Isaya 61

Isaya 61

Mwaka wa upendeleo wa Bwana

1Roho wa Bwana Mwenyezi yu juu yangu,

kwa sababu Bwana amenipaka mafuta

kuwahubiria maskini habari njema.

Amenituma kuwafariji waliovunjika moyo,

kuwatangazia mateka uhuru wao,

na hao waliofungwa

habari za kufunguliwa kwao;

2kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,

na siku ya kisasi ya Mungu wetu,

kuwafariji wote wanaoomboleza,

3na kuwapa mahitaji

wale wanaohuzunika katika Sayuni,

ili kuwapa taji za uzuri badala ya majivu,

mafuta ya furaha badala ya maombolezo,

vazi la sifa badala ya roho ya kukata tamaa.

Nao wataitwa mialoni ya haki,

pando la Bwana ,

ili kuonesha utukufu wake.

4Watajenga upya magofu ya zamani

na kupatengeneza mahali palipoachwa ukiwa zamani;

watafanya upya miji iliyoharibiwa,

iliyoachwa ukiwa kwa vizazi vingi.

5Wageni watayachunga makundi yenu,

wageni watafanya kazi katika mashamba yenu,

na kutunza mashamba yenu ya mizabibu.

6Nanyi mtaitwa makuhani wa Bwana ,

mtaitwa watumishi wa Mungu wetu.

Mtakula utajiri wa mataifa,

nanyi katika utajiri wao mtajisifu.

7Badala ya aibu yao

watu wangu watapokea sehemu maradufu,

na badala ya fedheha

watafurahia katika urithi wao;

hivyo watarithi sehemu maradufu katika nchi yao,

nayo furaha ya milele itakuwa yao.

8“Kwa maana Mimi, Bwana , napenda haki,

na ninachukia unyangʼanyi na uovu.

Katika uaminifu wangu nitawapa malipo yao

na kufanya agano la milele nao.

9Wazao wao watajulikana miongoni mwa mataifa,

na uzao wao miongoni mwa makabila ya watu.

Wale wote watakaowaona watatambua

kuwa ni taifa ambalo Bwana amelibariki.”

10Ninafurahia sana katika Bwana ,

nafsi yangu inashangilia katika Mungu wangu.

Kwa maana amenivika mavazi ya wokovu,

na kunipamba kwa joho la haki,

kama vile bwana arusi apambavyo

kichwa chake kama kuhani,

na kama bibi arusi ajipambavyo

kwa vito vyake vya thamani.

11Kwa maana kama vile ardhi ifanyavyo chipukizi kuota,

na bustani isababishavyo mbegu kuota,

ndivyo Bwana Mwenyezi atafanya haki na sifa

zichipuke mbele ya mataifa yote.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.