyo tayari vilitosha na kuzidi kuifanya kazi yote.

Maskani ya Mungu

(Kut 26:1‑37)

8Watu wote wenye ustadi miongoni mwa wafanyakazi wote wakatengeneza maskani ya Mungu kwa mapazia kumi ya kitani iliyosokotwa vizuri, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu, naye fundi stadi akatirizi makerubi kwenye mapazia hayo.

9Mapazia yote yalitoshana kwa ukubwa: kila moja lilikuwa na urefu wa dhiraa ishirini na nane, na upana wa dhiraa nne.[#36:9 Dhiraa 28 ni sawa na mita 12.6.; #36:9 Dhiraa nne ni sawa na mita 1.8.]

10Wakayaunganisha mapazia matano pamoja, pia wakafanya vivyo hivyo kwa hayo mengine matano.

11Kisha wakatengeneza vitanzi vya kitambaa cha buluu kwenye upindo wa pazia la mwisho la fungu la kwanza, pia wakafanya vivyo hivyo na pazia la fungu la mwisho.

12Wakatengeneza pia vitanzi hamsini katika pazia mmoja, na vitanzi vingine hamsini kwenye pazia la mwisho la fungu hilo lingine, navyo vitanzi vyote vikaelekeana.

13Kisha wakatengeneza vifungo hamsini vya dhahabu, na wakavitumia kufunga na kuunganisha zile fungu mbili za mapazia pamoja ili maskani ya Mungu ipate kuwa kitu kimoja.

14Wakatengeneza mapazia kumi na moja ya singa za mbuzi kwa ajili ya kufunika Maskani.

15Mapazia hayo kumi na moja yalikuwa na kipimo sawa, yaani urefu wa dhiraa thelathini, na upana wa dhiraa nne.[#36:15 Dhiraa 30 ni sawa na mita 13.5.]

16Wakaunganisha mapazia matano kuwa fungu moja, na hayo mengine sita kuwa fungu lingine.

17Kisha wakatengeneza vitanzi hamsini kwenye upindo wa pazia la mwisho la fungu moja, na vivyo hivyo kwenye upindo wa pazia la mwisho la fungu hilo lingine.

18Wakatengeneza vifungo hamsini vya shaba ili kukaza hema pamoja kuwa kitu kimoja.

19Kisha wakatengeneza kifuniko cha hema kwa ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, na juu yake kifuniko cha ngozi za pomboo.[#36:19 pengine ni mnyama mwenye ngozi laini aishiye kwenye milima yenye misitu, au pengine nguva au sili]

20Wakatengeneza mihimili ya kusimamisha ya mti wa mshita kwa ajili ya maskani ya Mungu.

21Kila mhimili ulikuwa na urefu wa dhiraa kumi, na upana wa dhiraa moja na nusu,[#36:21 Dhiraa 10 ni sawa na mita 4.5.; #36:21 Dhiraa moja na nusu ni sawa na sentimita 67.5.]

22zikiwa na ndimi mbili zilizokuwa sambamba kila mmoja na mwingine. Wakatengeneza mihimili yote ya Maskani jinsi hii.

23Wakatengeneza mihimili ishirini kwa ajili ya upande wa kusini wa Maskani,

24na wakatengeneza vitako arobaini vya fedha vya kuweka chini ya hiyo mihimili, vitako viwili kwa kila mhimili, kimoja chini ya kila ulimi.

25Kwa upande wa kaskazini wa Maskani wakatengeneza mihimili ishirini

26na vitako arobaini vya fedha, viwili chini ya kila mhimili.

27Wakatengeneza mihimili sita kwa mwisho ulio mbali, yaani upande wa magharibi wa Maskani,

28na mihimili miwili ikatengenezwa kwa ajili ya pembe za Maskani za upande uliokuwa mbali.

29Katika pembe hizi mbili mihimili yake ilikuwa miwili kuanzia chini hadi juu, na ikaingizwa kwenye pete moja; mihimili ya pembe hizi mbili ilifanana.

30Kwa hiyo kulikuwa na mihimili nane, na vitako kumi na sita vya fedha, viwili chini ya kila mhimili.

31Wakatengeneza pia mataruma kwa mti wa mshita: matano kwa ajili ya mihimili ya upande mmoja wa Maskani,

32matano kwa ajili ya mihimili ya upande mwingine, na matano kwa ajili mihimili ya upande wa magharibi, mwisho kabisa mwa Maskani.

33Wakatengeneza taruma la katikati, likapenya katikati ya mihimili kutoka mwisho mmoja hadi mwisho mwingine.

34Wakaifunika hiyo mihimili kwa dhahabu, na wakatengeneza pete za dhahabu za kushikilia hayo mataruma. Pia wakayafunika hayo mataruma kwa dhahabu.

35Wakatengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa vizuri, naye fundi stadi akatirizi makerubi kwenye hilo pazia.

36Wakatengeneza nguzo nne za mti wa mshita kwa ajili yake na kuzifunika kwa dhahabu. Wakatengeneza kulabu za dhahabu kwa ajili ya nguzo hizo, na kusubu vitako vinne vya fedha.

37Kwa ajili ya ingilio la hema wakatengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa vizuri, kazi ya mtarizi.

38Pia wakatengeneza nguzo tano zenye kulabu. Wakafunika ncha za juu za hizo nguzo pamoja na tepe zake kwa dhahabu, na pia wakatengeneza vitako vyake vitano vya shaba.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.