Walawi 2

Walawi 2

Sadaka ya nafaka

1“ ‘Mtu yeyote aletapo sadaka ya nafaka kwa Bwana , sadaka yake itakuwa ya unga laini. Atamimina mafuta juu yake, aweke uvumba juu yake,

2naye atapeleka kwa makuhani wana wa Haruni. Kuhani atachukua konzi moja unga laini na mafuta, pamoja na uvumba wote, na kuviteketeza kama sehemu ya kumbukumbu juu ya madhabahu, sadaka iliyotolewa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza Bwana .

3Sadaka ya nafaka iliyobaki ni ya Haruni na wanawe; ni sehemu ya sadaka iliyo takatifu sana iliyotolewa kwa Bwana kwa moto.

4“ ‘Kama utaleta sadaka ya nafaka iliyookwa, itakuwa ya unga laini: iwe maandazi yaliyotengenezwa bila kutiwa chachu, yaliyochanganywa na mafuta, au mikate myembamba iliyotengenezwa bila kutiwa chachu na iliyopakwa mafuta.

5Iwapo sadaka yako ya nafaka imeandaliwa kwenye kikaango, itakuwa ni ya unga laini uliochanganywa na mafuta, bila chachu.

6Vunjavunja na kumimina mafuta juu yake; hii ni sadaka ya nafaka.

7Ikiwa sadaka yako ya nafaka imepikwa kwenye sufuria, itatengenezwa kwa unga laini na mafuta.

8Ilete hiyo sadaka ya nafaka iliyotengenezwa kwa vitu hivi kwa Bwana ; mkabidhi kuhani, ambaye ataipeleka madhabahuni.

9Naye atatoa ile sehemu ya kumbukumbu katika hiyo sadaka ya nafaka, na kuiteketeza juu ya madhabahu kuwa sadaka iliyotolewa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza Bwana .

10Sadaka ya nafaka iliyobaki ni ya Haruni na wanawe; ni sehemu ya sadaka takatifu sana kati ya sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto.

11“ ‘Kila sadaka ya nafaka unayoleta kwa Bwana ni lazima ifanywe bila kutiwa chachu, kwa kuwa huna ruhusa kuchoma chachu yoyote au asali katika sadaka inayotolewa kwa Bwana kwa moto.

12Unaweza kuzileta kwa Bwana kuwa sadaka ya malimbuko, lakini haziwezi kutolewa juu ya madhabahu kama harufu nzuri ya kupendeza.

13Koleza sadaka zako zote za nafaka kwa chumvi. Usiache kuweka chumvi ya agano la Mungu wako katika sadaka zako za nafaka; weka chumvi kwenye sadaka zako zote.

14“ ‘Ukileta malimbuko ya sadaka ya nafaka kwa Bwana , utatoa masuke yaliyopondwa ya nafaka mpya iliyookwa kwa moto.

15Weka mafuta na uvumba juu yake; ni sadaka ya nafaka.

16Kuhani atateketeza ile sehemu ya kumbukumbu katika hiyo sadaka ya nafaka iliyopondwa, na mafuta, pamoja na uvumba wote, kuwa sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa moto.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.