Mwanzo 28

Mwanzo 28

Yakobo akimbilia kwa Labani

1Basi Isaka akamwita Yakobo, akambariki na akamwamuru, akisema, “Usioe mwanamke Mkanaani.

2Nenda mara moja hadi Padan-Aramu, kwenye nyumba ya Bethueli, baba wa mama yako. Uchukue mke kati ya binti za Labani ambaye ni ndugu wa mama yako.

3Mungu Mwenyezi na akubariki, uwe na uzao, uongezeke idadi yako hadi upate kuwa jamii kubwa ya watu.[#28:3 Kiebrania El-Shaddai (yaani Mungu Mwenye utoshelevu wote).]

4Akupe wewe na uzao wako baraka aliyopewa Abrahamu, upate kumiliki nchi unayoishi sasa kama mgeni, nchi ambayo Mungu alimpa Abrahamu.”

5Kisha Isaka akamuaga Yakobo, naye akaenda Padan-Aramu, kwa Labani mwana wa Bethueli Mwaramu, ndugu wa Rebeka, mama yao Yakobo na Esau.[#28:5 au Mshami]

6Basi Esau akajua kuwa Isaka amembariki Yakobo na kumtuma Padan-Aramu ili achukue mke huko, na kwamba alipombariki alimwamuru, akisema, “Usioe mke katika binti za Wakanaani,”

7tena kwamba Yakobo amewatii baba yake na mama yake, naye ameenda Padan-Aramu.

8Esau akatambua jinsi baba yake Isaka alivyowachukia binti za Wakanaani.

9Ndipo Esau akaenda kwa Ishmaeli, akamwoa Mahalati, ndugu wa Nebayothi na binti ya Ishmaeli mwana wa Abrahamu, kuongezea wale wake wengine aliokuwa nao.

Ndoto ya Yakobo huko Betheli

10Yakobo akatoka Beer-Sheba kwenda Harani.

11Alipofika mahali fulani, akalala hapo kwa sababu jua lilikuwa limetua. Akachukua jiwe moja la mahali pale, akaliweka chini ya kichwa chake, akajinyoosha na akalala usingizi.

12Akaota ndoto, na katika ndoto hiyo aliona ngazi imesimamishwa juu ya ardhi, ncha yake ikiwa imefika mbinguni. Nao malaika wa Mungu walikuwa wakipanda na kushuka kwa ngazi hiyo.

13Juu yake alisimama Bwana , akasema, “Mimi ni Bwana , Mungu wa baba yako Abrahamu, na Mungu wa Isaka. Nchi ambayo umelala juu yake, nitakupa wewe na uzao wako.

14Uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi na mashariki, kaskazini na kusini. Kupitia wewe na uzao wako, mataifa yote ya duniani yatabarikiwa.

15Niko pamoja nawe, nami nitakulinda popote utakapoenda, na nitakurudisha katika nchi hii. Sitakuacha hadi nitakapofanya hayo niliyokuahidi.”

16Yakobo alipoamka kutoka usingizi, akawaza, “Hakika Bwana yuko mahali hapa, wala mimi sikujua.”

17Kwa hiyo akaogopa, akasema, “Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka hapa ndipo nyumba ya Mungu ilipo; hili ni lango la mbinguni.”

18Kesho yake asubuhi na mapema, Yakobo akalichukua lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake, akalisimamisha kama nguzo, na kumimina mafuta juu yake.

19Mahali pale akapaita Betheli, ingawa mji ule hapo awali uliitwa Luzu.[#28:19 maana yake Nyumba ya Mungu]

20Kisha Yakobo akaweka nadhiri, akisema, “Mungu akiwa pamoja nami na kunilinda katika safari hii, akinipa chakula nile na nguo nivae,

21na nirudi salama nyumbani mwa baba yangu, hapo ndipo Bwana atakuwa Mungu wangu.

22Nalo jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu, na katika yote utakayonipa nitakutolea sehemu ya kumi.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.