Yeremia 23

Yeremia 23

Tawi la haki

1“Ole wao wachungaji wanaoharibu na kutawanya kondoo wa malisho yangu!” asema Bwana .

2Kwa hiyo hili ndilo Bwana , Mungu wa Israeli, analowaambia wachungaji wanaowachunga watu wangu: “Kwa sababu mmelitawanya kundi langu na kuwafukuzia mbali, wala hamkuwatunza, basi mimi nitawaadhibu kwa ajili ya uovu mliofanya,” asema Bwana .

3“Mimi mwenyewe nitayakusanya mabaki ya kundi langu kutoka nchi zote ambazo nimewafukuzia, nami nitawarudisha katika malisho yao, ambapo watazaa na kuongezeka idadi yao.

4Nitaweka wachungaji juu yao ambao watawachunga, nao hawataogopa tena au kutishwa, wala hatapotea hata mmoja,” asema Bwana .

5Bwana asema, “Siku zinakuja,

nitakapomwinulia Daudi Tawi lenye haki,

Mfalme atakayetawala kwa hekima,

na kutenda lililo haki na sawa katika nchi.

6Katika utawala wake, Yuda ataokolewa,

na Israeli ataishi salama.

Hili ndilo jina atakaloitwa:

Bwana ni Haki Yetu.”

7Bwana asema, “Hivyo basi, siku zinakuja, ambapo watu hawatasema tena, ‘Hakika kama Bwana aishivyo, aliyewapandisha Waisraeli kutoka Misri,’

8bali watasema, ‘Hakika kama Bwana aishivyo, aliyewatoa wazao wa Israeli kutoka nchi ya kaskazini na nchi zote alizokuwa amewafukuzia.’ Ndipo wataishi katika nchi yao wenyewe.”

Manabii wasemao uongo

9Kuhusu manabii:

Moyo wangu umevunjika ndani yangu;

mifupa yangu yote inatetemeka.

Nimekuwa kama mtu aliyelewa,

kama mtu aliyelemewa na divai,

kwa sababu ya Bwana

na maneno yake matakatifu.

10Nchi imejaa wazinzi;

kwa sababu ya laana, nchi imekauka,

na malisho ya nyikani yamekauka.

Mwenendo wa manabii ni mbaya

na mamlaka yao si ya haki.

11“Nabii na kuhani wote si wacha Mungu;

hata hekaluni mwangu ninaona uovu wao,”

asema Bwana .

12“Kwa hiyo mapito yao yatakuwa utelezi,

watafukuziwa mbali gizani

na huko wataanguka.

Nitaleta maafa juu yao

katika mwaka wa kuadhibiwa kwao,”

asema Bwana .

13“Miongoni mwa manabii wa Samaria

nililiona jambo la kuchukiza:

Walitabiri kwa Baali

na kuwapotosha Israeli watu wangu.

14Nako miongoni mwa manabii wa Yerusalemu

nimeona jambo baya sana:

Wanafanya uzinzi

na kuenenda katika uongo.

Wanatia nguvu mikono ya watenda maovu,

kwa ajili hiyo hakuna yeyote

anayeachana na uovu wake.

Wote wako kama Sodoma kwangu;

watu na Yerusalemu wako kama Gomora.”

15Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana wa majeshi kuhusu manabii:

“Nitawafanya wale chakula kichungu

na kunywa maji yaliyotiwa sumu,

kwa sababu kutokana na manabii wa Yerusalemu

kutokumcha Mungu kumeenea katika nchi yote.”

16Hili ndilo asemalo Bwana wa majeshi:

“Msisikilize wanachowatabiria manabii,

wanawajaza matumaini ya uongo.

Wanasema maono kutoka akili zao wenyewe,

hayatoki katika kinywa cha Bwana .

17Huendelea kuwaambia wale wanaonidharau mimi,

‘Bwana asema: Mtakuwa na amani.’

Kwa wale wote wafuatao ugumu wa mioyo yao,

wao husema, ‘Hakuna dhara litakalowapata.’

18Lakini ni yupi miongoni mwao aliyesimama katika baraza la Bwana

ili kuona au kusikia neno lake?

Ni nani aliyesikiliza

na kusikia neno lake?

19Tazama, dhoruba ya Bwana

itatokea kwa ghadhabu,

kisulisuli kitazunguka na kuanguka

juu ya vichwa vya waovu.

20Hasira ya Bwana haitageuka

hadi amelitimiza kusudi la moyo wake.

Siku zijazo mtalifahamu kwa wazi.

21Mimi sikuwatuma manabii hawa,

lakini bado wamekimbia wakitangaza ujumbe wao.

Mimi sikusema nao,

lakini wametabiri.

22Lakini kama wangesimama barazani pangu,

wangetangaza maneno yangu kwa watu wangu,

nao wangewageuza kutoka njia zao mbaya

na kutoka matendo yao maovu.

23“Je, mimi ni Mungu aliye karibu tu,

wala si Mungu aliye pia mbali?”

Bwana asema.

24“Je, mtu yeyote aweza kujificha

mahali pa siri nisiweze kumwona?”

Bwana asema.

“Je, mimi sikuijaza mbingu na nchi?”

Bwana asema.

25“Nimesikia wanayoyasema manabii, hao wanaotabiri uongo kwa jina langu. Wanasema, ‘Nimeota ndoto! Nimeota ndoto!’

26Mambo haya yataendelea hata lini ndani ya mioyo ya hawa manabii wa uongo, ambao hutabiri maono ya uongo ya akili zao wenyewe?

27Wanadhani ndoto wanazoambiana wao kwa wao zitawafanya watu wangu walisahau jina langu, kama baba zao walivyolisahau kwa kumwabudu Baali.

28Mwache nabii aliye na ndoto aseme ndoto yake, lakini yule aliye na neno langu na aliseme kwa uaminifu. Kwa maana jani kavu lina uhusiano gani na ngano?” asema Bwana .

29“Je, neno langu si kama moto,” asema Bwana , “na kama nyundo ivunjayo mwamba vipande vipande?

30“Kwa hiyo, niko kinyume na manabii wanaoibiana maneno kana kwamba ni yangu,” asema Bwana .

31“Naam, mimi niko kinyume na manabii wanaotumia ndimi zao wenyewe na kusema, ‘Bwana asema.’

32Kweli, niko kinyume na hao wanaotabiri ndoto za uongo,” asema Bwana . “Wanazisimulia na kuwapotosha watu wangu kwa uongo wao bila kujali, lakini sikuwatuma wala sikuwaamuru. Hawawafaidi watu hawa hata kidogo,” asema Bwana .

Unabii wa uongo

33“Basi watu hawa, au nabii, au kuhani, watakapokuuliza, ‘Ujumbe wa Bwana ni nini?’ Wewe utawaambia, ‘Ninyi ndio ujumbe. Nami nitawavua kama vazi, asema Bwana .’

34Nabii, kuhani, au mtu yeyote akisema, ‘Huu ndio ujumbe wa Bwana ,’ nitamwadhibu huyo na nyumba yake.

35Mnaambiana kila mmoja na mwenzake, au kwa mtu wa nyumba yao: ‘Bwana amejibu nini?’ au ‘Bwana amesema nini?’

36Lakini kamwe msiseme tena, ‘Nina ujumbe wa Bwana ,’ kwa sababu kila neno la mtu binafsi linakuwa mzigo wake mwenyewe, na hivyo kupotosha maneno ya Mungu aliye hai, Bwana wa majeshi, Mungu wetu.

37Hivi ndivyo utakavyoendelea kumuuliza nabii: ‘Bwana amekujibu nini?’ au ‘Je, Bwana amesema nini?’

38Ingawa unadai, ‘Huu ndio ujumbe wa Bwana ,’ asema Bwana . Ulitumia maneno, ‘Huu ndio ujumbe wa Bwana ,’ Ingawa nilikuambia kuwa kamwe usiseme, ‘Huu ni ujumbe wa Bwana .’

39Kwa hiyo, hakika nitakusahau na kukutenga mbali na uso wangu pamoja na mji niliowapa ninyi na baba zenu.

40Nitaleta juu yako fedheha ya kudumu: yaani aibu ya kudumu ambayo haitasahaulika.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.