Ayubu 13

Ayubu 13

Ayubu anaendelea

1“Macho yangu yameona hili lote,

masikio yangu yamesikia na kulielewa.

2Hayo mnayoyajua mimi pia ninayajua;

mimi si mtu duni kuliko ninyi.

3Lakini ninayo shauku ya kuzungumza na Mwenyezi

na kuhojiana shauri langu na Mungu.

4Ninyi, hata hivyo, hunipakaza uongo;

ninyi ni matabibu wasiofaa kitu, ninyi nyote!

5Laiti wote mngenyamaza!

Kwa kuwa kwenu hilo lingekuwa hekima.

6Sikieni sasa hoja yangu;

sikilizeni kusihi kwangu.

7Je, mtazungumza kwa uovu kwa niaba ya Mungu?

Je, mtazungumza kwa udanganyifu kwa niaba yake?

8Mtamwonesha upendeleo?

Mtamtetea Mungu kwenye mashtaka yake?

9Je, ingekuwa vyema

Mungu akiwahoji ninyi?

Je, mngeweza kumdanganya kama ambavyo

mngeweza kuwadanganya wanadamu?

10Hakika angewakemea

mkiwapendelea watu kwa siri.

11Je, huo ukuu wake haungewatisha ninyi?

Je, hofu yake isingewaangukia ninyi?

12Maneno yenu ni mithali za majivu;

utetezi wenu ni ngome za udongo wa mfinyanzi.

13“Nyamazeni kimya nipate kusema;

kisha na yanipate yatakayonipata.

14Kwa nini nijiweke mwenyewe kwenye hatari

na kuyaweka maisha yangu mikononi mwangu?

15Ingawa ataniua, bado nitamtumaini;

hakika nitazitetea njia zangu mbele zake.

16Naam, hili litanigeukia kuwa wokovu wangu,

kwa maana hakuna mtu asiyemcha Mungu

atakayethubutu kuja mbele yake!

17Sikilizeni maneno yangu kwa makini;

nayo masikio yenu yaingize kile nisemacho.

18Sasa kwa kuwa nimekwisha tayarisha kesi yangu,

ninajua nitahesabiwa kuwa haki.

19Je, kuna yeyote anayeweza kuleta mashtaka dhidi yangu?

Kama ndivyo, nitanyamaza na nife.

20“Ee Mungu, unijalie tu mimi haya mambo mawili,

nami sitajificha uso wako:

21Ondoa mkono wako uwe mbali nami,

uache kuniogofya kwa vitisho vyako.

22Niite kwenye shauri nami nitajibu,

au niache niseme, nawe upate kujibu.

23Ni makosa na dhambi ngapi nilizotenda?

Nioneshe kosa langu na dhambi yangu.

24Kwa nini kuuficha uso wako

na kunihesabu mimi kuwa adui yako?

25Je, utaliadhibu jani lipeperushwalo na upepo?

Je, utayasaka makapi makavu?

26Kwa kuwa unaandika mambo machungu dhidi yangu

na kunifanya nizirithi dhambi za ujana wangu.

27Umeifunga miguu yangu kwenye pingu.

Unazichunga kwa makini njia zangu zote

kwa kutia alama kwenye nyayo za miguu yangu.

28“Hivyo mwanadamu huangamia kama kitu kilichooza,

kama vazi lililoliwa na nondo.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.