Mwanzo 32

Mwanzo 32

Yakobo ajiandaa kukutana na Esau

1Yakobo pia akaondoka akaenda zake, nao malaika wa Mungu wakakutana naye.

2Yakobo alipowaona, akasema, “Hii ni kambi ya Mungu!” Kwa hiyo akapaita mahali pale Mahanaimu.[#32:2 maana yake Kambi mbili]

3Yakobo akatuma wajumbe kumtangulia kwa Esau ndugu yake huko Seiri, katika nchi ya Edomu.

4Akawaagiza, akisema: “Hili ndilo mtakalomwambia bwana wangu Esau: ‘Mtumishi wako Yakobo anasema: nimekuwa nikiishi pamoja na Labani na nimekuwa huko hadi sasa.

5Ninao ngʼombe na punda, kondoo na mbuzi, watumishi wa kiume na wa kike. Sasa ninatuma ujumbe huu kwa bwana wangu, ili nipate kibali machoni pako.’ ”

6Wajumbe waliporudi kwa Yakobo, wakamwambia, “Tulienda kuonana na ndugu yako Esau, naye sasa anakuja kukulaki akifuatana na wanaume mia nne.”

7Kwa hofu kuu na huzuni, Yakobo akagawanya watu aliokuwa nao katika makundi mawili; pia akagawanya makundi ya kondoo na mbuzi, na vilevile ngʼombe na ngamia.

8Yakobo alifikiri, “Kama Esau akija na kushambulia kundi moja, kundi lililobaki litanusurika.”

9Ndipo Yakobo akaomba, “Ee Mungu wa baba yangu Abrahamu, Mungu wa baba yangu Isaka, Ee Bwana , ndiwe uliniambia, ‘Rudi katika nchi yako na jamaa yako, nami nitakufanya ustawi.’

10Sistahili fadhili na uaminifu wako wote ulionitendea mimi, mtumishi wako. Nilikuwa na fimbo tu mkononi mwangu nilipovuka mto huu wa Yordani, lakini sasa nimekuwa makundi mawili.

11Nakuomba uniokoe kutoka kwa mkono wa ndugu yangu Esau, kwa maana ninaogopa kuwa atakuja kunishambulia, pia kina mama pamoja na watoto wao.

12Lakini umeshasema, ‘Hakika nitakufanya ustawi na kuufanya uzao wako kuwa mwingi kama mchanga wa baharini ambao hauwezi kuhesabika!’ ”

13Akalala pale usiku ule. Miongoni mwa vitu alivyokuwa navyo, akachagua zawadi kwa ajili ya Esau ndugu yake:

14beberu ishirini na mbuzi jike mia mbili, kondoo dume ishirini na kondoo jike mia mbili,

15ngamia jike thelathini pamoja na ndama zao, ngʼombe arobaini na mafahali kumi, punda jike ishirini, na punda wa kiume kumi.

16Akaviweka chini ya uangalizi wa watumishi wake, kila kundi peke yake, na kuwaambia, “Nitangulieni na kuacha nafasi kati ya makundi.”

17Akamwagiza yule aliyetangulia hivi, “Ndugu yangu Esau atakapokutana nawe na kukuuliza, ‘Wewe ni wa nani? Unaenda wapi? Wanyama hawa wote mbele yako ni mali ya nani?’

18utamjibu hivi, ‘Ni mali ya mtumishi wako Yakobo. Ni zawadi iliyotumwa kwa bwana wangu Esau, naye anakuja nyuma yetu.’ ”

19Akamwagiza pia yule mtumishi wa kundi la pili, na wa kundi la tatu, na kila mtumishi wa yale mengine yaliyofuata, hivi: “Mtamwambia Esau maneno hayo hayo mtakapokutana naye.

20Hakikisheni mmesema, ‘Mtumishi wako Yakobo anakuja nyuma yetu.’ ” Kwa kuwa alifikiri, “Nitaweza kumtuliza kwa zawadi hizi ninazotanguliza; hatimaye nitakapomwona, huenda atanikubali.”

21Kwa hiyo zawadi za Yakobo zilitangulia mbele yake, lakini yeye mwenyewe alilala kambini usiku ule.

Yakobo amenyana na Mungu

22Usiku ule Yakobo akaamka, akawachukua wake zake wawili, wajakazi wake wawili, na wanawe kumi na mmoja, akavuka kivuko cha Mto Yaboki.

23Baada ya kuwavusha ngʼambo ya kijito, alivusha pia mali yake yote.

24Kwa hiyo Yakobo akaachwa peke yake; naye mtu mmoja akashikana naye mweleka hadi mapambazuko.

25Yule mtu alipoona kuwa hawezi kumshinda, aligusa kiungio cha nyonga ya Yakobo; kwa hiyo nyonga yake ikateguka alipokuwa akishikana mweleka na yule mtu.

26Ndipo yule mtu akasema, “Niache niende, kwa kuwa ni mapambazuko.”

Lakini Yakobo akajibu, “Sitakuacha uende usiponibariki.”

27Yule mtu akamuuliza, “Jina lako ni nani?”

Akamjibu, “Ni Yakobo.”

28Ndipo yule mtu akasema, “Jina lako halitakuwa tena Yakobo, bali Israeli, kwa sababu umeshindana na Mungu na watu pia, nawe umeshinda.”[#32:28 maana yake Yeye ashindanaye na Mungu]

29Yakobo akasema, “Tafadhali niambie jina lako.”

Lakini akajibu, “Kwa nini kuniuliza Jina langu?” Ndipo akambariki huko.

30Kwa hiyo Yakobo akapaita mahali pale Penieli, akisema, “Ni kwa sababu nimemwona Mungu uso kwa uso, na bado uhai wangu umehifadhiwa.”[#32:30 maana yake Uso wa Mungu ; sawa na Penueli kwa Kiebrania]

31Jua lilikuwa linachomoza Yakobo alipoondoka Penueli, naye alikuwa akichechemea kwa sababu ya nyonga yake.

32Kwa hiyo hadi leo Waisraeli hawali mshipa ulioungana na kiungio cha nyonga, kwa sababu kiungio cha nyonga ya Yakobo kiliteguliwa karibu na mshipa huo.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.