The chat will start when you send the first message.
1Neno la unabii alilopokea nabii Habakuki.
2Ee Bwana , hata lini nitakuomba msaada,
lakini wewe husikilizi?
Au kukulilia, “Udhalimu!”
lakini hutaki kuokoa?
3Kwa nini unanifanya nitazame dhuluma?
Kwa nini unavumilia makosa?
Uharibifu na udhalimu viko mbele yangu;
kuna mabishano na mapambano kwa wingi.
4Kwa hiyo sheria imepotoshwa,
nayo haki haipo kabisa.
Waovu wanawazunguka wenye haki,
kwa hiyo haki imepotoshwa.
5“Yatazame mataifa,
uangalie na ushangae kabisa.
Kwa sababu katika siku zako nitafanya kitu
ambacho hungeamini,
hata kama ungeambiwa.
6Tazama! Nitawainua Wakaldayo,
watu wakatili na wenye haraka,
ambao hupita dunia yote
ili kuteka makazi yasiyo yao.
7Ni watu wanoogopwa na wanaotisha;
wenyewe ndio sheria yao,
na huinua heshima yao wenyewe.
8Farasi wao ni wepesi kuliko chui,
na wakali kuliko mbwa-mwitu wakati wa machweo.
Askari wapanda farasi wao huenda mbio;
waendesha farasi wao wanatoka mbali.
Wanaruka kasi kama tai
ili kurarua mawindo;
9wote wanakuja tayari kutenda udhalimu.
Makundi yao wanasonga mbele
kama upepo wa jangwani,
na kukusanya wafungwa
kama mchanga.
10Wanawabeza wafalme,
na kuwadhihaki watawala.
Wanaicheka miji yote yenye ngome;
wanalundika udongo na kuiteka hiyo miji.
11Kisha wanapita kasi kama upepo na kusonga mbele:
watu wenye hatia, ambao nguvu zao ndio mungu wao.”
12Ee Bwana , je, wewe sio wa tangu milele?
Mungu wangu, Uliye Mtakatifu wangu, hatutakufa.
Ee Bwana , umewachagua wao ili watekeleze hukumu;
Ee Mwamba, umewaamuru watuadhibu.
13Macho yako ni safi mno hata yasiweze kuutazama uovu,
wala huwezi kuvumilia makosa.
Kwa nini basi unawavumilia wadanganyifu?
Kwa nini unakuwa kimya wakati waovu
wanawameza wale wenye haki
kuliko wao wenyewe?
14Umewafanya watu kama samaki baharini,
kama viumbe wa bahari wasio na mtawala.
15Adui mwovu anawavuta wote kwa ndoana,
anawakamata katika wavu wake,
anawakusanya katika juya lake;
kwa hiyo anashangilia na anafurahi.
16Kwa hiyo anatoa sadaka kwa wavu wake,
na kuchoma uvumba kwa juya lake,
kwa kuwa kwa wavu wake anaishi kwa starehe,
na anafurahia chakula kizuri.
17Je, aendelee kuwatoa walio katika wavu wake,
akiangamiza mataifa bila huruma?