Isaya 63

Isaya 63

Siku ya Mungu ya kisasi na ukombozi

1Ni nani huyu anayekuja kutoka Edomu,

kutoka Bosra, mwenye mavazi yaliyotiwa madoa mekundu?

Ni nani huyu, aliyevikwa joho la kifahari,

anayetembea kwa ukuu wa nguvu zake?

“Mimi ndimi, nisemaye katika haki,

mwenye nguvu wa kuokoa.”

2Kwa nini mavazi yako ni mekundu,

kama ya yule akanyagaye shinikizo la zabibu?

3“Nimekanyaga shinikizo la kukamulia zabibu peke yangu;

kutoka mataifa hakuna mtu aliyekuwa pamoja nami.

Nimewaponda kwa miguu katika hasira yangu

na kuwakanyaga chini katika ghadhabu yangu;

damu yao ilitia matone kwenye mavazi yangu,

na kutia madoa nguo zangu zote.

4Kwa kuwa siku ya kisasi ilikuwa moyoni mwangu,

mwaka wa ukombozi wangu umefika.

5Nilitazama, lakini hapakuwa yeyote wa kunisaidia,

nilishangaa kwa kuwa hapakuwa yeyote aliyetoa msaada;

hivyo mkono wangu wenyewe ndio ulionifanyia wokovu,

na ghadhabu yangu mwenyewe ndiyo iliyonitegemeza.

6Nilikanyaga mataifa kwa miguu katika hasira yangu,

katika ghadhabu yangu niliwalewesha,

na kumwaga damu yao juu ya ardhi.”

Kusifu na kuomba

7Nitasimulia kuhusu wema wa Bwana ,

kwa matendo ambayo apaswa kusifiwa,

sawasawa na yote ambayo Bwana

ametenda kwa ajili yetu:

naam, mambo mengi mema aliyoyatenda

kwa ajili ya nyumba ya Israeli,

sawasawa na huruma zake

na wema wake mwingi.

8Alisema, “Hakika wao ni watu wangu,

wana ambao hawatanidanganya”;

hivyo akawa Mwokozi wao.

9Katika taabu zao zote naye alitaabika,

na malaika wa uso wake akawaokoa.

Katika upendo wake na rehema zake aliwakomboa,

akawainua na kuwachukua siku zote zilizopita.

10Lakini waliasi,

na kumhuzunisha Roho Mtakatifu wake.

Hivyo aligeuka na kuwa adui yao,

na yeye mwenyewe akapigana dhidi yao.

11Ndipo watu wake wakazikumbuka siku zilizopita,

siku za Musa na watu wake:

yuko wapi yeye aliyewaleta kupitia katikati ya bahari,

pamoja na wachungaji wa kundi lake?

Yuko wapi yule aliyeweka

Roho wake Mtakatifu katikati yao,

12aliyetuma mkono wake uliotukuka wenye nguvu

kuwa katika mkono wa kuume wa Musa,

aliyegawa maji ya bahari mbele yao,

ili kujipatia jina milele,

13aliyewaongoza kupitia kwenye vilindi?

Kama farasi katika nchi iliyo wazi,

wao hawakujikwaa,

14kama ngʼombe wanaoshuka bondeni,

walipewa pumziko na Roho wa Bwana .

Hivi ndivyo ulivyowaongoza watu wako

ili kujipatia jina tukufu.

15Tazama chini kutoka mbinguni ukaone

kutoka kiti chako cha enzi

kilichoinuliwa juu, kitakatifu na kitukufu.

Uko wapi wivu wako na uweza wako?

Umetuzuilia wema wako na huruma zako.

16Lakini wewe ni Baba yetu,

ingawa Abrahamu hatufahamu sisi

wala Israeli hatutambui;

wewe, Ee Bwana , ndiwe Baba yetu,

Mkombozi wetu tangu zamani za kale ndilo jina lako.

17Ee Bwana , kwa nini unatuacha twende mbali na njia zako,

na kuifanya mioyo yetu migumu hata hatukukuheshimu?

Rudi kwa ajili ya watumishi wako,

yale makabila ambayo ni urithi wako.

18Kwa maana kwa muda mfupi watu wako walimiliki mahali pako patakatifu,

lakini sasa adui zetu wamepakanyaga mahali patakatifu pako.

19Sisi tumekuwa kama wale ambao hujawatawala kamwe,

kama wale ambao hawajaitwa kwa jina lako.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.