The chat will start when you send the first message.
1“Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke
siku zake ni chache nazo zimejaa taabu.
2Huchanua kama ua kisha hunyauka;
huwa kama kivuli kipitacho upesi, wala hadumu.
3Je, unamwekea jicho lako mtu kama huyo?
Je, utamleta mbele yako katika hukumu?
4Ni nani awezaye kutoa kitu safi kutoka kitu najisi?
Hakuna awezaye!
5Siku za mwanadamu zimewekewa mpaka;
umekwisha kutangaza idadi ya miezi yake
na kuweka mpaka ambao hawezi kuuvuka.
6Hivyo angalia mbali umwache,
hadi awe amekamilisha muda wake
kama mtu aliyeajiriwa.
7“Kwa maana lipo tumaini kwa mti;
kama ukikatwa utachipuka tena,
nayo machipukizi yake mapya hayatakoma.
8Mizizi yake yaweza kuchakaa ardhini
na kisiki chake kufa udongoni,
9lakini kwa kupata dalili ya maji utachipua
na kutoa machipukizi kama mche.
10Lakini mwanadamu hufa, na huo ndio mwisho wake;
hutoa pumzi ya mwisho, naye hayuko tena!
11Kama vile maji yanavyotoweka katika bahari,
au mkondo wa mto ukaushwavyo na kuwa mkavu,
12ndivyo mwanadamu alalavyo chini asiamke;
hadi mbingu zitakapokuwa hazipo tena,
wanadamu hawataamka au kuamshwa
kutoka usingizi wao.
13“Laiti kama ungenificha kaburini,[#14:13 Kaburini maana yake ni Kuzimu ; kwa Kiebrania ni Sheol.]
na kunisitiri hadi hasira yako ipite!
Laiti ungeniwekea wakati,
na kisha ukanikumbuka!
14Je, kama mtu akifa, aweza kuishi tena?
Siku zote za kazi zangu ngumu
nitangojea kufanywa upya kwangu.
15Utaniita nami nitakuitika;
utakionea shauku kiumbe ambacho mikono yako ilikiumba.
16Hakika ndipo utakapozihesabu hatua zangu,
lakini hutazifuatia dhambi zangu.
17Makosa yangu yatatiwa muhuri kwenye mfuko,
nawe utazifunika dhambi zangu.
18“Lakini kama mlima umomonyokavyo na kufikichika
na kama vile mwamba uondolewavyo mahali pake,
19kama maji yamalizavyo mawe,
na mafuriko yachukuavyo udongo,
ndivyo unavyoharibu tegemeo la mwanadamu.
20Humshinda mara moja kwa daima, naye hutoweka;
waibadilisha sura yake na kumwondoa.
21Kama wanawe wakipewa heshima, yeye hafahamu;
kama wazao wake wakidharauliwa, yeye haoni.
22Yeye hasikii kingine isipokuwa maumivu ya mwili wake mwenyewe,
naye huomboleza kwa ajili yake mwenyewe.”