The chat will start when you send the first message.
1“ ‘Ikiwa mtu anatoa sadaka ya amani, naye akatoa ngʼombe, akiwa dume au jike, atamleta mnyama asiye na dosari mbele za Bwana .
2Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha sadaka yake na kumchinja penye ingilio la Hema la Kukutania. Ndipo makuhani, wana wa Haruni, watanyunyiza damu ya huyo mnyama pande zote za madhabahu.
3Katika hiyo sadaka ya amani ataleta sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa moto: sehemu za ndani na mafuta yote yanayoungana nazo,
4figo zote pamoja na mafuta yaliyozifunika karibu na kiuno, na kipande kirefu cha ini; utayaondoa pamoja na figo.
5Kisha wana wa Haruni wataiteketeza juu ya madhabahu, juu ya ile sadaka ya kuteketezwa iliyo juu ya kuni zinazowaka; ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza Bwana .
6“ ‘Akitoa kondoo au mbuzi kutoka kundi kuwa sadaka ya amani kwa Bwana , atamtoa dume au jike asiye na dosari.
7Akimtoa mwana-kondoo, atamleta mbele za Bwana .
8Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha sadaka yake, naye atamchinja mbele ya Hema la Kukutania. Kisha wana wa Haruni watanyunyiza damu ya huyo mnyama pande zote za madhabahu.
9Katika hiyo sadaka ya amani ataleta dhabihu iliyotolewa kwa Bwana kwa moto: mafuta yake, mafuta yote ya mkia uliokatwa karibu na uti wa mgongo, mafuta yote yanayofunika sehemu za ndani au yale yanayounganika nazo,
10figo mbili pamoja na mafuta yanayozifunika yaliyo karibu na kiuno, na kipande kirefu cha ini, ambayo utayaondoa pamoja na figo.
11Kuhani ataviteketeza juu ya madhabahu viwe chakula, sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa moto.
12“ ‘Ikiwa sadaka yake ni mbuzi, ataileta mbele za Bwana .
13Ataweka mkono wake juu ya kichwa chake na kumchinja mbele ya Hema la Kukutania. Kisha wana wa Haruni watanyunyiza damu ya huyo mnyama pande zote za madhabahu.
14Katika ile sadaka anayotoa, atatoa hii sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana : mafuta yote yanayofunika sehemu za ndani na yale yanayoungana nazo,
15figo zote mbili pamoja na mafuta yaliyo juu yake karibu na kiuno, na kipande kirefu cha ini, ambayo atayaondoa pamoja na figo.
16Kuhani ataviteketeza juu ya madhabahu viwe chakula, sadaka iliyotolewa kwa moto, harufu nzuri. Mafuta yote ya mnyama ni ya Bwana .
17“ ‘Hili ni agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo, popote mnapoishi: Msile mafuta yoyote ya mnyama wala damu.’ ”