The chat will start when you send the first message.
1Maneno ya Yeremia mwana wa Hilkia, mmoja wa makuhani katika mji wa Anathothi, katika nchi ya Benyamini.
2Neno la Bwana lilimjia katika mwaka wa kumi na tatu wa utawala wa Yosia mwana wa Amoni mfalme wa Yuda,
3na pia wakati wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, hadi mwezi wa tano wa mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, wakati watu wa Yerusalemu walipopelekwa uhamishoni.
4Neno la Bwana lilinijia, kusema,
5“Kabla sijakuumba ndani ya tumbo la mama yako, nilikujua;
kabla hujazaliwa nilikutenga kwa kazi maalum;
nilikuweka uwe nabii kwa mataifa.”
6Nami nikasema, “Aa, Bwana Mwenyezi, sijui kusema, kwani mimi ni mtoto mdogo tu.”
7Lakini Bwana akaniambia, “Usiseme, ‘Mimi ni mtoto mdogo tu.’ Utaenda popote nitakapokutuma na kunena lolote nitakalokuagiza.
8Usiwaogope, kwa maana niko pamoja nawe nikuokoe,” asema Bwana .
9Kisha Bwana akaunyoosha mkono wake na kugusa kinywa changu, akaniambia, “Sasa nimeyaweka maneno yangu kinywani mwako.
10Tazama, leo nimekuweka juu ya mataifa na falme ili kungʼoa na kubomoa, kuharibu na kuangamiza, kujenga na kupanda.”
11Neno la Bwana likanijia kusema, “Je, Yeremia unaona nini?”
Nami nikajibu, “Naona tawi la mti wa mlozi.”
12Bwana akaniambia, “Umeona vyema kwa maana ninaliangalia neno langu ili kuona kwamba limetimizwa.”
13Neno la Bwana likanijia tena, “Unaona nini?”
Nikajibu, “Naona chungu kinachochemka, kikiwa kimeinama kutoka kaskazini.”
14Bwana akaniambia, “Kutoka kaskazini maafa yatamwagwa kwa wote wanaoishi katika nchi.
15Nitawaita watu wote wa falme za kaskazini,” asema Bwana .
“Wafalme wao watakuja na kuweka viti vyao vya utawala
katika maingilio ya malango ya Yerusalemu,
watakuja dhidi ya kuta zake zote zinazouzunguka,
na dhidi ya miji yote ya Yuda.
16Nitatoa hukumu zangu kwa watu wangu
kwa sababu ya uovu wao wa kuniacha mimi,
kwa kufukiza uvumba kwa miungu mingine
na kuabudu kazi za mikono yao.
17“Jiandae! Simama useme chochote nitakachokuamuru. Usiwaogope, la sivyo nitakufanya uwaogope wao.
18Leo nimekufanya mji wenye ngome, nguzo ya chuma, na ukuta wa shaba ili kusimama dhidi ya nchi yote: dhidi ya wafalme wa Yuda, maafisa wake, makuhani wake na watu wa nchi hiyo.
19Watapigana nawe lakini hawatakushinda, kwa kuwa niko pamoja nawe, nami nitakuokoa,” asema Bwana .