Ayubu 7

Ayubu 7

Ayubu anaendelea

1“Je, mwanadamu hana kazi ngumu duniani?

Siku zake si kama zile za mtu aliyeajiriwa?

2Kama mtumwa anavyovionea shauku vivuli vya jioni,

au mtu aliyeajiriwa anavyoungojea mshahara wake,

3ndivyo nilivyogawiwa miezi ya ubatili,

nami nimeandikiwa huzuni usiku hata usiku.

4Nilalapo ninawaza, ‘Itachukua muda gani kabla sijaamka?’

Usiku huwa mrefu, nami najigeuzageuza hadi mapambazuko.

5Mwili wangu umevikwa mabuu na uchafu,

ngozi yangu imetumbuka na kutunga usaha.

Ayubu amlilia Mungu

6“Siku zangu zinapita upesi kuliko mtande wa kufuma,

nazo zinafikia mwisho wake bila matumaini.

7Kumbuka, Ee Mungu, maisha yangu ni kama pumzi;

macho yangu kamwe hayataona tena raha.

8Lile jicho linaloniona sasa halitaniona tena;

utanitafuta, wala sitakuwepo.

9Kama vile wingu liondokavyo na kutoweka,

vivyo hivyo yeye ashukaye kaburini harudi tena.

10Kamwe harudi tena nyumbani mwake;

wala mahali pake hapatamjua tena.

11“Kwa hiyo sitanyamaza;

nitanena kutokana na maumivu makuu ya roho yangu,

nitalalama kwa uchungu wa nafsi yangu.

12Je, mimi ni bahari, au yule mnyama mkubwa wa baharini,

hata uniweke chini ya ulinzi?

13Ninapofikiri kwamba kitanda changu kitanifariji,

nacho kiti changu cha fahari kitapunguza malalamiko yangu,

14ndipo wanitisha kwa ndoto

na kunitia hofu kwa maono,

15hivyo ninachagua kujinyonga na kufa,

kuliko huu mwili wangu.

16Ninayachukia maisha yangu; nisingetamani kuendelea kuishi.

Niache; siku zangu ni ubatili.

17“Mwanadamu ni kitu gani hata umjali kiasi hiki,

kwamba unamtia sana maanani,

18kwamba unamwangalia kila asubuhi

na kumjaribu kila wakati?

19Je, hutaacha kamwe kunitazama,

au kuniacha japo kwa kitambo kidogo tu?

20Ikiwa nimetenda dhambi, nimekufanyia nini,

Ewe mlinzi wa wanadamu?

Kwa nini umeniweka niwe shabaha yako?

Je, nimekuwa mzigo kwako?

21Kwa nini husamehi makosa yangu

na kuachilia dhambi zangu?

Kwa kuwa hivi karibuni nitalala mavumbini;

nawe utanitafuta, wala sitakuwepo.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.