Yeremia 18

Yeremia 18

Katika nyumba ya mfinyanzi

1Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Bwana :

2“Shuka uende hadi nyumba ya mfinyanzi, nami huko nitakupa ujumbe wangu.”

3Kwa hiyo nikashuka hadi nyumba ya mfinyanzi, nikamkuta akifinyanga kwa gurudumu lake.

4Lakini chombo alichokuwa akikifinyanga kutokana na udongo kilivunjika mikononi mwake; hivyo mfinyanzi akakifanya kuwa chombo kingine, umbo jingine kwa namna alivyoona ni vyema machoni pake.

5Kisha neno la Bwana likanijia kusema:

6“Ee nyumba ya Israeli, je, siwezi kuwafanyia kama huyu mfinyanzi afanyavyo?” asema Bwana . “Kama vile udongo ulivyo katika mikono ya mfinyanzi, ndivyo mlivyo katika mkono wangu, ee nyumba ya Israeli.

7Wakati wowote nitatangaza kuwa taifa au ufalme utangʼolewa, utaangushwa na kuangamizwa,

8Lakini ikiwa taifa nililolionya litatubu na kuacha uovu wake nitaghairi, wala sitaleta maafa niliyokuwa nimekusudia kwa taifa hilo.

9Wakati mwingine nitakapotangaza kuwa taifa au ufalme utasimikwa na kujengwa,

10ikiwa litafanya uovu mbele zangu na halitaitii sauti yangu, nitaghairi kutenda jema nililokuwa nimekusudia.

11“Basi kwa hiyo waambie watu wa Yuda na wale wanaoishi Yerusalemu, ‘Hili ndilo asemalo Bwana : Tazama! Ninaandaa maafa juu yenu, nami ninapanga mabaya dhidi yenu. Kwa hiyo geukeni kutoka njia zenu mbaya, kila mmoja wenu. Tengenezeni njia zenu na matendo yenu.’

12Lakini wao watajibu, ‘Hakuna faida. Tutaendelea na mipango yetu wenyewe, kila mmoja wetu atafuata ukaidi wa moyo wake mbaya.’ ”

13Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana :

“Ulizia miongoni mwa mataifa:

Ni nani alishasikia jambo kama hili?

Jambo la kutisha sana limefanywa

na Bikira Israeli.

14Je, barafu ya Lebanoni iliwahi kutoweka

kwenye miteremko yake ya mawe wakati wowote?

Je, maji yake baridi kutoka vyanzo vilivyo mbali

yaliwahi kukoma kutiririka?

15Lakini watu wangu wamenisahau mimi,

wanafukizia uvumba sanamu batili,

zilizowafanya wajikwae katika njia zao

na katika mapito ya zamani.

Zimewafanya wapite kwenye vichochoro

na kwenye barabara ambazo hazikujengwa.

16Nchi yao itakuwa kitu cha kutisha,

na cha kudharauliwa daima;

wote wapitao karibu nayo watashangaa

na kutikisa vichwa vyao.

17Kama upepo unaotoka mashariki,

nitawatawanya mbele ya adui zao;

nitawapa kisogo wala sio uso,

katika siku ya maafa yao.”

18Wakasema, “Njooni, tutunge hila dhidi ya Yeremia; kwa kuwa kufundisha sheria kwa kuhani hakutapotea, wala shauri litokalo kwa mwenye hekima, wala neno la manabii. Hivyo njooni, tumshambulie kwa ndimi zetu na tusijali chochote asemacho.”

19Nisikilize, Ee Bwana ,

sikia wanayosema washtaki wangu!

20Je, mema yalipwe kwa mabaya?

Lakini wao wamenichimbia shimo.

Kumbuka kwamba nilisimama mbele yako

na kunena mema kwa ajili yao,

ili wewe ugeuze hasira yako kali mbali nao.

21Kwa hiyo uwaache watoto wao waone njaa;

uwaache wauawe kwa makali ya upanga.

Wake zao wasiwe na watoto, na wawe wajane;

wanaume wao wauawe,

nao vijana wao wa kiume

wachinjwe kwa upanga vitani.

22Kilio na kisikike kutoka nyumba zao

ghafula uwaletapo adui dhidi yao,

kwa kuwa wamechimba shimo ili kunikamata

na wameitegea miguu yangu mitego.

23Lakini unajua, Ee Bwana ,

hila zao zote za kuniua.

Usiyasamehe makosa yao

wala usifute dhambi zao

mbele za macho yako.

Wao na waangamizwe mbele zako;

uwaadhibu wakati wa hasira yako.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.