Luka 10

Luka 10

Yesu awatuma sabini na wawili

1Baada ya hayo, Bwana akawachagua wengine sabini na wawili, akawatuma wawili wawili katika kila mji na kila sehemu aliyokusudia kwenda baadaye.

2Akawaambia, “Mavuno ni mengi, lakini watendakazi ni wachache. Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, ili apeleke watendakazi katika shamba lake la mavuno.

3Nendeni! Tazama ninawatuma kama wana-kondoo katikati ya mbwa-mwitu.

4Msichukue mkoba, wala mfuko, wala viatu, na msimsalimu mtu yeyote njiani.

5“Mkiingia katika nyumba yoyote, kwanza semeni, ‘Amani iwe kwenu.’

6Kama kuna mtu wa amani humo, basi amani yenu itakuwa juu yake. La sivyo, itawarudia.

7Kaeni katika nyumba hiyo, mkila na kunywa kile watakachowapa, kwa sababu kila mtendakazi anastahili malipo yake. Msihamehame kutoka nyumba hadi nyumba.

8“Mkienda katika mji na watu wake wakawakaribisha, kuleni chochote kiwekwacho mbele yenu,

9waponyeni wagonjwa waliomo na waambieni: ‘Ufalme wa Mungu umewakaribia.’

10Lakini mkiingia katika mji, nao hawakuwakaribisha, tokeni mwende katika barabara zake mkaseme:

11‘Hata mavumbi ya mji wenu yaliyoshikamana na miguu yetu, tunayakungʼuta dhidi yenu. Lakini mjue kwamba ufalme wa Mungu umekaribia.’

12Ninawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa Sodoma kustahimili katika siku ile kuliko mji ule.

Onyo kwa miji isiyotubu

(Mt 11:20‑24)

13“Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingefanyika Tiro na Sidoni, miji hiyo ingekuwa imetubu zamani, kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu.

14Lakini itakuwa rahisi zaidi kwa Tiro na Sidoni kustahimili katika siku ya hukumu, kuliko ninyi.

15Nawe Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha! Utashushwa hadi Kuzimu.[#10:15 Kuzimu kwa Kiyunani ni Hades , yaani mahali pa wafu.]

16“Yeye awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi; naye awakataaye ninyi amenikataa mimi. Lakini yeye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma.”

17Wale sabini na wawili wakarudi kwa furaha, na kusema, “Bwana, hata pepo wachafu wanatutii kwa jina lako.”

18Yesu akawaambia, “Nilimwona Shetani akianguka kutoka mbinguni kama radi.

19Tazama nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge na juu ya nguvu zote za adui; wala hakuna kitu chochote kitakachowadhuru.

20Basi, msifurahi kwa kuwa pepo wachafu wanawatii, bali furahini kwa kuwa majina yenu yameandikwa mbinguni.”

Hakuna amjuaye Baba ila Mwana

(Mt 11:25‑27; 13:16‑17)

21Wakati huo Yesu akashangilia katika Roho Mtakatifu, akasema, “Nakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo. Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.

22“Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu. Hakuna mtu amjuaye Mwana ni nani ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ni nani ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.”

23Basi Yesu akawageukia wanafunzi wake akanena nao faraghani, akawaambia, “Heri macho yanayoona yale mambo mnayoyaona.

24Kwa maana nawaambia, manabii wengi na wafalme walitamani kuona yale mnayoyaona lakini hawakuyaona, na walitamani kusikia yale mnayoyasikia lakini hawakuyasikia.”

Mfano wa Msamaria mwema

25Wakati huo mtaalamu mmoja wa sheria alisimama ili kumjaribu Yesu, akamuuliza, “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”

26Yesu akamjibu, “Imeandikwaje katika Sheria? Kwani unasoma nini humo?”

27Akajibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote’; tena, ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’”[#10:27 Kum 6:5; #10:27 Law 19:18]

28Yesu akamwambia, “Umejibu vyema. Fanya hivyo nawe utaishi.”

29Lakini yule mtaalamu wa sheria, akitaka kujionesha kuwa mwenye haki, akamuuliza Yesu, “Jirani yangu ni nani?”

30Yesu akamjibu akasema, “Mtu mmoja alikuwa akiteremka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko, naye akaangukia mikononi mwa wanyangʼanyi. Wakampiga, wakaondoka, wakamwacha akiwa karibu kufa.

31Kuhani mmoja alikuwa akipitia njia ile, alipomwona huyo mtu, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani.

32Vivyo hivyo, Mlawi mmoja naye alipofika mahali pale, alimwona, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani

33Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa akisafiri alipomwona, alimhurumia.

34Akaenda alipokuwa na akasafisha majeraha yake kwa divai na mafuta, kisha akayafunga. Ndipo akampandisha kwenye punda wake, akampeleka hadi kwenye nyumba ya wageni na kumtunza.

35Kesho yake, yule Msamaria akachukua dinari mbili akampa yule mwenye nyumba ya wageni na kusema, ‘Mtunze, nami nirudipo nitakulipa gharama yoyote ya ziada uliyotumia kwa ajili yake.’[#10:35 Dinari mbili ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku mbili.]

36“Ni yupi basi miongoni mwa hawa watatu wewe unadhani ni jirani yake yule mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyangʼanyi?”

37Yule mtaalamu wa sheria akajibu, “Ni yule aliyemhurumia.”

Ndipo Yesu akamwambia, “Nenda, ukafanye vivyo hivyo.”

Yesu awatembelea Martha na Mariamu

38Ikawa Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakienda Yerusalemu, akaingia kwenye kijiji kimoja ambapo mwanamke mmoja aliyeitwa Martha alimkaribisha nyumbani mwake.

39Martha alikuwa na dada yake aliyeitwa Mariamu, ambaye aliketi chini miguuni mwa Bwana akisikiliza yale alikuwa akisema.

40Lakini Martha alikuwa akihangaika na maandalizi yote yaliyokuwa yafanyike. Martha akaja kwa Yesu na kumuuliza, “Bwana, hujali kwamba dada yangu ameniachia kazi zote mwenyewe? Basi mwambie anisaidie.”

41Lakini Bwana akamjibu, “Martha, Martha, mbona unasumbuka na kuhangaika na mengi?

42Lakini kunahitajika kitu kimoja tu. Mariamu amechagua kile kilicho bora, wala hakuna mtu atakayemwondolea.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.