Isaya 65

Isaya 65

Hukumu na wokovu

1“Nilijifunua kwa watu wale ambao hawakuniulizia.

Nimeonekana na watu wale ambao hawakunitafuta.

Kwa taifa lile ambalo halikuliita Jina langu,

nilisema, ‘Niko hapa, niko hapa.’

2Mchana kutwa nimeinyoosha mikono yangu

kwa watu wakaidi,

wanaoenda katika njia ambazo si nzuri,

wafuatao mawazo yao wenyewe:

3taifa ambalo daima hunikasirisha

machoni pangu,

wakitoa dhabihu katika bustani

na kufukiza uvumba juu ya madhabahu za matofali;

4watu waketio katika makaburi

na kukesha mahali pa siri,

walao nyama za nguruwe,

nazo sufuria zao zina mchuzi wa nyama zilizo najisi,

5wasemao, ‘Kaa mbali; usinikaribie,

kwa maana mimi ni mtakatifu mno kwako!’

Watu wa aina hiyo ni moshi katika pua zangu,

ni moto uwakao mchana kutwa.

6“Tazama, jambo hili hubakia limeandikwa mbele zangu:

sitanyamaza, bali nitalipiza kwa ukamilifu;

nitalipiza mapajani mwao:

7dhambi zenu na dhambi za baba zenu,”

asema Bwana .

“Kwa sababu walitoa dhabihu za kuteketezwa juu ya milima

na kunichokoza mimi juu ya vilima,

nitawapimia mapajani mwao

malipo makamilifu kwa matendo yao ya zamani.”

8Hili ndilo asemalo Bwana :

“Kama vile divai mpya ingali bado inapatikana

katika kishada cha zabibu,

nao watu husema, ‘Usikiharibu,

kwa kuwa bado kuna baraka ndani yake,’

hivyo ndivyo nitakavyofanya kwa ajili ya watumishi wangu;

sitawaangamiza wote.

9Nitawaleta wazao kutoka kwa Yakobo,

na kutoka kwa Yuda watakaomiliki milima yangu,

nao watu wangu wateule watairithi,

nako huko wataishi watumishi wangu.

10Sharoni itakuwa malisho

kwa ajili ya makundi ya kondoo,

na Bonde la Akori mahali pa kupumzikia

kwa makundi ya ngʼombe,

kwa ajili ya watu wangu wanaonitafuta.

11“Bali ninyi mnaomwacha Bwana

na kuusahau mlima wangu mtakatifu,

ninyi mnaoandaa meza kwa ajili ya Bahati,

na kujaza mabakuli ya mvinyo uliochanganywa

kwa ajili ya Ajali,

12nitawaagiza mfe kwa upanga,

nanyi nyote mtainama chini ili kuchinjwa;

kwa kuwa niliwaita lakini hamkuitika,

nilisema lakini hamkusikiliza.

Mlitenda maovu machoni pangu,

nanyi mkachagua mambo yale yanayonichukiza.”

13Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:

“Watumishi wangu watakula,

lakini ninyi mtaona njaa;

watumishi wangu watakunywa

lakini ninyi mtaona kiu;

watumishi wangu watafurahi,

lakini ninyi mtaona haya.

14Watumishi wangu wataimba

kwa furaha ya mioyo yao,

lakini ninyi mtalia

kutokana na uchungu wa moyoni,

na kupiga yowe kwa sababu

ya uchungu wa roho zenu.

15Mtaliacha jina lenu

kuwa laana kwa watu wangu waliochaguliwa;

Bwana Mwenyezi atawaua ninyi,

lakini watumishi wake atawapa jina jingine.

16Yeye aombaye baraka katika nchi

atafanya hivyo kwa Mungu wa kweli;

yeye aapaye katika nchi

ataapa kwa Mungu wa kweli.

Kwa kuwa taabu za zamani zitasahaulika

na kufichwa kutoka machoni pangu.

Mbingu mpya na dunia mpya

17“Tazama, nitaumba

mbingu mpya na dunia mpya.

Mambo ya zamani hayatakumbukwa,

wala hayatakuja akilini.

18Lakini furahini na kushangilia daima

katika hivi nitakavyoumba,

kwa kuwa nitaumba Yerusalemu uwe wa kupendeza,

nao watu wake wawe furaha.

19Nami nitaifurahia Yerusalemu

na kuwafurahia watu wangu;

sauti ya maombolezo na ya kilio

haitasikika humo tena.

20“Kamwe hapatakuwa tena ndani yake

mtoto mchanga atakayeishi siku chache tu,

au mzee ambaye hataishi akatimiza miaka yake.

Yeye atakayekufa akiwa na umri wa miaka mia moja

atahesabiwa kwamba ni kijana tu,

yeye ambaye hatafika miaka mia moja,

atahesabiwa kuwa amelaaniwa.

21Watajenga nyumba na kuishi ndani yake;

watapanda mashamba ya mizabibu na kula matunda yake.

22Hawatajenga nyumba, nao watu wengine waishi ndani yake,

au kupanda mazao na wengine wale.

Kwa kuwa kama zilivyo siku za mti,

ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu,

wateule wangu watafurahia kwa siku nyingi

kazi za mikono yao.

23Hawatajitaabisha kwa kazi bure,

wala hawatazaa watoto ili wapatwe na majanga,

kwa kuwa watakuwa taifa lililobarikiwa na Bwana ,

wao na wazao wao pamoja nao.

24Kabla hawajaita, nitajibu,

nao wakiwa katika kunena, nitasikia.

25Mbwa-mwitu na mwana-kondoo watalisha pamoja,

naye simba atakula nyasi kama maksai,

lakini mavumbi yatakuwa chakula cha nyoka.

Hawatadhuru wala kuharibu

katika mlima wangu mtakatifu wote,”

asema Bwana .

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.