Waamuzi 6

Waamuzi 6

Gideoni

1Waisraeli wakafanya tena yaliyo maovu mbele za Bwana , naye Bwana akawatia mikononi mwa Wamidiani kwa muda wa miaka saba.

2Kwa kuwa Wamidiani walikuwa na nguvu juu yao, Waisraeli walijitengenezea maficho milimani, kwenye mapango, na katika ngome.

3Kila wakati Waisraeli walipopanda mazao mashambani, Wamidiani, Waamaleki na mataifa mengine ya mashariki walivamia nchi yao.

4Wakapiga kambi katika mashamba yao na kuharibu mazao ya nchi yote hadi kufikia Gaza, wala hawakuacha kiumbe chochote kilicho hai kwa Waisraeli, iwe kondoo au ngʼombe au punda.

5Walipanda na mifugo yao na mahema yao, mfano wa makundi ya nzige. Ilikuwa haiwezekani kuwahesabu watu na ngamia wao; wakavamia nchi ili kuiharibu.

6Wamidiani wakaifanya Israeli kuwa maskini sana, hata Waisraeli wakamlilia Bwana kumwomba msaada.

7Waisraeli walipomlilia Bwana kwa sababu ya Wamidiani,

8Bwana akawapelekea nabii, ambaye aliwaambia, “Hili ndilo Bwana , Mungu wa Israeli, asemalo: Niliwapandisha mtoke Misri, toka nchi ya utumwa.

9Nikawaokoa kutoka mikononi mwa Wamisri na kutoka mikononi mwa watesi wenu wote. Nikawafukuza watoke mbele yenu, nami nikawapa ninyi nchi yao.

10Nikawaambia, ‘Mimi ndimi Bwana Mungu wenu; msiiabudu miungu ya Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao!’ Lakini ninyi hamkuitii sauti yangu.”

11Malaika wa Bwana akaja akaketi chini ya mwaloni ulio Ofra, ambao ulikuwa mali ya Yoashi Mwabiezeri, pale Gideoni mwanawe alikuwa akipepeta ngano penye shinikizo la kukamulia zabibu, ili kuificha Wamidiani wasiione.

12Malaika wa Bwana alipomtokea Gideoni, akamwambia, “Bwana yu pamoja nawe, ewe shujaa mwenye nguvu.”

13Gideoni akajibu, “Nisamehe, Ee Bwana wangu. Kama Bwana yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametutokea? Yako wapi yale matendo yake makuu ambayo baba zetu walitusimulia juu yake waliposema, ‘Je, Bwana hakutupandisha kutoka Misri?’ Lakini sasa Bwana ametuacha na kututia katika mkono wa Midiani.”

14Bwana akamgeukia na kusema “Nenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli kutoka mikononi mwa Wamidiani. Je, si mimi ninayekutuma wewe?”

15Gideoni akauliza, “Ee Bwana wangu, nitawezaje kuwaokoa Israeli? Ukoo wangu ndio dhaifu kuliko zote katika Manase, nami ndiye mdogo wa wote katika jamaa yangu.”

16Bwana akamjibu, “Nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kana kwamba walikuwa ni mtu mmoja.”

17Gideoni akajibu, “Kama basi nimepata kibali machoni pako, nipe ishara kuonesha kuwa kweli ni wewe unayesema nami.

18Tafadhali nakuomba usiondoke hapa hadi nitakaporudi, nilete sadaka yangu na kuiweka mbele yako.”

Naye Bwana akamwambia, “Nitangoja hadi utakaporudi.”

19Gideoni akaingia ndani ya nyumba yake na kuandaa mwana-mbuzi pamoja na kuoka mikate isiyotiwa chachu kutokana na efa moja ya unga. Akaweka nyama kwenye kikapu na mchuzi kwenye chungu, akamletea huyo malaika hapo nje chini ya mwaloni, akampa.[#6:19 Efa moja ni sawa na lita 22.]

20Malaika wa Mungu akamwambia, “Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uviweke juu ya mwamba huu na umimine huo mchuzi juu yake.” Gideoni akafanya hivyo.

21Malaika wa Bwana akainyoosha fimbo iliyokuwa mkononi mwake, ncha yake ikagusa ile nyama na ile mikate isiyotiwa chachu, nao moto ukatoka kwenye mwamba ukateketeza ile nyama na ile mikate. Malaika wa Bwana akatoweka machoni pake.

22Gideoni alipotambua kuwa ni malaika wa Bwana , akapaza sauti, akasema, “Ole wangu, Bwana Mwenyezi! Kwa kuwa nimemwona malaika wa Bwana uso kwa uso!”

23Lakini Bwana akamwambia, “Amani iwe kwako! Usiogope. Hutakufa.”

24Hivyo Gideoni akamjengea Bwana madhabahu mahali pale na kupaita Yehova-Shalomu. Hata leo imesimama huko Ofra ya Waabiezeri.[#6:24 maana yake ni Amani]

25Usiku ule ule Bwana akamwambia, “Mchukue ngʼombe dume wa baba yako, yule wa pili mwenye miaka saba, ubomoe madhabahu ya Baali aliyo nayo baba yako, na ukaikate nguzo ya Ashera iliyo karibu nayo.

26Kisha mjengee Bwana Mungu wako madhabahu kwa taratibu zake juu ya mwamba katika ngome hii. Kwa kutumia kuni za hiyo nguzo ya Ashera uliyoikatakata, mtoe sadaka huyo dume wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa.”

27Basi Gideoni akawachukua watumishi wake kumi na kufanya kama Bwana alivyomwambia. Lakini kwa kuwa aliwaogopa jamaa yake na watu wa mji, akafanya haya usiku badala ya mchana.

28Watu wa mji walipoamka asubuhi, tazama madhabahu ya Baali imebomolewa, na nguzo ya Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwakatwa, na yule ngʼombe wa pili ametolewa sadaka juu ya madhabahu iliyojengwa upya!

29Wakaulizana, “Ni nani aliyetenda mambo haya?”

Walipochunguza kwa makini, wakaambiwa, “Ni Gideoni mwana wa Yoashi, ndiye alitenda hivi.”

30Watu wa mji wakamwambia Yoashi, “Mlete mwanao hapa. Ni lazima afe, kwa sababu amebomoa madhabahu ya Baali na kukatakata nguzo ya Ashera iliyokuwa karibu nayo.”

31Lakini Yoashi akaambia umati wa watu waliomzunguka wakiwa kinyume naye, “Je, ninyi mtamtetea Baali? Mnajaribu kumwokoa? Yeyote mwenye kumpigania atauawa kufikia kesho asubuhi! Kama Baali ni mungu kweli, anaweza kujitetea mwenyewe wakati mtu anapobomoa madhabahu yake.”

32Basi siku ile wakamwita Gideoni “Yerub-Baali,” yaani “Baali na ashindane naye,” kwa sababu alibomoa madhabahu yake.

33Basi Wamidiani wote, Waamaleki na mataifa mengine ya mashariki wakaunganisha majeshi yao, wakavuka ngʼambo ya Yordani na kupiga kambi katika Bonde la Yezreeli.

34Ndipo Roho wa Bwana akamjia Gideoni, naye Gideoni akapiga tarumbeta kuwaita Waabiezeri ili wamfuate.

35Akatuma wajumbe waende katika Manase yote, akiwataka wachukue silaha na pia katika Asheri, Zabuloni na Naftali, nao wakakwea ili kukutana nao.

36Gideoni akamwambia Mungu, “Kama utawaokoa Waisraeli kwa mkono wangu, kama ulivyoahidi:

37tazama, nitaweka manyoya ya kondoo kwenye sakafu ya kupuria nafaka, na kama utakuwepo umande juu ya manyoya tu, na ardhi yote ikiwa kavu, ndipo nitakapojua kuwa utaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema.”

38Hivyo ndivyo ilivyotokea. Gideoni akaamka asubuhi na mapema kesho yake, akayakamua yale manyoya yenye umande, yakatoka maji kiasi cha kujaa bakuli.

39Kisha Gideoni akamwambia Bwana , “Usinikasirikie. Ninaomba nifanye ombi moja lingine. Niruhusu nifanye jaribio jingine moja kwa manyoya haya. Wakati huu uyafanye manyoya kuwa kavu, na ardhi yote ifunikwe na umande.”

40Usiku ule Mungu akafanya hivyo. Manyoya yakawa kavu, na ardhi yote ikafunikwa na umande.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.