Walawi 6

Walawi 6

Kurudisha kilichochukuliwa

1Bwana akamwambia Musa:

2“Mtu yeyote akitenda dhambi, naye si mwaminifu kwa Bwana kwa kumdanganya jirani yake kuhusu kitu fulani alichokabidhiwa, au kimeachwa chini ya utunzaji wake, au kimeibwa, au kama akimdanganya,

3au akiokota mali iliyopotea na akadanganya kuihusu, au kuapa kwa uongo, au kama akitenda dhambi yoyote ambayo watu wanaweza kuitenda;

4wakati akitenda dhambi hizo na kuwa mwenye hatia, ni lazima arudishe kile alichokuwa amekiiba au amekichukua kwa dhuluma, au alichokuwa amekabidhiwa, au mali iliyokuwa imepotea akaipata,

5au chochote alichokuwa amekiapia kwa uongo. Lazima akirudishe kikamilifu, na aongeze sehemu ya tano ya thamani yake, vyote ampe mwenye mali siku ile anapeleka sadaka yake ya hatia.

6Kisha kama adhabu lazima amletee kuhani, yaani kwa Bwana , kuwa sadaka yake ya hatia, kondoo dume kutoka kundi lake asiye na dosari, mwenye thamani kamili.

7Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana , naye atasamehewa kwa kosa lolote katika mambo aliyoyatenda lililomfanya kuwa na hatia.”

Sadaka ya kuteketezwa

8Bwana akamwambia Musa:

9“Mpe Haruni na wanawe agizo hili: ‘Haya ndio masharti kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa: Sadaka ya kuteketezwa itabaki kwenye moto juu ya madhabahu usiku kucha, hadi asubuhi, nao moto lazima uwe unaendelea kuwaka juu ya madhabahu.

10Kisha kuhani atavaa mavazi yake ya kitani, pamoja na nguo za ndani za kitani mwilini wake, na aondoe majivu ya sadaka ya kuteketezwa ambayo moto umeteketeza juu ya madhabahu, na kuyaweka kando ya madhabahu.

11Kisha atayavua mavazi haya na kuvaa mengine, naye achukue yale majivu nje ya kambi na kuyapeleka mahali palipo safi.

12Moto ulio juu ya madhabahu lazima uwe unaendelea kuwaka; kamwe usizimike. Kila asubuhi kuhani ataongeza kuni na kupanga sadaka ya kuteketezwa juu ya moto, na kuteketeza mafuta ya wanyama wa sadaka za amani juu yake.

13Moto lazima uendelee kuwaka juu ya madhabahu mfululizo, kamwe usizimike.

Sadaka ya nafaka

14“ ‘Haya ndio masharti ya sadaka ya nafaka: Wana wa Haruni wataileta mbele za Bwana , mbele za madhabahu.

15Kuhani atachukua konzi moja ya unga laini na mafuta, pamoja na uvumba wote ulio juu ya sadaka ya nafaka, na kuteketeza sehemu hiyo ya kumbukumbu juu ya madhabahu kama harufu nzuri ya kumpendeza Bwana .

16Haruni na wanawe watakula sehemu iliyobaki, lakini italiwa bila kutiwa chachu mahali patakatifu, nao wataila katika ua wa Hema la Kukutania.

17Kamwe haitaokwa na chachu; nimewapa kama fungu lao la sadaka iliyotolewa kwangu kwa moto. Ni takatifu sana, kama vile ilivyo sadaka ya dhambi na ya hatia.

18Kila mwanaume mzao wa Haruni aweza kuila. Ni fungu lake milele la sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto kwa vizazi vijavyo. Chochote kinachozigusa kitakuwa kitakatifu.’ ”

19Tena Bwana akamwambia Musa,

20“Hii ni sadaka ambayo Haruni na wanawe wanapaswa kuleta kwa Bwana siku atakapopakwa mafuta: sehemu ya kumi ya efa ya unga laini kama sadaka ya kawaida ya nafaka. Nusu yake ataitoa asubuhi na nusu nyingine jioni.[#6:20 Sehemu ya kumi ya efa ni sawa na kilo moja.]

21Iandae kwa mafuta kwenye kikaango; ilete ikiwa imechanganywa vizuri, na utoe hiyo sadaka ya nafaka ikiwa imevunjwa vipande vipande kuwa harufu nzuri ya kumpendeza Bwana .

22Mwanawe atakayeingia mahali pake kama kuhani aliyepakwa mafuta ndiye atakayeiandaa. Ni fungu la milele la Bwana , nalo litateketezwa kabisa.

23Kila sadaka ya nafaka ya kuhani itateketezwa kabisa; kamwe haitaliwa.”

Sadaka ya dhambi

24Bwana akamwambia Musa,

25“Mwambie Haruni na wanawe: ‘Haya ndio masharti kwa ajili ya sadaka ya dhambi: Sadaka ya dhambi itachinjiwa mbele za Bwana mahali sadaka ya kuteketezwa huchinjiwa; ni takatifu sana.

26Kuhani anayeitoa ndiye atakayeikula; itakuliwa katika mahali patakatifu, katika ua wa Hema la Kukutania.

27Chochote kitakachogusa nyama yoyote ya hiyo sadaka kitakuwa kitakatifu; na kama damu ya hiyo sadaka itadondokea juu ya vazi, lazima ulifulie mahali patakatifu.

28Chungu cha udongo kitakachopikiwa nyama lazima kivunjwe, lakini kama imepikiwa kwenye chombo cha shaba, chombo hicho kitasuguliwa na kusuuzwa kwa maji.

29Kila mwanaume katika jamaa ya kuhani aweza kula nyama hiyo; ni takatifu sana.

30Lakini kila sadaka ya dhambi ambayo damu yake imeletwa ndani ya Hema la Kukutania kufanya upatanisho katika Mahali Patakatifu kamwe haitaliwa; lazima iteketezwe.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.