The chat will start when you send the first message.
1Bwana atamhurumia Yakobo,
atamchagua Israeli tena,
na kuwakalisha katika nchi yao wenyewe.
Wageni wataungana nao
na kujiunga na nyumba ya Yakobo.
2Mataifa watawachukua
na kuwaleta mahali pao wenyewe.
Nayo nyumba ya Israeli itamiliki mataifa
kama watumishi na wajakazi katika nchi ya Bwana .
Watawafanya watekaji wao kuwa mateka,
na kuwatawala waliowadhulumu.
3Katika siku Bwana atakapokuondolea mateso, udhia na utumwa wa kikatili,
4utaichukua dhihaka hii dhidi ya mfalme wa Babeli:
Tazama jinsi mtesi alivyofikia mwisho!
Tazama jinsi ghadhabu yake kali ilivyokoma!
5Bwana amevunja fimbo ya mwovu,
fimbo ya utawala ya watawala,
6ambayo kwa hasira waliyapiga mataifa
kwa mapigo yasiyo na kikomo,
nao kwa ghadhabu kali waliwatiisha mataifa
kwa jeuri pasipo huruma.
7Nchi zote ziko kwenye mapumziko na kwenye amani,
wanabubujika kwa kuimba.
8Hata misunobari na mierezi ya Lebanoni
inashangilia mbele yako na kusema,
“Basi kwa kuwa umeangushwa chini,
hakuna mkata miti atakayekuja kutukata.”
9Kuzimu kumetaharuki[#14:9 Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol , yaani Shimo lisilo na mwisho.]
kukulaki unapokuja,
kunaamsha roho za waliokufa ili kukupokea,
wote waliokuwa viongozi katika ulimwengu,
kunawafanya wainuke kwenye viti vyao vya kifalme:
wale wote waliokuwa wafalme juu ya mataifa.
10Wote wataitikia,
watakuambia,
“Wewe pia umekuwa dhaifu, kama sisi tulivyo;
wewe umekuwa kama sisi.”
11Majivuno yako yote yameshushwa hadi Kuzimu,
pamoja na kelele ya vinubi vyako,
mafunza yametanda chini yako,
na minyoo imekufunika.
12Tazama jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni,
ewe nyota ya asubuhi, mwana wa mapambazuko!
Umetupwa chini duniani,
wewe uliyepata kuangusha mataifa!
13Ulisema moyoni mwako,
“Nitapanda juu hadi mbinguni,
nitakiinua kiti changu cha utawala
juu ya nyota za Mungu;
nitaketi nimetawazwa juu ya mlima wa kusanyiko,
kwenye vimo vya juu sana vya Mlima Mtakatifu.
14Nitapaa juu kupita mawingu,
nitajifanya kama Yeye Aliye Juu Sana.”
15Lakini umeshushwa chini hadi Kuzimu,
hadi kwenye vina vya shimo.
16Wale wanaokuona wanakukazia macho,
wanatafakari hatima yako:
“Je, huyu ndiye yule aliyetikisa dunia
na kufanya falme zitetemeke,
17yule aliyeifanya dunia kuwa jangwa,
aliyeipindua miji yake,
na ambaye hakuwaachia mateka wake
waende nyumbani?”
18Wafalme wote wa mataifa wamelala kwa heshima
kila mmoja katika kaburi lake.
19Lakini wewe umetupwa nje ya kaburi lako
kama tawi lililokataliwa,
umefunikwa na waliouawa
pamoja na wale waliochomwa kwa upanga,
wale wanaoshuka hadi
kwenye mawe ya shimo.
Kama mzoga uliokanyagwa chini ya nyayo,
20Hutajumuika nao kwenye mazishi,
kwa kuwa umeharibu nchi yako
na kuwaua watu wako.
Mzao wa mwovu
hatatajwa tena kamwe.
21Andaa mahali pa kuwachinjia wanawe
kwa ajili ya dhambi za baba zao,
wasije wakainuka ili kuirithi nchi
na kuijaza dunia kwa miji yao.
22Bwana wa majeshi asema,
“Nitainuka dhidi yao,
nitalikatilia mbali jina lake kutoka Babeli pamoja na watu wake walionusurika,
watoto wake na wazao wake,”
asema Bwana .
23“Nitaifanya kuwa mahali pa bundi,
na kuwa nchi ya matope;
nitaifagia kwa ufagio wa maangamizi,”
asema Bwana wa majeshi.
24Bwana wa majeshi ameapa,
“Hakika, kama vile nilivyopanga, ndivyo itakavyokuwa,
nami kama nilivyokusudia, ndivyo itakavyosimama.
25Nitamponda Mwashuru katika nchi yangu,
juu ya milima yangu nitawakanyagia chini.
Nira yake itaondolewa kutoka kwa watu wangu,
nao mzigo wake utaondolewa kutoka mabegani mwao.”
26Huu ndio mpango uliokusudiwa kwa ajili ya ulimwengu wote,
huu ni mkono ulionyooshwa juu ya mataifa yote.
27Kwa kuwa Bwana wa majeshi amekusudia,
ni nani awezaye kumzuia?
Mkono wake umenyooshwa,
ni nani awezaye kuurudisha?
28Neno hili lilikuja mwaka ule Mfalme Ahazi alipofariki:
29Msifurahi, enyi Wafilisti wote,
kwamba fimbo iliyowapiga imevunjika;
kutoka mzizi wa huyo nyoka
atachipuka nyoka mwenye sumu kali,
uzao wake utakuwa joka lirukalo,
lenye sumu kali.
30Maskini kuliko maskini wote watapata malisho,
nao wahitaji watalala salama.
Lakini mzizi wako nitauangamiza kwa njaa,
nayo njaa itawaua walionusurika.
31Piga yowe, ee lango! Bweka, ee mji!
Yeyukeni, enyi Wafilisti wote!
Wingu la moshi linakuja toka kaskazini,
wala hakuna atakayechelewa katika safu zake.
32Ni jibu gani litakalotolewa
kwa wajumbe wa taifa hilo?
“Bwana ameifanya imara Sayuni,
na ndani yake watu wake walioonewa watapata kimbilio.”