Isaya 21

Isaya 21

Unabii dhidi ya Babeli

1Neno la unabii kuhusu Jangwa kando ya Bahari:

Kama upepo wa kisulisuli unaopita katika nchi hadi kusini,

mshambuliaji anakuja kutoka jangwani,

kutoka nchi inayotisha.

2Nimeoneshwa maono ya kutisha:

Msaliti anasaliti, mteka nyara anateka nyara.

Elamu, shambulia! Umedi, zingira kwa jeshi!

Nitakomesha huzuni zote alizosababisha.

3Kwa sababu hii, mwili wangu umeteswa na maumivu,

maumivu makali ya ghafula yamenishika,

kama yale ya mwanamke mwenye uchungu wa kuzaa.

Nimeduwazwa na lile ninalolisikia,

nimeshangazwa na lile ninaloliona.

4Moyo wangu unababaika,

woga unanifanya nitetemeke,

gizagiza la jioni nililolitamani sana,

limekuwa hofu kuu kwangu.

5Wanaandaa meza,

wanatandaza mazulia,

wanakula, wanakunywa!

Amkeni, enyi maafisa,

zitieni ngao mafuta!

6Hili ndilo Bwana analoniambia:

“Nenda, weka mlinzi,

na atoe taarifa ya kile anachokiona.

7Anapoona magari ya vita

pamoja na kundi la farasi,

wapanda punda au wapanda ngamia,

na awe macho, awe macho kikamilifu.”

8Naye mlinzi alipaza sauti,

“Mchana baada ya mchana, bwana wangu,

ninasimama katika mnara wa ulinzi,

kila usiku ninakaa mahali pangu nilipoamriwa.

9Tazama, yuaja mtu anayepanda gari la vita

pamoja na kundi la farasi.

Naye anajibu:

‘Babeli umeanguka, umeanguka!

Vinyago vyote vya miungu yake

vimelala chini vikiwa vimevunjwa!’ ”

10Ee watu wangu, mliopondwa kwenye sakafu ya kupuria,

ninawaambia kile nilichokisikia

kutoka kwa Bwana wa majeshi,

kutoka kwa Mungu wa Israeli.

Unabii dhidi ya Edomu

11Neno la unabii kuhusu Duma:

Mtu fulani ananiita kutoka Seiri,

“Mlinzi, usiku utaisha lini?

Mlinzi, usiku utaisha lini?”

12Mlinzi anajibu,

“Asubuhi inakuja, lakini pia usiku.

Ukitaka kuuliza, basi uliza;

na urudi mara tena.”

Unabii dhidi ya Arabia

13Neno la unabii kuhusu Arabia:

Enyi misafara ya Wadedani,

mnaopiga kambi katika vichaka vya Arabia,

14leteni maji kwa wenye kiu,

ninyi mnaoishi Tema,

leteni chakula kwa ajili ya wakimbizi.

15Wanaukimbia upanga,

upanga uliochomolewa alani,

kutoka upinde uliopindwa,

na kutoka kwa joto la vita.

16Hili ndilo Bwana analoniambia: “Katika muda wa mwaka mmoja, kama vile mtumishi aliyefungwa na mkataba angeihesabu, majivuno yote ya Kedari yatafikia mwisho.

17Wanaume wavutao pinde walionusurika, mashujaa wa Kedari, watakuwa wachache.” Bwana , Mungu wa Israeli, amesema.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.