The chat will start when you send the first message.
1Adamu akakutana kimwili na mkewe Hawa, naye akapata mimba, akamzaa Kaini. Hawa akasema, “Kwa msaada wa Bwana nimemzaa mtoto wa kiume.”
2Baadaye akamzaa Abeli ndugu yake.
Basi Abeli akawa mfugaji, na Kaini akawa mkulima.
3Baada ya muda, Kaini akaleta baadhi ya mazao ya shamba ikiwa sadaka kwa Bwana .
4Lakini Abeli akaleta fungu nono kutoka baadhi ya wazaliwa wa kwanza wa mifugo yake. Bwana akamkubali Abeli pamoja na sadaka yake,
5lakini Mungu hakumkubali Kaini pamoja na sadaka yake. Kwa hiyo Kaini akakasirika sana, uso wake ukawa na huzuni.
6Kisha Bwana akamwambia Kaini, “Kwa nini umekasirika? Kwa nini uso wako una huzuni?
7Ukifanya lililo sawa, je, hutakubalika? Lakini usipofanya lililo sawa, dhambi inakuvizia mlangoni mwako, ikikutamani wewe, lakini inakupasa uishinde.”
8Basi Kaini akamwambia ndugu yake Abeli, “Twende shambani.” Walipokuwa shambani, Kaini akamshambulia Abeli ndugu yake, akamuua.
9Kisha Bwana akamuuliza Kaini, “Ndugu yako Abeli yuko wapi?”
Akamjibu, “Sijui. Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?”
10Bwana akasema, “Umefanya nini? Sikiliza! Damu ya ndugu yako inanililia mimi kutoka ardhini.
11Sasa umelaaniwa na umehamishwa kutoka ardhi, ambayo imefungua kinywa chake na kupokea damu ya ndugu yako kutoka mkononi mwako.
12Utakapoilima ardhi, haitakupa tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga duniani bila utulivu.”
13Kaini akamwambia Bwana , “Adhabu yangu ni zaidi ya ninavyoweza kustahimili.
14Leo unanifukuza kutoka nchi, nami nitafichwa mbali na uwepo wako. Nitakuwa mtu wa kutangatanga duniani bila utulivu, na yeyote anionaye ataniua.”
15Lakini Bwana akamwambia, “La, sivyo! Ikiwa mtu yeyote atamuua Kaini, atalipizwa kisasi mara saba.” Kisha Bwana akamwekea Kaini alama ili yeyote angemwona asimuue.
16Kwa hiyo Kaini akaondoka mbele za Bwana , akaenda kuishi katika nchi ya Nodi, mashariki mwa Edeni.
17Kaini akakutana kimwili na mkewe, naye akapata mimba na akamzaa Henoko. Wakati huo Kaini alikuwa anajenga mji, akauita Henoko, jina la mtoto wake.
18Henoko akamzaa Iradi; Iradi akamzaa Mehuyaeli; Mehuyaeli akamzaa Methushaeli; naye Methushaeli akamzaa Lameki.
19Lameki alioa wanawake wawili: mmoja aliitwa Ada, na mwingine Sila.
20Ada akamzaa Yabali; huyu akawa baba wa wale wanaoishi katika mahema na kufuga wanyama.
21Kaka yake aliitwa Yubali, aliyekuwa baba wa wote wapigao zeze na filimbi.
22Pia Sila alikuwa na mtoto wa kiume aliyeitwa Tubali-Kaini, ambaye alifua vifaa vya aina mbalimbali vya shaba na chuma. Naama alikuwa dada wa Tubali-Kaini.
23Lameki akawaambia wake zake,
“Ada na Sila, nisikilizeni mimi;
wake wa Lameki sikieni maneno yangu.
Nimemuua mtu kwa kunijeruhi,
kijana mdogo kwa kuniumiza.
24Kama Kaini atalipizwa kisasi mara saba,
basi Lameki itakuwa mara sabini na saba.”
25Adamu akakutana kimwili na mke wake tena, akamzaa mwana, akamwita jina Sethi, akisema, “Mungu amenijalia mwana mwingine badala ya Abeli, kwa kuwa Kaini alimuua.”
26Naye Sethi akamzaa mwana, akamwita jina Enoshi.
Wakati huo watu wakaanza kuliitia jina la Bwana .