Maombolezo 5

Maombolezo 5

1Kumbuka, Ee Bwana , yaliyotupata,

tazama, nawe uione aibu yetu.

2Urithi wetu umegeuziwa kwa wageni,

na nyumba zetu kwa wageni.

3Tumekuwa yatima wasio na baba,

mama zetu wamekuwa kama wajane.

4Ni lazima tununue maji tunayokunywa,

kuni zetu zapatikana tu kwa kununua.

5Wanaotufuatilia wapo kwenye visigino vyetu,

tumechoka na hakuna pumziko.

6Tumejitolea kwa Misri na Ashuru

tupate chakula cha kutosha.

7Baba zetu walitenda dhambi na hawapo tena,

na sisi tunachukua adhabu yao.

8Watumwa wanatutawala

na hakuna wa kutuokoa mikononi yao.

9Tunapata chakula chetu kwa kuhatarisha maisha yetu

kwa sababu ya upanga jangwani.

10Ngozi yetu ina joto kama tanuru,

kutokana na fadhaa ya njaa.

11Wanawake wametendwa jeuri katika Sayuni,

na mabikira katika miji ya Yuda.

12Wakuu wametungikwa juu kwa mikono yao,

wazee hawapewi heshima.

13Vijana wanataabika kwenye mawe ya kusagia,

wavulana wanayumbayumba chini ya mizigo ya kuni.

14Wazee wameondoka katika lango la mji,

vijana wameacha kuimba nyimbo zao.

15Furaha imeondoka mioyoni mwetu,

kucheza kwetu kumegeuka maombolezo.

16Taji limeanguka kutoka kichwani petu.

Ole wetu, kwa maana tumetenda dhambi!

17Kwa sababu hiyo, mioyo yetu inazimia,

kwa sababu ya hayo, macho yetu yamefifia,

18kwa sababu Mlima Sayuni umekaa ukiwa,

na mbweha wanatembea juu yake.

19Wewe, Ee Bwana unatawala milele,

kiti chako cha enzi chadumu kizazi hadi kizazi.

20Kwa nini watusahau siku zote?

Kwa nini umetuacha kwa muda mrefu?

21Turudishe kwako mwenyewe, Ee Bwana ,

ili tupate kurudi.

Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale,

22isipokuwa uwe umetukataa kabisa

na umetukasirikia pasipo kipimo.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.