The chat will start when you send the first message.
1Bezaleli akatengeneza Sanduku la mbao za mshita: urefu wake ulikuwa dhiraa mbili na nusu, upana wake dhiraa moja na nusu, na kimo chake dhiraa moja na nusu.[#37:1 Dhiraa moja na nusu ni sawa na mita 1.13.]
2Akalifunika kwa dhahabu safi ndani na nje, na kulizungushia ukingo wa dhahabu.
3Akasubu pete nne za dhahabu na kuzifungia kwenye miguu yake minne, pete mbili kwa upande mmoja na pete mbili kwa upande mwingine.
4Kisha akatengeneza mipiko ya mti wa mshita na kuzifunika kwa dhahabu.
5Akaiingiza hiyo mipiko kwenye zile pete katika pande mbili za Sanduku ili kulibeba.
6Akatengeneza kifuniko cha upatanisho kwa dhahabu safi: urefu wake ulikuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu.
7Kisha akatengeneza makerubi wawili wa dhahabu iliyofuliwa katika miisho ya hicho kifuniko.
8Akatengeneza kerubi mmoja kwenye mwisho mmoja, na kerubi mwingine kwenye mwisho mwingine; akawatengeneza kuwa kitu kimoja na hicho kifuniko katika miisho hiyo miwili.
9Makerubi hao walikuwa wametandaza mabawa kuelekea juu, wakitia kivuli hicho kifuniko. Makerubi hao walielekeana, wakitazama hicho kifuniko.
10Akatengeneza meza ya mbao za mshita yenye urefu wa dhiraa mbili, upana wa dhiraa moja, na kimo cha dhiraa moja na nusu.[#37:10 Dhiraa 2 ni sawa na sentimita 90.; #37:10 Dhiraa moja ni sawa na sentimita 45.]
11Kisha akaifunika kwa dhahabu safi, na kuitengenezea ukingo wa dhahabu kuizunguka pande zote.
12Pia akatengeneza upapi wenye upana wa nyanda moja, na kuufanyia ule upapi ukingo wa dhahabu kuuzunguka pande zote.[#37:12 Nyanda moja ni sawa na sentimita 7.5]
13Akasubu pete nne za dhahabu kwa ajili ya meza hiyo, na kuzifungia kwenye pembe nne, pale penye miguu yake minne.
14Pete hizo ziliwekwa karibu na ukingo ule ili kuishikilia ile mipiko iliyotumika kuibebea hiyo meza.
15Mipiko hiyo ya kubebea meza ilitengenezwa kwa mti wa mshita, na ilikuwa imefunikwa kwa dhahabu.
16Vyombo vyote vya mezani vilitengenezwa kwa dhahabu safi: yaani sahani zake, masinia, na bakuli na bilauri zake kwa ajili ya kumiminia sadaka za vinywaji.
17Akatengeneza kinara cha taa cha dhahabu safi iliyofuliwa vizuri katika kitako chake na ufito wake; vikombe vyake vilivyofanana na ua, matovu na maua vilikuwa kitu kimoja.
18Matawi sita yalitokeza kuanzia ule ufito wa katikati wa kinara cha taa: matawi matatu upande mmoja na matatu upande mwingine.
19Vikombe vitatu vya mfano wa maua ya mlozi yenye matovu na maua vilikuwa katika tawi moja, vikombe vitatu katika tawi jingine, na vivyo hivyo kwa matawi yote sita yaliyotokeza kwenye kile kinara cha taa.
20Juu ya kinara chenyewe kulikuwa vikombe vinne vya mfano wa maua ya mlozi yakiwa na matovu yake na maua yake.
21Tovu moja lilikuwa chini ya jozi ya kwanza ya matawi yaliyotokeza kwenye kinara cha taa, tovu la pili chini ya jozi ya pili, nalo tovu la tatu chini ya jozi ya tatu, yaani matawi sita kwa jumla.
22Matovu na matawi yote yalikuwa kitu kimoja na kile kinara cha taa, yakiwa yamefuliwa kwa dhahabu safi.
23Akatengeneza taa zake saba, na pia mikasi ya kusawazishia tambi, pamoja na masinia, zote kwa dhahabu safi.
24Akatengeneza kinara hicho cha taa pamoja na vifaa vyake vyote kutumia talanta moja ya dhahabu safi.[#37:24 Talanta moja ya dhahabu ni sawa na kilo 34.]
25Akatengeneza madhabahu ya kufukizia uvumba kwa mbao za mshita. Ilikuwa ya mraba, urefu na upana wake dhiraa moja, na kimo cha dhiraa mbili, nazo pembe zake zilikuwa kitu kimoja nayo.
26Akafunika hayo madhabahu juu na pande zote na pia zile pembe zake kwa dhahabu safi, na akayafanyizia ukingo wa dhahabu kuizunguka.
27Akatengeneza pete mbili za dhahabu kwa ajili ya madhabahu chini ya huo ukingo, zikiwa mbili kila upande, za kushikilia mipiko iliyotumika kubebea madhabahu.
28Akatengeneza mipiko kwa miti ya mshita na kuifunika kwa dhahabu.
29Pia akatengeneza mafuta matakatifu ya upako, na uvumba safi wenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato.