The chat will start when you send the first message.
1Hili ndilo Bwana aliloniambia: “Nenda ununue mkanda wa kitani, ujivike kiunoni mwako, lakini usiuache uguse maji.”
2Kwa hiyo nikanunua mkanda, kama Bwana alivyoniagiza, nikajivika kiunoni.
3Ndipo neno la Bwana likanijia kwa mara ya pili:
4“Chukua mkanda ulionunua ambao umeuvaa kiunoni mwako, uende sasa Frati uufiche ndani ya ufa mdogo kwenye mwamba.”
5Ndipo nikaenda na kuuficha ule mkanda huko Frati, kama Bwana alivyoniamuru.
6Baada ya siku nyingi Bwana akaniambia, “Nenda sasa Frati ukauchukue ule mkanda niliokuambia uufiche huko.”
7Hivyo nikaenda Frati na kuuchimbua ule mkanda kutoka pale nilipokuwa nimeuficha, lakini sasa ulikuwa umeharibika na haufai tena kabisa.
8Ndipo neno la Bwana likanijia:
9“Hili ndilo asemalo Bwana : ‘Vivyo hivyo ndivyo nitakavyokiharibu kiburi cha Yuda na kiburi kikuu cha Yerusalemu.
10Watu hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wafuatao ukaidi wa mioyo yao na kufuata miungu mingine wakiitumikia na kuiabudu, watakuwa kama mshipi huu ambao haufai kabisa!
11Kwa maana kama vile mshipi ufungwavyo kiunoni mwa mtu, ndivyo nilivyoifunga nyumba yote ya Israeli na nyumba yote ya Yuda,’ asema Bwana , ‘ili wawe watu wangu kwa ajili ya utukufu wangu, sifa na heshima yangu. Lakini hawajasikiliza.’
12“Waambie: ‘Hili ndilo Bwana , Mungu wa Israeli, asemalo: kila kiriba inapasa kijazwe mvinyo.’ Wakikuambia, ‘Kwani hatujui kwamba kila kiriba inapasa kijazwe mvinyo?’
13Uwaambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana : nitawajaza ulevi wote wanaoishi katika nchi hii, pamoja na wafalme wanaoketi kwenye kiti cha ufalme cha Daudi, makuhani, manabii na wakaaji wote wa Yerusalemu.
14Nitawagombanisha kila mmoja na mwenzake, baba na wana wao, asema Bwana . Sitawarehemu wala kuwahurumia ili niache kuwaangamiza.’ ”
15Sikieni na mzingatie,
msiwe na kiburi,
kwa kuwa Bwana amenena.
16Mpeni utukufu Bwana Mungu wenu,
kabla hajaleta giza,
kabla miguu yenu haijajikwaa
juu ya vilima vitakavyotiwa giza.
Mlitarajia nuru,
lakini ataifanya kuwa giza nene
na kuibadili kuwa huzuni kubwa.
17Lakini kama hamtasikiliza,
nitalia sirini
kwa ajili ya kiburi chenu;
macho yangu yatalia kwa uchungu,
yakitiririka machozi,
kwa sababu kundi la kondoo la Bwana
litachukuliwa mateka.
18Mwambie mfalme na mama malkia,
“Shukeni kutoka viti vyenu vya utawala,
kwa kuwa taji zenu za utukufu
zitaanguka kutoka vichwani mwenu.”
19Miji ya Negebu itafungwa,
wala hapatakuwa na mtu wa kuifungua.
Watu wa Yuda wote watapelekwa uhamishoni,
wakichukuliwa kabisa waende mbali.
20Inua macho yako uone
wale wanaokuja kutoka kaskazini.
Liko wapi lile kundi ulilokabidhiwa,
wale kondoo uliojivunia?
21Utasema nini Bwana atakapowaweka juu yako
wale ulioungana nao kama rafiki zako maalum?
Je, hutapatwa na uchungu kama mwanamke
aliye katika uchungu wa kuzaa?
22Nawe ukijiuliza,
“Kwa nini haya yamenitokea?”
Ni kwa sababu ya dhambi zako nyingi
marinda yako yameraruliwa
na mwili wako umetendewa vibaya.
23Je, Mkushi aweza kubadili ngozi yake
au chui kubadili madoadoa yake?
Vivyo hivyo, wewe uliyezoea kutenda mabaya
huwezi kufanya mema.
24“Nitawatawanya kama makapi
yapeperushwayo na upepo wa jangwani.
25Hii ndiyo kura yako,
fungu nililokuamulia,”
asema Bwana ,
“kwa sababu umenisahau mimi
na kuamini miungu ya uongo.
26Nitayafunua marinda yako juu ya uso wako
ili aibu yako ionekane,
27yaani uzinzi wako na kulia kwako kulikojaa tamaa kama farasi,
na ukahaba wako usio na aibu!
Nimeyaona matendo yako ya machukizo
juu ya vilima na mashambani.
Ole wako, ee Yerusalemu!
Utaendelea kuwa najisi hadi lini?”