Yohana 7

Yohana 7

Kutokuamini kwa ndugu zake Yesu

1Baada ya mambo haya, Yesu alienda sehemu mbalimbali za Galilaya. Hakutaka kwenda Yudea kwa sababu viongozi wa Wayahudi huko walitaka kumuua.

2Sikukuu ya Vibanda ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.

3Hivyo ndugu zake Yesu wakamwambia, “Ondoka hapa uende Yudea ili wanafunzi Wako wapate kuona miujiza unayofanya.

4Mtu anayetaka kujulikana hafanyi mambo yake kwa siri. Kama unafanya mambo haya, jioneshe kwa ulimwengu.”

5Hata ndugu zake mwenyewe hawakumwamini.

6Yesu akawaambia, “Wakati wangu bado haujawadia, lakini wakati wenu upo siku zote.

7Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi, lakini unanichukia mimi kwa sababu ninawashuhudia kwamba matendo yao ni maovu.

8Ninyi nendeni kwenye Sikukuu, lakini mimi sitahudhuria Sikukuu hii kwa sababu wakati wangu haujawadia.”

9Baada ya kusema hayo, akabaki Galilaya.

Yesu kwenye Sikukuu ya Vibanda

10Lakini ndugu zake walipokwisha kuondoka kwenda kwenye Sikukuu, yeye pia alienda lakini kwa siri.

11Viongozi wa Wayahudi walikuwa wakimtafuta huko kwenye Sikukuu na kuulizana, “Yuko wapi huyu mtu?”

12Kulikuwa na minongʼono iliyoenea kumhusu Yesu katika umati wa watu, wakati wengine wakisema, “Ni mtu mwema.”

Wengine walikuwa wakisema, “La, yeye anawadanganya watu.”

13Lakini hakuna mtu yeyote aliyemsema waziwazi kwa sababu ya kuwaogopa viongozi wa Wayahudi.

Yesu afundisha kwenye Sikukuu

14Ilipokaribia katikati ya Sikukuu, Yesu alipanda kwenda Hekaluni na kuanza kufundisha.

15Wayahudi wakastaajabia mafundisho yake wakasema, “Mtu huyu amepataje kujua mambo haya bila kufundishwa?”

16Ndipo Yesu akawajibu, “Mafundisho yangu si yangu mwenyewe, bali yanatoka kwake yeye aliyenituma.

17Mtu yeyote akipenda kufanya mapenzi ya Mungu, atajua kama mafundisho yangu yanatoka kwa Mungu au ninasema kwa ajili yangu mwenyewe.

18Wale wanenao kwa ajili yao wenyewe hufanya hivyo kwa kutaka utukufu wao wenyewe. Lakini yeye atafutaye utukufu wa yule aliyemtuma ni wa kweli, wala hakuna uongo ndani yake.

19Je, Musa hakuwapa ninyi sheria? Lakini hakuna hata mmoja wenu anayeishika hiyo sheria. Kwa nini mnataka kuniua?”

20Ule umati wa watu wakamjibu, “Wewe una pepo mchafu! Ni nani anayetaka kukuua?”

21Yesu akawajibu, “Nimefanya muujiza mmoja na nyote mkastaajabu.

22Lakini kwa kuwa Musa aliwaamuru tohara (ingawa kwa kweli haikutoka kwa Musa bali kwa baba zetu wa zamani), mnamtahiri mtoto hata siku ya Sabato.

23Ikiwa mtoto aweza kutahiriwa siku ya Sabato kusudi sheria ya Musa isivunjwe, kwa nini mnanikasirikia kwa kumponya mtu mwili wake wote siku ya Sabato?

24Acheni kuhukumu mambo kwa jinsi mnavyoona tu, bali hukumuni kwa haki.”

Je, Yesu ndiye Kristo?

25Ndipo baadhi ya watu wa Yerusalemu wakawa wanasema, “Tazameni, huyu si yule mtu wanayetaka kumuua?

26Mbona yuko hapa anazungumza hadharani, na wala hawamwambii neno lolote? Je, inawezekana viongozi wanafahamu kuwa huyu ndiye Kristo?[#7:26 maana yake Masiya , yaani Aliyetiwa mafuta.]

27Tunafahamu huyu mtu anakotoka, lakini Kristo atakapokuja, hakuna yeyote atakayejua atokako.”

28Ndipo Yesu, akaendelea kufundisha Hekaluni, akisema, “Ninyi mnanifahamu na kujua nitokako. Mimi sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, bali yeye aliyenituma ni wa kweli na ninyi hammjui.

29Mimi namjua kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye alinituma.”

30Ndipo wakatafuta kumkamata, lakini hakuna mtu yeyote aliyethubutu kumshika kwa sababu saa yake ilikuwa bado haijawadia.

31Nao watu wengi wakamwamini, wakasema, “Je, Kristo atakapokuja, atafanya miujiza mikuu kuliko aliyoifanya mtu huyu?”

Walinzi wanatumwa kumkamata Yesu

32Mafarisayo wakasikia watu wakinongʼona mambo kama hayo kuhusu Yesu, ndipo wao pamoja na viongozi wa makuhani wakatuma walinzi wa Hekalu waende kumkamata.

33Yesu akasema, “Mimi bado niko pamoja nanyi kwa kitambo kidogo, kisha nitarudi kwake yeye aliyenituma.

34Mtanitafuta lakini hamtaniona, nami niliko ninyi hamwezi kuja.”

35Wayahudi wakaulizana wao kwa wao, “Huyu mtu anataka kwenda wapi ambako hatuwezi kumfuata? Je, anataka kwenda kwa Wayunani ambako baadhi ya watu wetu wametawanyikia, akawafundishe Wayunani?

36Yeye ana maana gani anaposema, ‘Mtanitafuta lakini hamtaniona,’ na, ‘nami niliko ninyi hamwezi kuja’?”

Mito ya maji ya uzima

37Siku ile ya mwisho ya Sikukuu, siku ile kuu, wakati Yesu akiwa amesimama huko, akapaza sauti yake akasema, “Kama mtu yeyote anaona kiu na aje kwangu anywe.

38Yeyote aniaminiye mimi, kama Maandiko yanavyosema, vijito vya maji ya uzima vitatiririka kutoka ndani yake.”

39Yesu aliposema haya, alimaanisha Roho Mtakatifu, ambaye wote waliomwamini wangempokea. Kwa maana hadi wakati huo Roho alikuwa hajatolewa, kwa kuwa Yesu alikuwa bado hajatukuzwa.

Mgawanyiko miongoni mwa watu

40Waliposikia maneno hayo, baadhi ya watu miongoni mwa umati ule wakasema, “Hakika huyu ndiye yule Nabii.”

41Wengine wakasema, “Huyu ndiye Kristo!”

Lakini wengine wakauliza, “Je, Kristo kwao ni Galilaya?

42Je, Maandiko hayasemi kwamba Kristo atakuja kutoka jamaa ya Daudi na kutoka Bethlehemu, mji alioishi Daudi?”

43Kwa hiyo watu wakagawanyika kwa ajili ya Yesu.

44Baadhi yao walitaka kumkamata, lakini hakuna aliyethubutu kumgusa.

Kutokuamini kwa viongozi wa Wayahudi

45Hatimaye wale walinzi wa Hekalu wakarudi kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo waliokuwa wamewatuma ili kumkamata Yesu, wakaulizwa, “Mbona hamkumkamata?”

46Wale walinzi wakajibu, “Kamwe hajanena mtu yeyote kama yeye anenavyo.”

47Mafarisayo wakajibu, “Je, nanyi pia mmedanganyika?

48Je, kuna kiongozi yeyote au mmoja wa Mafarisayo ambaye amemwamini?

49Lakini umati huu wa watu wasiojua Sheria ya Musa, wamelaaniwa.”

50Ndipo Nikodemo, yule aliyekuwa amemwendea Yesu siku moja usiku, na alikuwa mmoja wao, akauliza,

51“Je, sheria zetu zinaturuhusu kumhukumu mtu kabla ya kumsikiliza na kufahamu alilotenda?”

52Wakamjibu, “Je, wewe pia unatoka Galilaya? Chunguza nawe utaona kwamba hakuna nabii atokae Galilaya!”

[

53Kisha wakaondoka, kila mtu akarudi nyumbani mwake.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.