Ezekieli 32

Ezekieli 32

1Katika mwaka wa kumi na mbili, mwezi wa kumi na mbili, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema:

2“Mwanadamu, fanya maombolezo kwa ajili ya Farao mfalme wa Misri na umwambie:

“ ‘Wewe ni kama simba miongoni mwa mataifa,

wewe ni kama mnyama mkubwa baharini,

unapiga maji kwa kishindo katika vijito vyako,

unayavuruga maji kwa miguu yako,

na kuchafua vijito.

3“ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:

“ ‘Nikiwa pamoja na wingi mkubwa wa watu

nitautupa wavu wangu juu yako,

nao watakukokota katika wavu wangu.

4Nitakutupa nchi kavu

na kukuvurumisha uwanjani.

Nitawafanya ndege wote wa angani watue juu yako

na wanyama wote wa nchi

watajishibisha nyama yako.

5Nitatawanya nyama yako juu ya milima

na kujaza mabonde kwa mabaki yako.

6Nitailowanisha nchi kwa damu yako inayotiririka

njia yote hadi milimani,

nayo mabonde yatajazwa na nyama yako.

7Nitakapokuzimisha, nitafunika mbingu

na kuzitia nyota zake giza;

nitalifunika jua kwa wingu,

nao mwezi hautatoa nuru yake.

8Mianga yote itoayo nuru angani

nitaitia giza juu yako;

nitaleta giza juu ya nchi yako,

asema Bwana Mwenyezi.

9Nitaifadhaisha mioyo ya mataifa mengi

nitakapokuangamiza miongoni mwa mataifa,

nikikuleta uhamishoni miongoni mwa nchi

ambazo hujapata kuzijua.

10Nitayafanya mataifa mengi wakustaajabie,

wafalme wao watatetemeka

kwa hofu kwa ajili yako

nitakapotikisa upanga wangu mbele yao.

Siku ya anguko lako

kila mmoja wao atatetemeka

kila dakika kwa ajili ya maisha yake.

11“ ‘Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:

“ ‘Upanga wa mfalme wa Babeli

utakuja dhidi yako.

12Nitayafanya makundi yako kuanguka

kwa panga za mashujaa:

taifa katili kuliko mataifa yote.

Watakivunjavunja kiburi cha Misri,

nayo makundi yake yote yatashindwa.

13Nitaangamiza mifugo yake yote

wanaojilisha kando ya maji mengi:

hayatavurugwa tena kwa mguu wa mwanadamu

wala kwato za mnyama

hazitayachafua tena.

14Kisha nitafanya maji yake yatulie

na kufanya vijito vyake

vitiririke kama mafuta,

asema Bwana Mwenyezi.

15Nitakapoifanya Misri kuwa ukiwa,

na kuiondolea nchi kila kitu kilichomo,

nitakapowapiga wote wanaoishi humo,

ndipo watajua kuwa

Mimi ndimi Bwana .’

16“Hili ndilo ombolezo watakalomwimbia. Binti za mataifa wataliimba, kwa kuwa Misri na makundi yake yote wataliimba, asema Bwana Mwenyezi.”

17Katika mwaka wa kumi na mbili, mwezi wa kwanza, siku ya kumi na tano ya mwezi, neno la Bwana likanijia kusema:

18“Mwanadamu, omboleza kwa ajili ya makundi ya Misri na uwatupe Kuzimu, yeye na binti za mataifa yenye nguvu, waende huko pamoja nao wanaoshuka shimoni.

19Je, ninyi mmekubalika zaidi ya wengine? Shukeni chini! Nanyi mkalazwe pamoja na hao wasiotahiriwa!

20Wataanguka miongoni mwa wale waliouawa kwa upanga. Upanga umefutwa; mwache aburutwe mbali pamoja na hao watu wake wote.

21Kutoka Kuzimu viongozi hodari watanena kuhusu Misri pamoja na wale walioungana nao, ‘Wameshuka chini, nao wamelala kimya pamoja na hao wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga.’

22“Ashuru yuko huko pamoja na jeshi lake lote, amezungukwa na makaburi ya watu wake wote waliouawa, wale wote walioanguka kwa upanga.

23Makaburi yao yako kwenye kina cha chini cha shimo na jeshi lake limelala kulizunguka kaburi lake. Wote waliokuwa wameeneza hofu kuu katika nchi ya walio hai wameuawa, wameanguka kwa upanga.

24“Elamu yuko huko, pamoja na makundi yake yote wakiwa wamelizunguka kaburi lake. Wote wameuawa, wameanguka kwa upanga. Wote waliokuwa wameeneza hofu katika nchi ya walio hai walishuka Kuzimu bila kutahiriwa. Wanaichukua aibu yao pamoja na wale wanaoshuka shimoni.

25Kitanda kimetandikwa kwa ajili yake miongoni mwa waliouawa, pamoja na makundi yake yote wakiwa wamelizunguka kaburi lake. Wote ni watu wasiotahiriwa, wameuawa kwa upanga. Kwa sababu vitisho vyao vilienea katika nchi ya walio hai, wameichukua aibu yao pamoja na wale wanaoshuka shimoni, nao wamewekwa miongoni mwa waliouawa.

26“Mesheki na Tubali wako humo, pamoja na makundi yao wakiwa wameyazunguka makaburi yao. Wote hawakutahiriwa, wameuawa kwa upanga kwa sababu walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai.

27Je, hawakulala na mashujaa wengine wasiotahiriwa waliouawa, ambao wameshuka kaburini wakiwa na silaha zao za vita, ambao panga zao ziliwekwa chini ya vichwa vyao na uovu wao juu ya mifupa yao? Adhabu kwa ajili ya dhambi zao ilikuwa juu ya mifupa yao, ingawa vitisho vya mashujaa hawa vilikuwa vimeenea hadi kwenye nchi ya walio hai.[#32:27 Kaburini maana yake ni Kuzimu ; kwa Kiebrania ni Sheol.]

28“Wewe pia, ee Farao, utavunjwa nawe utalala miongoni mwa wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga.

29“Edomu yuko humo, wafalme wake wote na wakuu wake wote, ambao ijapokuwa wana nguvu, wamelazwa pamoja na wale waliouawa kwa upanga. Wamelala pamoja na wasiotahiriwa, pamoja na wale wanaoshuka shimoni.

30“Wakuu wote wa kaskazini na Wasidoni wote wako huko, wameshuka chini pamoja na waliouawa kwa aibu ijapokuwa kuna vitisho vilivyosababishwa na nguvu zao. Wamelala bila kutahiriwa pamoja na wale waliouawa kwa upanga na kuchukua aibu yao pamoja na wale wanaoshuka shimoni.

31“Farao, yeye pamoja na jeshi lake lote, atakapowaona atafarijiwa kwa ajili ya makundi yake yote, wale waliouawa kwa upanga, asema Bwana Mwenyezi.

32Ingawa nilimfanya Farao aeneze vitisho vyake katika nchi ya walio hai, Farao pamoja na makundi yake yote watalazwa miongoni mwa wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga, asema Bwana Mwenyezi.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.