Yeremia 15

Yeremia 15

Adhabu isiyoepukika

1Kisha Bwana akaniambia: “Hata kama Musa na Samweli wangesimama mbele zangu, moyo wangu usingewaelekea watu hawa. Waondoe mbele za macho yangu! Waache waende!

2Nao wakikuuliza, ‘Twende wapi?’ Waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana :

“ ‘Wale waliowekwa kwa ajili ya kufa, na wafe;

waliowekewa kufa kwa upanga, kwa upanga;

waliowekewa kufa kwa njaa, kwa njaa;

na waliowekewa kupelekwa uhamishoni,

wapelekwe uhamishoni.’ ”

3Bwana asema, “Nitatuma aina nne za waangamizi: upanga ili kuua, mbwa ili kukokota mbali, ndege wa angani na wanyama wa nchi ili wale na waangamize.

4Nitawafanya wawe machukizo kwa falme zote za dunia kwa sababu ya kile alichofanya Manase mwana wa Hezekia mfalme wa Yuda huko Yerusalemu.

5“Ni nani atakayekuhurumia, ee Yerusalemu?

Ni nani atakayeomboleza kwa ajili yako?

Ni nani atakayesimama ili kuuliza

kuhusu hali yako?

6Umenikataa mimi,” asema Bwana .

“Unazidi kukengeuka.

Hivyo nitanyoosha mkono wangu juu yako na kukuangamiza,

siwezi kuendelea kukuonea huruma.

7Nitawapepeta kwa ungo

kwenye malango ya miji ya nchi.

Nitaleta msiba na maangamizi juu ya watu wangu,

kwa maana hawajabadili njia zao.

8Nitawafanya wajane wao kuwa wengi

kuliko mchanga wa bahari.

Wakati wa adhuhuri nitamleta mwangamizi

dhidi ya mama wa vijana wao wa kiume;

kwa ghafula nitaleta juu yao

maumivu makuu na hofu kuu.

9Mama mwenye watoto saba atazimia

na kupumua pumzi yake ya mwisho.

Jua lake litatua kukiwa bado mchana,

atatahayarika na kufedheheka.

Wale wote waliobaki nitawaua kwa upanga

mbele ya adui zao,”

asema Bwana .

10Ole wangu, mama yangu, kwamba ulinizaa,

mtu ambaye ulimwengu wote

unashindana na kugombana naye!

Sikukopa wala sikukopesha,

lakini kila mmoja ananilaani.

11Bwana akasema,

“Hakika nitakuokoa kwa kusudi jema,

hakika nitawafanya adui zako wakuombe msaada

nyakati za maafa na nyakati za dhiki.

12“Je, mtu aweza kuvunja chuma,

chuma kinachotoka kaskazini, au avunje shaba?

13“Utajiri wako na hazina zako nitavitoa kuwa nyara,

bila gharama,

kwa sababu ya dhambi zako zote

katika nchi yako yote.

14Nitakufanya uwe mtumwa wa adui zako

katika nchi usiyoijua,

kwa kuwa katika hasira yangu moto umewashwa

utakaowaka juu yako daima.”

15Wewe unafahamu, Ee Bwana ,

unikumbuke na unitunze mimi.

Lipiza kisasi juu ya watesi wangu.

Kwa uvumilivu wako usiniondolee mbali;

kumbuka jinsi ninavyoshutumiwa.

16Maneno yako yalipokuja, niliyala;

yakawa shangwe yangu

na furaha ya moyo wangu,

kwa kuwa nimeitwa kwa jina lako,

Ee Bwana Mungu wa majeshi.

17Kamwe sikuketi katika kundi la wafanyao sherehe,

wala kamwe sikujifurahisha pamoja nao;

niliketi peke yangu kwa sababu mkono wako ulikuwa juu yangu,

na wewe ulikuwa umenijaza hasira.

18Kwa nini maumivu yangu hayakomi,

na jeraha langu ni la kuhuzunisha,

wala haliponyeki?

Je, utakuwa kwangu kama kijito cha udanganyifu,

kama chemchemi iliyokauka?

19Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana :

“Ukitubu, nitakurejesha

ili uweze kunitumikia;

ukinena maneno yenye maana,

wala si ya upuzi,

utakuwa mnenaji wangu.

Watu hawa ndio watakaokugeukia,

wala si wewe utakayewageukia wao.

20Nitakufanya wewe uwe ukuta kwa watu hawa,

ngome ya ukuta wa shaba;

watapigana nawe

lakini hawatakushinda,

kwa maana mimi niko pamoja nawe

kukuponya na kukuokoa,”

asema Bwana .

21“Nitakuokoa kutoka mikono ya waovu,

na kukukomboa kutoka makucha ya watu wakatili.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.