The chat will start when you send the first message.
1Katika siku ya nane, Musa akawaita Haruni na wanawe, na wazee wa Israeli.
2Akamwambia Haruni, “Chukua ndama dume kwa ajili ya sadaka yako ya dhambi, na kondoo dume kwa sadaka yako ya kuteketezwa, wote wawili wasiwe na dosari, nao uwalete mbele za Bwana .
3Kisha waambie Waisraeli: ‘Chukueni beberu kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na ndama na mwana-kondoo, wote wawili wawe wa umri wa mwaka mmoja, na wasio na dosari, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa,
4na pia maksai na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya amani, ili kutoa dhabihu mbele za Bwana , pamoja na sadaka ya nafaka iliyochanganywa na mafuta. Kwa kuwa leo Bwana atawatokea.’ ”
5Wakavileta vile vitu Musa alivyowaagiza mbele ya Hema la Kukutania, na kusanyiko lote wakakaribia na kusimama mbele za Bwana .
6Ndipo Musa akasema, “Hili ndilo Bwana alilowaagiza mlifanye, ili utukufu wa Bwana upate kuonekana kwenu.”
7Musa akamwambia Haruni, “Njoo madhabahuni utoe dhabihu ya sadaka ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa, kuwa upatanisho kwa ajili yako mwenyewe na kwa ajili ya watu. Kisha utoe sadaka ya upatanisho kwa ajili ya watu, kama vile Bwana alivyoagiza.”
8Hivyo Haruni akaja madhabahuni na kumchinja yule ndama kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili yake mwenyewe.
9Wanawe wakamletea damu, naye akachovya kidole chake katika hiyo damu, akaitia kwenye pembe za madhabahu, nayo damu iliyobaki akaimwaga chini ya madhabahu.
10Juu ya madhabahu akateketeza mafuta, figo na kipande kirefu cha ini kutoka hiyo sadaka ya dhambi, kama Bwana alivyomwagiza Musa.
11Akateketeza nyama na ngozi nje ya kambi.
12Kisha Haruni akachinja sadaka ya kuteketezwa. Wanawe wakamletea damu, naye akainyunyiza pande zote za madhabahu.
13Wakamletea sadaka ya kuteketezwa kipande kwa kipande, pamoja na kichwa, naye akaviteketeza juu ya madhabahu.
14Akasafisha sehemu za ndani na miguu, akaviteketeza juu ya sadaka ya kuteketezwa juu ya madhabahu.
15Kisha Haruni akaleta sadaka ile iliyokuwa kwa ajili ya watu. Akachukua yule mbuzi wa sadaka ya dhambi kwa ajili ya watu, akamchinja na kumtoa kwa ajili ya sadaka ya dhambi, kama alivyofanya kwa ile ya kwanza.
16Haruni akaleta sadaka ya kuteketezwa na kuitoa kama ilivyoelekezwa.
17Pia akaleta sadaka ya nafaka, akachukua konzi moja na kuiteketeza juu ya madhabahu, pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi.
18Akachinja maksai na kondoo dume kuwa sadaka ya amani kwa ajili ya watu. Wanawe Haruni wakampa ile damu, naye akainyunyiza pande zote za madhabahu.
19Lakini sehemu zile za mafuta ya yule maksai na ya yule kondoo dume, yaani mafuta ya mkia, yaliyofunika tumbo, ya figo na kipande kirefu cha ini,
20hivi vyote wakaviweka juu ya vidari, kisha Haruni akayateketeza hayo mafuta ya wanyama juu ya madhabahu.
21Haruni akaviinua vile vidari na paja la kulia mbele za Bwana ili viwe sadaka ya kuinuliwa, kama Musa alivyoagiza.
22Kisha Haruni akainua mikono yake kuwaelekea watu na kuwabariki. Naye baada ya kutoa dhabihu ya sadaka ya dhambi, sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya amani, akashuka chini.
23Kisha Musa na Haruni wakaingia kwenye Hema la Kukutania. Walipotoka nje, wakawabariki watu. Nao utukufu wa Bwana ukawatokea watu wote.
24Moto ukaja kutoka kwa uwepo wa Bwana , ukaiteketeza ile sadaka ya kuteketezwa, pamoja na sehemu ya mafuta yaliyokuwa juu ya madhabahu. Watu wote walipoona jambo hili, wakashangilia kwa furaha na kusujudu.