Ayubu 42

Ayubu 42

Sehemu ya tano

Ayubu anamjibu Bwana

1Ndipo Ayubu akamjibu Bwana :

2“Ninajua ya kuwa unaweza kufanya mambo yote,

wala hakuna mpango wako unaoweza kuzuilika.

3Uliuliza, ‘Ni nani huyu

afichaye mashauri yangu

bila maarifa?’

Hakika nilisema mambo nisiyoyaelewa,

mambo ya ajabu mno

kwangu mimi kuyajua.

4“Ulisema, ‘Sikiliza sasa, nami nitanena;

nitakuuliza swali, nawe yakupasa kunijibu.’

5Masikio yangu yalikuwa yamesikia habari zako,

lakini sasa macho yangu yamekuona.

6Kwa hiyo najidharau mwenyewe,

na kutubu katika mavumbi na majivu.”

Mwisho: Rafiki zake Ayubu wanafedheheshwa

7Baada ya Bwana kusema mambo haya yote na Ayubu, akamwambia Elifazi Mtemani, “Nina hasira nawe na rafiki zako wawili, kwa sababu hamkusema yaliyo sawa kunihusu, kama alivyosema mtumishi wangu Ayubu.

8Basi sasa chukueni mafahali saba na kondoo dume saba mkamwendee mtumishi wangu Ayubu nanyi mkatoe sadaka za kuteketezwa kwa ajili yenu wenyewe. Mtumishi wangu Ayubu atawaombea, nami nitayakubali maombi yake ili nisiwatendee sawasawa na upumbavu wenu. Ninyi hamkusema yaliyo sawa kwa habari yangu, kama alivyosema mtumishi wangu Ayubu.”

9Kwa hiyo Elifazi Mtemani, Bildadi Mshuhi, na Sofari Mnaamathi wakafanya kama Bwana alivyowaambia; naye Bwana akayakubali maombi ya Ayubu.

10Baada ya Ayubu kuwaombea rafiki zake, Bwana akamwondoa kwenye uteka, akamfanikisha tena naye akampa mara mbili ya vile alivyokuwa navyo hapo mwanzoni.

11Ndipo ndugu zake na dada zake wote, na kila mtu aliyemfahamu mwanzoni wakaja, wakala pamoja naye katika nyumba yake. Wakamfariji na kumtuliza moyo juu ya taabu yote Bwana aliyoileta juu yake, nao kila mmoja akampa kipande cha fedha na pete ya dhahabu.

12Bwana akaibariki sehemu ya mwisho ya maisha ya Ayubu kuliko ile ya kwanza. Alikuwa na kondoo elfu kumi na nne, ngamia elfu sita, jozi za mafahali elfu moja, na punda jike elfu moja.

13Tena alikuwa na wana saba na binti watatu.

14Binti wa kwanza aliitwa Yemima, wa pili Kesia, na wa tatu Keren-Hapuki.

15Katika nchi ile yote hakukuwa wanawake wazuri kama binti za Ayubu; naye baba yao akawapa urithi pamoja na ndugu zao.

16Baada ya hili Ayubu akaishi miaka mia moja na arobaini; akawaona wanawe, na wana wa wanawe hata kizazi cha nne.

17Hivyo Ayubu akafa, akiwa mzee aliyeshiba siku.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.