The chat will start when you send the first message.
1Kristo alitupatia uhuru, akataka tubaki huru. Hivyo simameni imara wala msikubali tena kulemewa na nira ya utumwa.
2Sikilizeni! Mimi, Paulo, nawaambieni kwamba mkikubali kutahiriwa, basi Kristo hatakuwa na thamani kwenu hata kidogo.
3Namshuhudia tena kila mtu anayekubali kutahiriwa kwamba inampasa kushika sheria yote.
4Ninyi mnaotafuta kuhesabiwa haki kupitia kwa sheria mmetengwa na Kristo, mko mbali na neema ya Mungu.
5Kwa maana, kupitia Roho tunangojea kwa shauku tumaini la haki kwa imani.
6Kwa maana ndani ya Kristo Yesu, kutahiriwa au kutokutahiriwa hakuleti tofauti, bali lililo muhimu ni imani itendayo kazi kupitia kwa upendo.
7Mlikuwa mkipiga mbio vizuri. Ni nani aliyewazuia msiitii kweli?
8Ushawishi kama huo haukutoka kwa yule anayewaita.
9“Chachu kidogo huchachua donge zima.”
10Nina hakika katika Bwana kwamba hamtakuwa na msimamo mwingine. Mtu anayewachanganya anastahili adhabu, hata awe nani.
11Lakini ndugu zangu, kama mimi bado ninahubiri kuhusu kutahiriwa, kwa nini bado ninateswa? Katika hiyo hali basi, kwazo la msalaba limeondolewa.
12Laiti hao wanaowavuruga wangejihasi wao wenyewe!
13Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili mwe huru, hivyo msitumie uhuru wenu kama fursa ya kufuata tamaa za mwili, bali tumikianeni ninyi kwa ninyi kwa upendo.
14Kwa maana sheria yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.”[#5:14 Law 19:18]
15Lakini mkiumana na kutafunana, angalieni msije mkaangamizana.
16Kwa hiyo nasema, nendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.
17Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, naye Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka.
18Lakini mkiongozwa na Roho, hamko chini ya sheria.
19Basi matendo ya mwili ni dhahiri, nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi,
20kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,
21husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi ufalme wa Mungu.
22Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,
23upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria.
24Wote walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake.
25Kwa kuwa tunaishi kwa Roho, basi, tuenende kwa Roho.
26Tusijisifu bure, tukichokozana na kuoneana wivu.