Walawi 18

Walawi 18

Uhusiano wa kukutana kimwili kinyume cha Sheria

1Bwana akamwambia Musa,

2“Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.

3Msifanye kama wafanyavyo huko Misri, mahali mlipokuwa mnaishi, wala msifanye kama wanavyofanya katika nchi ya Kanaani, mahali ninapowapeleka. Msifuate matendo yao.

4Ni lazima mzitii sheria zangu, na mwe waangalifu kuzifuata amri zangu. Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.

5Zishikeni amri zangu na sheria zangu, kwa maana mtu anayezitii ataishi kwa hizo. Mimi ndimi Bwana .

6“ ‘Hakuna mtu yeyote atakayemsogelea ndugu wa karibu ili kukutana naye kimwili. Mimi ndimi Bwana .

7“ ‘Usimvunjie heshima baba yako kwa kukutana kimwili na mama yako. Yeye ni mama yako; usiwe na mahusiano kama hayo naye.

8“ ‘Usikutane kimwili na mke wa baba yako; hiyo itamvunjia heshima baba yako.

9“ ‘Usikutane kimwili na dada yako, wala binti ya baba yako, au binti ya mama yako, awe amezaliwa katika nyumba hiyo au mahali pengine.

10“ ‘Usikutane kimwili na binti ya mwanao ama binti ya binti yako; utajivunjia heshima.

11“ ‘Usikutane kimwili na binti ya mke wa baba yako, aliyezaliwa na baba yako; huyo ni dada yako.

12“ ‘Usikutane kimwili na dada wa baba yako; ni ndugu wa karibu wa baba yako.

13“ ‘Usikutane kimwili na dada wa mama yako, kwa sababu ni ndugu wa mama yako wa karibu.

14“ ‘Usimvunjie heshima ndugu wa baba yako, kwa kukutana kimwili na mke wake; yeye ni shangazi yako.

15“ ‘Usikutane kimwili na mkwe wako, yeye ni mke wa mwanao; usiwe na mahusiano kama hayo naye.

16“ ‘Usikutane kimwili na mke wa kaka yako; utamvunjia heshima kaka yako.

17“ ‘Usikutane kimwili na mwanamke kisha na binti yake. Usikutane kimwili na binti ya mwanawe au binti ya binti yake; hao ni ndugu zake wa karibu. Huo ni uovu.

18“ ‘Usimchukue dada wa mke wako kuwa mke mwenza, na kukutana naye kimwili wakati bado mke wako anaishi.

19“ ‘Usimsogelee mwanamke ili kukutana naye kimwili wakati wa unajisi wa siku zake za mwezi.

20“ ‘Usikutane kimwili na mke wa jirani yako na kujitia naye unajisi.

21“ ‘Usimtoe kafara mtoto wako yeyote kwa Moleki, kwani hutalinajisi kamwe jina la Mungu wako. Mimi ndimi Bwana .

22“ ‘Usikutane kimwili na mwanaume vile mwanaume anavyokutana kimwili na mwanamke; hilo ni chukizo.

23“ ‘Usikutane kimwili na mnyama na kujitia unajisi kwake. Mwanamke asijipeleke kwa mnyama ili kukutana naye kimwili; huo ni upotovu.

24“ ‘Msijitie unajisi kwa njia yoyote katika hizi, kwa sababu hivi ndivyo mataifa nitakayoyafukuza mbele yenu yalivyojitia unajisi.

25Hata nchi ilitiwa unajisi, hivyo nikaiadhibu kwa dhambi zake, nayo nchi ikawatapika wakazi wake.

26Lakini ni lazima mzitunze amri zangu na sheria zangu. Wazawa na wageni wanaoishi miongoni mwenu kamwe wasifanye mambo yoyote ya machukizo haya,

27kwa kuwa mambo haya yote yalifanywa na watu walioishi katika nchi hii kabla yenu, na nchi ikawa najisi.

28Mkiinajisi nchi, itawatapika kama ilivyowatapika mataifa yaliyowatangulia.

29“ ‘Kila mtu atakayefanya mojawapo ya machukizo haya, watu hao ni lazima wakatiliwe mbali na watu wao.

30Shikeni maagizo yangu, wala msifuate desturi za machukizo yoyote yaliyofanywa kabla hamjafika katika nchi hii, na kujitia unajisi kwa hayo. Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.’ ”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.